Kauli Mbiu: Matumaini Mapya kwa Kizazi Kipya
Balozi Amina Salum Ali akiwaonyesha wanachi, waandishi wa habari na wanachama waliojitokeza kwa wingi kushuhudia tendo la kuchikua fomu ya kuwania kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Balozi Amina Salum Ali akiongea na mamia ya wanachama na wananchi waliojitokea kwa wingi ,mara baada ya kuchikua fomu ya kuwania kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
HOTUBA YA BALOZI AMINA SALUM ALI YA KUCHUKUA FOMU YA KUGOMBEA NAFASI YA RAIS WA JAMHURI WA MUUNGANO WA TANZANIA.
JUNI 3, 2015
- Ndugu wana habari
- Wananchi wote mnaonisikiliza
- Mabibi na Mabwana
Habari za mchana,
Niliyesimama hapa mbele yenu naitwa Amina Salum Ali.
Mimi ni mzaliwa wa Tanzania, kwa upande wa Zanzibar.
Ni Mtanzania Mzaliwa wa Zanzibar, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Ndugu zangu, nimewasili hapa mjini Dodoma kutoka Zanzibar ili kutimiza dhamira na kwa kweli nia na kusudio langu la siku nyingi la kukiomba chama changu cha CCM kinipatie fursa ya kuiongoza nchi yetu kama Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kutokana na azma hiyo, awali ya yote, hususan kabla ya tendo hilo la kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa katika nchi yetu na CCM, ni vizuri kwangu kuwaeleza kile ambacho kimekuwa kikinisukuma kuchukua fomu ya kuomba Chama changu cha CCM kiridhie na hivyo kubariki kusudio langu la kuiongoza nchi yetu katika awamu ya tano ya utawala katika nchi yetu.
Kwanza, mimi ni Mtanzania wa kuzaliwa na ni Mwanachama na mmoja wa wanachama waanzilishi wa_CCM-- ndio maana nachukulia fomu hapa makao makuu ya kitaifa ya CCM!
Kwa kipindi cha miaka takribani arobaini iliyopita nimebahatika kuwa mjumbe wa kamati mbalimbali ndani ya CCM kiasi ambacho kwa sasa naifahamu fika katiba yake na malengo kitaifa na kimataifa.
Pili, natambua kazi ya kuiongoza nchi si lele mama. Ni kazi kubwa inayohititaji nia ya kweli, uwezo, uzoefu, na uadilifu wa kutosha ukibarikiwa na kusimimiwa na Mwenyenzi Mungu. Kwa kutambua haya napenda kuuthibitia uma wa Watanzania kwa kupitie nyie Wanahabari kwamba:
Nia ya kuiongoza nchi yetu Ninayo, tena sana. Mtakumbuka mwaka 2000 nilijitokeza kuchukua fomu ya kukiomba Chama cha Mapinduzi (CCM) kinipatie fursa ya kuiongoza nchi yetu. Ombi langu kwa wakati ule halikuwa riziki. Kwa mara hii ya pili sasa, najitokeza tena ili kukiomba Chama cha Mapinduzi kinipatie fursa ya kutimiza nia yangu hiyo ya miaka ishirini iliyopita ya kuiongoza nchi yetu kama Raisi.
Ndugu zangu Wanahabari, Uwezo ninao wa kuihudumia nchi yetu katika nafasi hiyo ya juu kabisa ya kiutawala katika nchi yetu. Kwanza ninayo elimu ya kutosha kunipa kuyatambua, kuyaelewa na kuzifanyia kazi changamoto zilizopo nchini mwetu kwa sasa.
Uzoefu ninao: Aidha kwa ridhaa ya CCM na/au Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serilali ya Mapinduzi ya Zanzibar nimepata uzoefu, tena mkubwa, kwa kushiriki, kuhudumia au kuwakilisha nchi yetu katika nafasi za uongozi za kitaifa na kimataifa.
Ndugu zangu, mtakumbuka ule usemi maaraufu Rais John F. Kennedy, ambaye alikuwa Raisi wa 35 aliyetawala Marekani tangu mwaka 1961 hadi alipouwawa mwaka 1963, alipata kuwaambia Wamerekani wenzake: “Msiuulize Marekani iwafanyia Nini, Ila mjiulize mtaiifanyia nini Marekani.” Maneno hayo ya hayati Raisi Kennedy (Mungu amlaze vyema peponi) kwangu mimi yamekuwa yakinipa changamoto kubwa na kwa siku nyingi---ni kitu gani ninataka na ninaweza kuifanyia nchi yangu ili kuipatia maendeleo ya haraka ya watu na vitu..
Ndugu Wanahabari, kutaka kwangu kuiongoza nchi yetu si kutaka tu. Ila KUNATOKANA na kutambua vyema na kutaka kuchangia kuondokana na changamoto nyingi na kubwa za kiuchumi, kisiasa, na kijamiizilizopo nchini mwetu; na pili changamoto za kufanyia kazi kwa haraka zitokanazo na mashirikiano ya nchi yetu nan nchi nyingine vile vile mashirika ya Kimataifa.
Kati azma ya kuomba ridhaa ya kuiletea nchi yetu maendeleo, leo hii Nimeamua kuchukua fomu ya kuiomba CCM inipatie fursa ya kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa nina nia dhabiti, uwezo na uzoefu wa kutosha kabisa kusimamia sera na mikakati ya kupambana na changamoto za maendeleo zilizopo ili kulipatia Taifa letu maendeleo makubwa, ya juu na ya haraka.
Azma hiyo inawezekana kwanza, kwa kuyaendeleza na kusimamia yale yote mazuri ambayo yametokana na uongozi wa Serikali ya awamu ya nne; na pili, kwa kubuni sera, mikakati, mipango, sheria na taratibu mpya za kuendelea kuutayarisha uchumi wetu kukua na kufikia kuwa nchi ya kiwango cha kati au cha juu cha maendeleo ya watu na vitu. Tatu ni kuzipa kipaumbele sekta na maeneo ambayo yatachangia kutatua changamoto za kiuchumi, kisiasa, na kijamii zilizopo nchini mwetu. Maeneo hayo ni kama yafuatayo:
KUONGEZA KASI YA UKUAJI UCHUMI KWA KUPANGA UPYA VIPAUMBELE VYA MAENDELEO KWA KUTUMIA VIZURI RASILMALI ZA NCHI ILI ZIWANUFAISHE WANANCHI.
Tanzania ina rasilmali za kutosha kwa ajili ya leo na kwa kizazi kipya. Malengo ya serikali ni kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati.Ni dhahiri inaonesha kwamba kuna haja ya kuwa na mapinduzi ya kifikra na kimkakati kwa kupitia upya Dira yetu ya maendeleo 2025 kwa kuweka mikakati madhubuti ya kufanya mapinduzi ya kutufikisha kwenye uchumi wa kwanza katika mpango wa muda mrefu kupitia katika uchumi wa kati.
Kuna haja ya kuwa na chombo maalum cha kusimamia masuala ya uchumi na maendeleo katika nchi yetu. Chombo hicho maalum ambacho kitasimamiwa na uongozi wa juu kitaifa kitakuwa na jukumu la kutoa ushauri wa haraka kuhusu maeneo na aina ya uwekezaji unaohitajika ambao utachangia haraka kukua kwa uchumi na upatikanaji wa ajira nchini mwetu.
Pia chombo hicho kitasaidia sana kuondosha ucheleweshwaji wa maamuzi ya uwekezaji, kuondoa mikataba mibovu na ya hasara na isiyo na tija kwa taifa letu, na pia kitasaidia kuziba mianya ya rushwa na ufisadi. Naamini mashirikiana kati ya chombo hicho kipya cha uchumi na maendeleo na Tume ya Mipango kutachangia haraka ukuaji wa uchumi utakaomgusa kila Mtanzania.
kipaumbele kitawekwa kwa sekta zitakazochangia haraka na moja kwa moja kupunguza umasikini, kwa mfano, kilimo na viwanda, Kwa sababu hii Serikali itabuni njia bora za kukuza uhusiano kati ya uwekezaji na ukuaji wa viwanda na kilimo, kuanzia wakulima na wajasiriamali wadogo wadogo hadi wakulima na viwanda vikubwa vya kusindika mazao ya kilimo. Naamini, kwa kufanya hivyo kukua kwa uchumi na maendeleo ya kiuchumi yatawagusa wanachi kwa kuwapatia tija katika uzalishaji mali na hivyo kuwapatia kipato kingi na cha kutosha kujikimu na kuweka akibaya kujipatia mahitaji na huduma za msingi, kama vile afya, elimu, na makazi bora.
njia kuu za usafirishaji, ikijumuisha reli, barabara, na usafiri wa baharini na maziwa, ama zitafufuliwa au kujengwa upya ili ziweze kuchangia haraka kukua kwa uchumi na pia kulinda uchumi wetu dhidi ya mfumuko wa bei. Sisi sote tunatambua kwamba nchi yetu bado ina uhitaji mkubwa wa njia nzuri na salama za kusafirisha watu na mizigo. Naamini kwamba uimarishaji wa miundo mbinu ya usafirishaji utaongeza uhitaji wa bandari zetu katika nchi jirani na hivyo kutupatia fursa ya kupatia kipato na kuhimarisha mahusiano ya kidugu ambayo ni ya muda mrefu sasa.
KUPUNGUZA KWA KASI UMASKINI NA KUONGEZA AJIRA KWA VIJANA
Lengo hili nitalisimamia kama ifuatavyo:
Kubuni sera na mikakati ya kupunguza kwa kasi ndani ya muda mfupi umasikini unaowaathiri sehemu kubwa ya wananchi kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya 2025. Kuleta Mapinduzi ya dhati katika sekta muhimu zinazoleta maendeleo ya haraka kwa wananchi.
Mapinduzi hayo yatatokana na matumizi ya teknolojia za kisasa uzalishaji katika sekta zote kuu za kiuchumi, hususan kilimo, ufugaji, na uvuvi, ikisaidiwa sana na matumizi ya teknolojia ya mawasiliano, na kuwawezesha wakulima, wafugaji, na wavuvi waweze kuuza ndani na nje ya nchi na/au kuuzia viwanda vitakavyoanzishwa au vile vilivyopo nchini.
Kupunguza ukosefu wa ajira na kuongeza ukuaji wa uchumi kwa kukaribisha na kushirikiana na sekata binafsi katika kufufua viwanda vinavyotumia mali ghafi itokanayo na kilimo, mathalan, pamba, korosho, maziwa, matunda, na, alizeti. Pia nalenga kusimamia kuchakatwa kwa mali ghafi, madini na vito ili kuviongezea thamani kwa kutumia viwanda vilivyopo au vitakavyojengwa nchini mwetu. Ili kuchangia haraka upatikana wa ajira kwa vijana, hasa wanawake, viwanda vitakavyoanzishwa nchini mwetu vitasimamiwa au kuongozwa vyema ili view na mahusiano ya kiuchumi na yatakayoto chngamoto za uwezekezaji katika sekta na maeneo mengine ya nchi yetu.
KASI YA,UWEZESHWAJI KWA WANAWAKE NA FAMILIA.
KUTOA MATUMAINI MAPYA KWA KIZAZI KIPYA
Nchi yetu ina idadi kubwa ya wanawake. Takwimu zinaonesha idadi ya wanawake wote wa Tanzania ni takriban milioni 25, yaani zaidi ya nusu ya Watanzania wote, wanaohitaji kutambuliwa na kupewa fursa sawa kwa kushirikishwa kikamilifu katika upangaji wa matumizi ya rasilimali za kitaifa. Hili linawezekana kwa wanawake kushirikishwa au kuwezeshwa kushiriki katika mipango yote ya maendeleo ya kiuchumi kijammi na kisiasa hasa katika maeneo ya kutoa maamuzi yaayogusa jamii. Kwa hiyo basi, Serikali yangu itapigania kuondoa kasoro za mfumo dume ambao bado unachangia kudumaza huduma za msingi kwa wanawake, kwa mfano Elimu, ili tupate maendelo ya haraka.
Mimi ninaamini, kwa wingi wao, mkakati wa kumuendeleza na kuwainua kimaendeleo mwanamke wa Kitanzania utakuwa ni njia nzuri pia ya kuwainua Watanzania kutoka katika ufukara wa kipato, kielimu, n.k. Usemi uliotawala kati yetu ambao ni wa kuuzingatia ni kwamba: Ukimwendeleza mwanamke utakuwa umeendeleza jamii.
KUKUZA UTOAJI WA HUDUMA ZA JAMII KWA USAWANA KWA WOTE
Kwa miaka takriban 50 sasa nchi yetu bado inagubikwa na tatizo la huduma duni kwa jamii, kwa mfano utoaji wa afya na kinga za mama na mwana ili kupunguza vifo vya wazazi na watoto walio chini ya miaka mitano.
Ukosefu wa huduma muhimu katika utoaji wa afya na kinga za mama na mwana ili kupunguza vifo vya wazazi na watoto walio chini ya miaka mitano. Serikali imechukua hatua kubwa sana za kupeleka huduma za afya kwa wanachipia imejitahidi kutafuta ufumbuzi wa kushughulikia matatizo ya sekta hii. Hata hivyo bado hatua za ziada zinahitajika hususan kwa kuwekeza katika hospitali zetu kwa kuwa na zana zinazohitajika na pia kuwa nadawa ya kuwahudumia wagonjwa wanapo hitaji.suala la madaktari na wafanya wa sekta ya afya ni la msingi kabisa ni muhimu kutafuta mkakati wa kuwapa motisha na vitendea kazi waweze kutoa huduma muafaka.hivyo kero walizo nazo ni muhimu zipatiwe ufumbuzi wa haraka.sera ya afye kwa wote itizamwe upya na iwe ni sekta ya uwekezaji badala ya mtizamo wa sasa kwamba ni kitengo cha huduma kwa wananchi kwa misingi hiyo utaratibu maalum uwepo wa kuongeza mtaji katika sekta hii ya afya kwa kuwasajiisha wawekezaji wan je na ndani kuwekeza kwa kujenga hospitali za kisasa ,zenye vifaa vya kisasa vya kutolea huduma na watendaji mabingwa ambao hivi sasa tunao ambao wengi wao wamevunjika moyo .
Pia kushajiisha vituo vya utafiti vya masuala ya afya na huduma mbali mbali. Vifo vya mama na mtoto vimepunguwa lakini bado vinahitaji vipunguzwe Zaidi. Kwa hiyo basi kuna sababu za kimsingi kabisa za kusimamia vyema au kubuni sera na mikakati bora zaidi itakayopelekea kuwepo nchiniu upatikanaji wa huduma bora za jamii, kwa usawa, kwa wote na kwa unafuu.
MGAWO BORA WA PATO LA TAIFA
Kwa miaka kumi iliyopita pato la nchi yetu limekuwa likiuwa kwa kiwango kinachoridhisha. Hata hivyo, ukuaji huo wa pato la taifa haujaambatana na kuwaletea maisha bora Watanzania walio wengi. Taifa letu limekuwa sasa kama linakubikwa na hulka ya aliyenacho kutojali au kumjua asienacho angali tofauti ya kipato na maisha kati ya Watanzania ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwangu mie tofauti hiyo kubwa ya kipato katika jamii ya Kitanzania ni hatari kwa mustakbali wa umoja wa kitaifa na amani na utulivu wa kuletea nchi yetu maendeleo.
Kuna sababu ya kimsingi inayohitaji utekelezaji wa haraka wa kuwepo mgawo bora wa pato la taifa ili Mtanzania wa kawaida aweze kujikimu kimaisha. Hili linawezekana kwa Serikali kurekebisha viwango vya kodi zinazolipwa na watu wa kipato cha chini; kwa Serikali kusimamia vyema sekta binafsi ilipe kodi stahiki na kwa viwango vilivyowekwa; kubuni sera na taratibu bora zaidi za kuiendesha na kuiwezesha mifuko ya inayowahudumia wastaafu; na kubuni na kuendesha mifuko ya kuwahudumia wazee, kina mama walioachiwa majukumu makubwa kutokana na kuwapoteza wenzi wao aidha kwa ajali, ukimwi, n.k.;
Utaratibu huu utafanikiwa kwa kuangalia upya ulipaji na ukusanyaji wa kodi na kwa kuwa na njia nyingine za mapato. Vile vile ni tutaangalia upya ulipaji wa kodi wa walipaji wa kipato cha chini ili kudhihirisha azma yetu ya kuwa Taifa linalojali watu wake, wakiwemo wanawake, vijana, wazee, walemavu wote, ikijumuisha wale wenye ulemavu wa ngozi. Vipofu, viziwi, mtindio wa ubongo, n.k. Katika uongozi wangunitatoa kipaumbele kwa kupunguza tofauti hizo na kuwaangalia kwa kina maskini na wenye vipato vya chini walio wengi kwa kuwapatia uwezo na njia mbadala za kuweza kukimi maisha.
ELIMU
Kuporomoka kwa ubora wa elimu katika ngazi zote ni changamoto kubwa nchini mwetu. Sehemu kubwa ya wahitimu wetu wamekuwa wasio na uwezo au elimu ya kutosha kupata au kuijipatia ajira wao wenyewe ili waweze kujikimu kimaisha, Vile vile elimu yao haiwawezeshi kukabili kikamilifu ushindani katika soko la ajira ndani nan je ya nchi yetu.
Wakati umefika sasa wa kuinua kiwango cha elimu kwa kuangalia upya mitaala ya kufundishia na kuwaandaa vyema waalimu bora na wa kutoosha kufundisha kuanzia elimu ya chekechea hadi ya vyuo vya elimu ya juu.
Kwa serikali kusimamia vyema na haraka uwepo wa kiwango bora cha Elimu tutakuwa tumewaongezea vijana wetu uwezo wa kuajiriwa humu humu nchini au nchi nyinginezo zilizo ndani na nje ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Serikali yangu itapigana kuvutia wawekezaji makini au itashirikiana na sekta binafsi kuwekeza katika elimu.
Vipa umbele vitapewa katika elimu itakayojenga vipaji na na kuwaongezea wahitimu utaalam wa kutosha na unaohitajiwa katika taifa, hususan kwenye sekta mpya za mafuta na gesi asilia; kuwapatia elimu ya stadi maalum; kuongeza wataalam na mabingwa wa fani mbali mbali kwa wakati tulionao ili uchumi ukue kwenda uchumi wa kwanzakupitia wa kati. Hii itawezekana kwa kubuni mitaala ya kuwafundishia wataalaa njia bora za kufundishia na kuwafundisha watoto wetu ujasiriamali ili waweze kujiajiri pale wamalizapo masomo.
UTAWALA WA SHERIA
Kuweka mazingira bora ya kisheria ya kuwezesha uwekezaji katika uzalishaji mali na kuendesha biashara na miradi mikubwa nchini mwetu ili kukuza haraka ukuaji uchumi na kushinda vita dhidi ya umaskini. Ingawaje sote tunakubali mchango wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi wan chi yetu, sekat hiyo inahitaji kusimamiwa vyema kwa wawekezaji wa nje kuwekewe mazingira mazuri na utaratibu maalum kwanza wa kuwekeza na pili kuingia ubia na wawekezaji wa ndani katika utekeleza wa miradi mikubwa ya kitaifa.
Pia inabidi sasa kuwa na sheria zilizo za wazi ambazo zitawapatia wawekezaji wa ndani utaratibu wa kurahisisha shughuli zao. Ili ili litokee, Serikali yangu itajikita kusimamia vyema, au kuzifanyia mapitio yatakayolenga kuboresha na ikibidi kubuni sheria mpya za uwekezaji na kusimamia uendeshaji wa biashara ambazo zitaendana na mfumo wa uchumi utakaoendana na dira ya maendeleo ya taifa .
ULIPAJI NA UKUSANYAJI KODI
Takwimu za kitaifa zinaonyesha bayana kushuka kwa ukusanyaji wa kodi nchini mwetu mwaka hadi mwaka tangu mwishoni mwa miaka ya tisini (1990s). Mapungufu ambayo yamekuwa yakijitokeza katika ukusanyaji wa kodi yamekuwa yakileta adha nyingi kwa serikali n ahata watanzania, kwa mfano, kushuku au kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii, kuchelewa kwa mitihani, kutopatikana kwa haraka mikopo ya wanafunzi, wakulima kutolipwa mapema mauzo ya mazao yao, n.k.
Serikali yangu itaimaarisha vyombo, taratibu na sheria zinazosimamia ukusanyaji wa kodi na mapato mengineyo. Aidha sheria mpya au zilizopo zitasimamiwa kwa ukali na busara ili kufuta kabisa nchini ukwepaji wa kodi. Sambamba na hili kwa Kuweka mazingira bora ya kisheria. Serikali itaweka utaratibu mzuri wa kukusanya kodi na pia kupitia upya maeneo ya vyanzo vya kodi, kuweka uwazi katika ukusanyaji wa kodi ,kuwa na viwango vya kodi vinavyotabirika na vinavyoendana na ukuaji wa uchumi na huduma mbali mbalikuboresha utendaji katika idara za mapatokwa kuwa na ufuatiliaji na ukusanyaji taarifa za wakwepaji wa kodi na kuchukuliwa hatua kali za kuwabana na kuwaadhibu..
RUSHWA, UFISADI, UWAJIBIKAJI NA UKOSEFU WA MAADILI
Rushwa, ufisadi, uwajibikaji usioridhisha, na ukosefu wa maadili ni mambo ya msingi kwa taifa linalofuata sera ya uwazi na utawala bora na maadili mema. Tanzania imeingia doa sana kutokana na kugubikwa na vitendo vya ufisadi, rushwa, na mapungufu makubwa ya ukosefu wa uadilifu na uwajibikaji serikalini takriban katika ngazi zote.
Mimi naamini, Serikali ni lazima iwe inawahudumia wananchi wake wote kwa kusimamia upatikanaji wa huduma bila ya ufisadi na vitendo vya rushwa. Kwa kufanya hivyo, wananchi watakuwa na imani na serikali yao. Kwa bahati mbaya vitendo ambavyo vimekuwa vikiendelea hivi sasa ni vile vya kulindana, kupendeleana, kutofuata maadili ya uongozi.
Kazi kubwa iliyopo mbele ya serikali nitakayounda ni ya kupiga vita rushwa, ufisadi, ukosefu wa uwajibikaji kazini, ukosefu wa maadili serikalini na ndani ya jamii yetu. Vita hivyo ni vigumu na vinahitaji moyo na kuungwa mkono na watanzania wote wenye uchungu na nchi yao. Vita hivyo vitajumuisha kuwepo usimamiaji mzuri na wa karibu wa vyombo vya kusimamia maadili kwa kuvipa pia meno na kupitia upya sheria zake.
Mahakama maalum itawekwa ya kushughulikia masuala yote ya rushwa na ufisadi na ubadhirifu wa mali za uma ili sheria kali na stahiki zitolewe kuadabisha wahusika wawe na adabu na kuwa fundisho kwa wengine. Njia hizi ni lazima ziwepo ili tuweze kujenga tabia na utamaduni mpya wa kuchukia rushwa, uzembe, na ufisadi na pia kuweka misingi ya watu kujitegemea na kuishi kwa kutumia njia halali za kujipatia kipatao badala ya kutajirika haraka kwa ufisadi na hongo.
MUUNGANO NA KATIBA
Nikipewa ridhaa na chama change cha CCM nitaendeleza mchakato wa kupata katiba mpya ambao ulisimamiwa na serikali ya awamo ya nne.Mimi ni muumini wa uhakika wa utawala bora kwa kuamini kuwa katiba inahitaji ridhaa ya wananchi na ndio makubaliano yanayowekwa ili kiongozi wanch na utawala unatakiwa uyatekeleze.Hivyo katiba iliyo bora itatuvusha taifa letu kwenda katika hali ya juu ya maendeleo na amani na utulivu. Katika katiba ni vyema masuala ya liokuwa kero yanaondosha ili kuwa na muungano imara .
Muungano ni muhimu sana kwa taifa letu la Tanzania bado ipo haja ya kuufanya upendwe na wanachi ili wajisikie kuwa ni wahusika na wadau wakuu wa kuulinda usivunjike na kupitishwa kwenye misuko suko isio na manufaa na tija.kuwepo na mikakati maalum ya kufanya mambo yatakayo fanya wananchi wa pande zote mbili wafaidike na waone faida ya kuwa jamii moja .naelewa hii sio kazi rahisi inahitaji nia na dhamira ya makusudi ya kuona mungano unadumu.mimi nimekulia ndani ya muungano , nimefanya kazi ndani ya muungano katika serikali zote mbili nnaelewa change moto ziliopo na zitakazo endelea kuwepo.Mara nyingi ni vikwazo visivyo vya msingi vinazuia kuimarika muungano wetu .binafsi ni muumini kabisa wa hatima ya Tanzania yenye maendeleo ndani ya mungano uliopo. Ndio maisha yetu na maendeleo ya vizazi vyetu.
LUGHA
Lugha ya Kiswahili inayotumika nchini mwetu kwa ajili ya mawasiliano ya aina mbali mbali n ahata kufundisha katika shule nchini mwetu ni moja ya tunu na nguzo zinazotuweka kuwa taifa letu moja lenye umoja, upendo, na mshikamano ambao umetupatia kuwa na amani na usalama nchini mwetu kwa muda mrefu sasa. Kwa sabau huu pekee Kiswahili kinatakiwa kiendelezwe kudumishwa kama lugha ya Taifa letu. Hata hivyo kutokana na kuongezeka kwa mashirikiano ya kibiashara, kisiasa na kitamaduni kati ya nchi yetu na nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara inabidi pia tusimamie ufundishaji bora wa Kiswahili ili kiwe nyenzo ya kuwapatia vijana wetu ajira, mathlan, kwa kuajiriwa kufundisha, kutoa huduma ya ukalimani, au kwa kuwekeza katika miradi ya shule za kufundisha Kiswahili hapa ndani na nje ya nchi yetu kwa
MUSTAKABALI WA KITAIFA
Tanzania inapita katika kipindi kigumu. Taifa letu lina mpasuko katika misingi ya dini, ukabila, ukanda, uhasama utokanao na ufuasi wa vyama vya kisiasa, hasa katika vipindi vya uchaguzi. Hali hii inatishia mustakabali mzima wa taifa na maendeleo ya nchi yetu. Wakati umefika sasa wa kukemea kwa nguvu zote na kuweka sheria zitakazoleta na kukuza masikilizano, malumbano, na mashauriano ya amani ambayo yatajenga na kudumisha umoja wa kitaifa katika nchi yetu. Naamini kwamba umoja wa kitaifa utawezesha taifa letu kufanya mambo makubwa ya kujenga uchumi imara na endelevu ambao utapunguza sanaumasikini.
Tukumbuke pia kwamba kwa muda mrefu nchi yetu ilijikita kusimamia upatikanaji wa uhuru katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara. Ni wakati muafaka sasa wa kurudisha hadhi ya taifa letu katika usikani wa uongozi na kusukuma upatikanaji wa maendeleo katika ukanda Afrika na ulimwengu kwa ujumla.
HITIMISHO
Ndugu wana habari napenda kuhitimisha kwa kusema kwamba kama nikipata ridhaa wa kuwa mgombea wa CCM na baadaye kura zikatosha katika kinyang’anyiro cha nafasi ya Uraisi wan chi yetu nitapigania kwa nguvu zote maendeleo ya nchi yetu, yaliyoegemea kupunguza umaskini, kukuza upatikanaji bora, kujenga miundo mbinu bora, kujenga na kusimamia utawala wa sharia. Serikali nitakyoiunda haitamuonea mtu asie na hatia na haitampendelea mtu kwa sababu za urafiki, ukanda, ukabila, udini na jinsia. Vile vile serikali hiyo haitavumilia hata kidogo vitendo vya uvunjaji amani na usalama na vitendo vya rushwa na hujuma wataifa na uvujaji au matumizi mbaya wa rasilimali za nchi yetu kutokana na mikataba mibovu. Hatua madhubuti zitachukuliwa kwa wakati ili kutoa haki stahiki bila ya kuchelewa. Naamini kwamba inabidi sasa tuanze tena kujenga utaifa, uzalendo na utamaduni wa uadilifu, na uwajibikaji katika nchi yetu.
Kauli Mbiu: Matumaini Mapya kwa Kizazi Kipya
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika, Mapinduzi Daima.
Balozi Amina Salum Ali akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa timu yake ya kampeni.
Balozi Amina Salum Ali akiongea na mamia ya wanachama na wananchi waliojitokea kwa wingi ,mara baada ya kuchikua fomu ya kuwania kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Balozi Amina Salum Ali akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya CCM Wilaya ya Dodoma Mjini.
Wadhamini waliojitokeza kwa wingi katika Ofisi CCM Wilaya ya Dodoma kwa ajili kumdhamini Balozi Amina Salum Ali.
Balozi Amina Salum Ali akiwasili makao ya CCM kuchukua fomu ya kuwania kuteuliwa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baadhi Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Baadhi ya Viongzi wa Chama Cha Mapinduzi , Makao Makuu mjini Dodoma.
Waandishi wa habari wakiwa kazini.
Mmoja wa waandishi wa habari akimuuliza swali Balozi Amina Salum Ali mara baada ya kusoma hotuba yake.
Mtangazaji maarufu wa Televisheni ya Tanzania (TBC) akimuuliza maswali Balozi Amina Salim Ali.
Balozi Amina Salum Ali akiwa na Makongoro Nyerere katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM Mkoani Dodoma, walipokutana kuchukua fomu ya kuwania kuteuliwa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa tanzania.
Balozi Amina Salum Ali akilakiwa na baadhi ya Wanachama na mashabiki wa CCM Wilaya ya Dodoma mjini , mara baada ya kuwasili katika viwanja vya ofisi hizo.
Balozi Amina Salum Ali akilakiwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma mjini , mara baada ya kuwasili katika viwanja vya ofisi hizo.
Balozi Amina Salum Ali akilakiwa na baadhi ya viongozi wa CCM Wilaya ya Dodoma mjini , mara baada ya kuwasili katika viwanja vya ofisi hizo.
Balozi Amina Salum Ali akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi Wilya ya Dodoma Mjini.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini akitoa nasaha na kumkaribisha Balozi Amina Salum katika Ofisi ya CCM Wilayani hapo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini akisaini fomu ya kuwania urais, mara baada ya zoezi la kudhamini kumalizika.
Balozi Amina Salum akiongea umati wa Wanachama na wananchi waliojitokeza kumdhamini ,katika ofisi za CCM Wilaya ya Dodoma Mjini.