Home » » Balozi Seif akabidhiwa fomu na Afisa wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar {ZEC } Wilaya ya Kaskazini “B”

Balozi Seif akabidhiwa fomu na Afisa wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar {ZEC } Wilaya ya Kaskazini “B”

Written By CCMdijitali on Monday, August 17, 2015 | August 17, 2015





Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisalimiana na baadhi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi mara baada ya kuchukuwa fomu za kuwania Uwakilishi Jimbo la Mahonda hapo Ofisi ya Tume ya Uchaguzi Wilaya ya Kaskazini B iliyopo Mahonda.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikabidhiwa Fomu za kuwania nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Jimbo la Mahonda kutoka kwa Afisa wa Uchaguzi
Wilaya ya Kaskazini B Ndugu Makame Pandu Khamis.


Afisa wa Uchaguzi Wilaya ya Kaskazini B Nd. Makame Pandu Khamis akitoa maelezo kumpatia Balozi Seif ya namna ya ujazaji wa fomu za kuwania Uwakilishi Jimbo la Mahonda Ofisini kwake Mahonda Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unaguja.
Picha na – OMPR – ZNZ.

 Press Release:-

Wanachama mbali mbali wa Vyama vya Siasa Nchini walioomba na kuthibitishwa na vyama vyao kuwania nafasi mbali mbali za uongozi wameanza rasmi kujitokeza kuchukuwa fomu za kuwania kugombea nafasi walizoomba katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi za Wilaya.

Zoezi hilo litalowashirikisha wagombea nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani linatarajiwa kuendelea hadi Tarehe 6 Septemba 2015 ambapo wanaochukuwa fomu hizo watalazimika kujaza vipengele vyote vinne vilivyomo kwenye Fomu hizo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikuwa miongoni mwa wanachama kadhaa wa Chama cha Mapinduzi waliojitokeza kuchukuwa Fomu hizo ambapo yeye ameamuwa kugombea nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishgi Jimbo la Mahonda.

Balozi Seif alikabidhiwa fomu hizo mapema asubuhi na Afisa wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar {ZEC } Wilaya ya Kaskazini “B” Ndugu Makame Pandu Khamis hapo ilipo ofisi hiyo Mahonda Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Akikabidhi fomu hizo Afisa huyo wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Wilaya ya Kaskazini B Ndugu Makame Pandu Khamis amethibitisha kwamba Balozi Seif Ali Iddi ni Mgombea halali wa kuwania nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Mahonda kupitia CCM.

Nd. Makame alisema kwamba uhalali huo unatokana na Ofisi yake kupokea barua rasmi kutoka Chama cha Mapinduzi { CCM } iliyoainisha na kuthibitisha kwamba Balozi Seif Ali Iddi ameteuliwa na chama hicho kuwania nafasi hiyo ya Uwakilishi kwenye Jimbo la Mahonda.

Afisa Uchaguzi huyo wa Wilaya ya Kakaskazini B alifafanua na kuwataka wagombea wote watakaochukuwa fomu za kuwania nafasi hizo kutumia fursa ya kufika kwenye Ofisi hiyo kwa kupata ushauri zaidi wa namna ya kujaza vyema fomu hizo licha ya kupatiwa maelezo ya awali wakati wanapokabidhiwa.

Alisema hatua hiyo kwa kiasi kikubwa itatoa fursa pana ya kutatua changamoyo zinazoweza kujitokeza na kuepukwa mapema ili kukidhi matarahio yaliyopangwa na tume hiyo.

Balozi Seif Ali Iddi alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kitope kupitia chama cha Mapinduzi kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita ambapo kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar jimbo hilo limevunjwa na kuzaliwa majimbo mawili ya Mahonda na Kiwengwa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/8/2015.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link