Mkurugenzi Uzalishaji Maji wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA } Mhandisi Moh’d Elyas aliyenyanyua mkono akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kazi zilizobakia katika kukamilisha Miundombinu ya ujenzi wa kisima cha Maji safi katika Kijiji cha Kinduni Wilaya ya Kaskazini “B”.
Balozi Seif akizungumza na Wananchi na wana Saccos wa Kijiji cha Kinduni baada ya kukagua harakati za ujenzi wa Kibanda pamoja na Kisima cha Maji katika Kijiji hicho pamoja kutekeleza ahadi aliyotoa kwa kikundi hicho ya kusaidia matofali na saruji kwa ujenzi wa Jengo lao.
Balozi Seif akimkabidhi Mwenyekiti wa Kikundi cha Saccos cha Kijiji cha Kinduni Nd. Abdulla Mihando mchango wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa saruji na matofali akitekeleza ahadi aliyoitoa kwa kikundi hicho hivi karibuni.Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Kisima cha maji safi na salama kilichochimbwa na Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA } katika Kijiji cha Kinduni Wilaya ya Kaskazini “B” chenye uwezo wa kuzalisha Maji Lita elfu 80,000 kwa saa kinatarajiwa kuwakomboa Wananchi wa eneo hilo pamoja na Vijiji vya jirani kupata huduma hiyo muhimu.
Uchimbwaji wa Kisima hicho utaleta faraja kwa Wananchi wa Kijiji cha Kindumi ambapo wataondokana na tatizo sugu la upatikanaji wa huduma hiyo katika muda si mrefu ujao baada kukamilika kwa kazi ndigo ndogo zilizobakia.
Mkurugenzi wa Uzalishaji Maji wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA } Mhandisi Moh’d Elyas alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyefika eneo hilo kukagua harakati za ujenzi wa Kibanda cha Maji katika Kisima hicho aliougharamia kwa lengo la kuwaondoshea tatizo la maji Wananchi hao.
Mhandisi Moh’d alisema kwamba kazi ya kukamilisha miundombinu iliyobakia katika eneo hilo inaweza kuchumuwa muda wa wiki moja mara tuu baada ya upatikanaji wa huduma za umeme katika eneo hilo.
“ Ikipatikana huduma ya Umeme katika Kibanda chetu hichi tuna uwezo wa kukamilisha kazi iliyobakia ya kuunganisha umeme na mabomba ya maji ndani ya wiki moja “. Alisema Mhandisi Elyas.
Alisema wahandisi wa Mamlaka ya Maji watalazimika kuweka Pampu ndogo kwa wakati huu kulingana na Transfoma iliyopo jirani na eneo hilo licha ya kwamba kisima hicho kina uwezo wa kusambaza huduma za maji safi hadi katika Kijiji cha Kinyasini endapo itafungwa Mota kubwa.
Akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Kinduni pamoja na wana saccos ya Kijiji hicho Balozi Seif ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope alisema kazi za Wawakilishi na Wabunge wakati wote ni kuwatumikia Wananchi.
Balozi Seif alisema katika kutekeleza wajibu huo aliwaahidi Wananchi hao kuchukuwa hatua za kugharamia usambazaji wa mabomba ya maji katika vitongoji vya Kijiji hicho.
Aliwashukuru Wananchi wa Kijiji cha Kinduni pamoja na Vitongoji vyake kwa ustahamilivu wao mkubwa waliouchukuwa wa kukosa huduma hiyo kwa kipndi kirefu.
Katika ziara hiyo Balozi Seif alikabidhi fedha Taslimu kutekeleza ahadi aliyoitoa hivi karibuni kwa Kikundi cha Saccos cha Kijiji cha Kinduni ya kuchangia Matofali pamoja na saruji kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la wana saccos hao.
Mapema Diwani wa Wadi ya Mgambo Bibi Pili Said Mbonde kwa niaba ya Wananchi wa Kijji hicho amemshukuru Balozi Seif kwa jitihada zake zilisaidia kuondosha tatizo la miaka mingi la Wananachi hao.
Bibi Pili alisema ukosefu wa huduma za maji safi na salama kwa takriban miaka Minane katika eneo hilo umechangia kuviza maendeleo na huduma zao za lazima za kila siku.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
20/7/2015.