Home » » Balozi Seif Ali Iddi aweka jiwe la msingi la ujenzi wa skuli mpya ya Mtaa wa Tomondo Wilaya ya Magharibi ”B”

Balozi Seif Ali Iddi aweka jiwe la msingi la ujenzi wa skuli mpya ya Mtaa wa Tomondo Wilaya ya Magharibi ”B”

Written By CCMdijitali on Friday, August 21, 2015 | August 21, 2015


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifungua kitambaa kuashiria kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa skuli mpya ya Mtaa wa Tomondo Wilaya ya Magharibi ”B” kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein.
Nyuma ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar 
Mheshimia Zahra Hmad.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifungua kitambaa kuashiria kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa skuli mpya ya Mtaa wa Tomondo Wilaya ya Magharibi ”B” kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein.

Nyuma ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar 
Mheshimia Zahra Hmad.
 
 Baadhi ya Wanafunzi wa maeneo ya Mtaa wa Tomondo wakishuhudia hafla ya uwekwaji wa jiwe la msingi la skuli mpya ya msingi ya eneo hilo.
 Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa kengo jipya la skuli ya msingi Tomondo ambae pia ni Mbunge anayemaliza muda wake wa Jimbo la Dimani Mh. Abdulla Sharia Ameri akipungia mkono wananchi waliohudhuria uwekaji wa jiwe la msingi la skuli hiyo.
Hayo ni makeke na mbwembwe za uvaaji wa majamsoni { Miwani } inayoonyesha mwaka 2015 yaliyovaliwa mmmoja wa wanafunzi waliohudhuria hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la skuli mpya ya Tomondo . { Jina la mwanafunzi hatukulipata }.
Picha na –OMPR – ZNZ.

 Press Release:-

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeazimia kujenga skuli Kumi Mpya za Msingi katika kiwango cha Ghorofa kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016 ambapo fedha kwa ajili ya kazi hiyo tayari zimeshatengwa.

Alisema kutokana na ongezeko la idadi ya watu hasa katika maeneo ya Mji hususan Wilaya ya Magharibi “A” na “B” Skuli za msingi zimekuwa na changamoto ya idadi kubwa ya wanafunzi madarasani.

Dr. Ali Mohammed Shein alieleza hayo wakati akizungumza na wazazi, walimu, wanafunzi na wananchi wa Mtaa wa Tomondo ndani ya Jimbo la Dimani Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kuweka Jiwe la msingi la Ujenzi wa Skuli Mpya inayojengwa katika eneo la Tomondo Wilaya ya Mgharibi “B “.

Alisema Serikali imekuwa ikichukuwa jitihada mbali mbali katika kuhakikisha kwamba Watoto wote wa Zanzibar waliofikia umri wa kwenda skuli wanaanza masomo ya msingi ili haki hiyo.

Alisema Zanzibar ni miongoni mwa Nchi chache Duniani zilizofikia kiwango cha watoto wake wote waliofikia umri wa kwenda skuli hupata fursa hiyo kwa asilimia 100% hadi mwaka huu wa 2015 na kupindukia kiwango kilichowekwa na Umoja wa Mataifa na Maendeleo ya Milenia.

Rais wa Zanzibar alizishukuru jitihada zinazochukuliwa na Wananchi katika maeneo mbali mbali Nchini kwa kushirikiana na Viongozi wao katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza majengo ya Skuli na kuanzisha ujenzi wa skuli mpya.

Alisema hali hiyo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuondoa tatizo la uhaba wa nafasi madarasani na kupunguza masafa kwa watoto wadogo waliokuwa wakilazimika kufuata masomo katika skuli za mbali.

Dr.Shein aliwahakikishia Wananchi kwamba Serikali inathamini jitihada hizo na itaendelea kuziunga mkono kwa vitendo ili lengo la kuwapatia haki yao ya Elimu Watoto liweze kufikiwa kwa shabaha ile ile ya Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya Tarehe 12 Januari mwaka 1964 Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Katika kuimarisha sekta ya elimu Nchini Rais wa Zanzibar alisema Serikali imeandaa sera na kutekeleza mipango mbali mbali ili kuongeza fursa za Elimu kwa Vijana Nchini.

Alisema Serikali hivi sasa inatekeleza Sera ya Elimu ya Mwaka 2006 ambayo imeweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha upatikanaji wa Elimu iliyo bora kwa watu wote bila ya ubaguzi.

“ Hii ni dhamira ya kutoa Elimu bila ya ubaguzi kwa Wananchi wote kama ilivyodhihirishwa kwa tamko la 
“ Elimu Bure ” lililotolewa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume Tarehe 23 Septemba, 1964 ”. Alisema Dr. Shein.

Alifahamisha kwamba Serikali Serikali imetafakari na kuzingatia changamoto iliyokuwa ikiwalazimu wazazi kuchangia baadhi ya gharama za huduma ya elimu ili kuhakikisha watoto wote wanapata elimu.

Dr. Shein alieleza kuwa uamuzi wa Serikali kwa sasa ni kubebe jukumu hilo kuanzia mwezi Julai mwaka huu wa 2015 ikiwa ni utekelezaji wa Tamko alilolitoa katika kilele cha maadhimisho ya Miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Aliwakumbusha wazazi na walezi kufuatilia watoto wao kwa kshirikiana na walimu ili kuondokana na tatizo la utoro kwani bila ya jitihada za pamoja azma hiyo haitafanikiwa wala kufikiwa.

Alifahamisha kwamba jitihada za pamoja zina mchango mkubwa kwa kuwa na kizazi bora kilichoelimika na chenye maadili mema yanayozingatia utamaduni wa malezi ya pamoja ambapo kuna haja ya kuyaendeleza ili kuinusuru jamii kutokana na changamoto zinazotokana na utandawazi.

Akisoma Risala ya walimu,wanafunzi na wazazi wa Tomondo Mwalimu Hadra Mkubwa Said alisema azma ya ujenzi wa skuli ya Tomondo imefikiwa baada ya Kamati ya Maendeleo ya Jimbo la Dimani kuamua ijenge skuli kwa lengo la kuwaondoshea usumbufu watoto wa maeneo ya Tomondo.

Mwalimu Hadra Alisema kwamba lengo la Kamati hiyo ni kuhakikisha kwamba Skuli hiyo inaendelea kukua hadi kufikia darasa na saba ikiwa na shabaha ya kuwa na majengo zaidi sambamba na maabara na huduma nyengine za skuli.

Alifahamisha kwamba lengo la Kamati hiyo ni kuhakikisha kwamba skuli hiyo inaendelea kukua hadi kufikia darasa la saba ikiwa na shabaha ya kuwa na majengo zaidi sambamba na maabara na huduma nyengine za skuli.

Akitoa taarifa ya Ujenzi wa skuli mpya ya Tomondo Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi ambae pia ni Mbunge anayemaliza muda wake wa Jimbo la Dimani Mh. Abdulla Sharia Ameir alisema ujenzi wa skuli hiyo ni kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa kuomba ridhaa ya kuliongoza Jimbo la Dimani mwaka 2010.

Mh. Abdulla Sharia aliwahakikishia wananchi na wazazi wa Jimbo la Dimani kwamba Madarasa mengine Matatu yataendelea kujengwa chini ya usimamizi wake licha ya kwamba atakuwa nje ya utumishi wa Jimbo la Dimani kwa nafasi ya Ubunge.

Alikanusha uvumi uliotolewa na baadhi ya watu wa kumtuhumu kuiacha CCM na kujiunga na upinzani na kusema kwamba hizo zilikuwa njama za kutaka kumvunja moyo aache juhudi hizo za kuwaletea maendeleo Wananchi wa Jimbo hilo.

Aliiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kumwachia mlango wazi kwa kuendelea kumpa ushirikiano katika azma yake ya kutandika maendeleo ya elimu ndani ya Jimbo hilo.

Naye Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Zahara Hamad alisema ujenzi wa skuli hiyo umeleta Ukombozi mkubwa kwa watoto wa Mtaa wa Tomondo na maeneo jirani ambao walikuwa wakifuata elimu katika masafa marefu.

Mh. Zahra aliupongeza Uongozi wa Kamati ya Ujenzi wa Skuli hiyo Mpya ya Tomondo chini ya Uenyekiti wa Mbunge wa Jimbo hilo anayemaliza muda wake kwa ujasiri iliyochukuwa ya kuwaondoshea matatizo ya kufuata elimu masafa marefu watoto wa eneo hilo.

Alisema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar itahakikisha kwamba ifikapo Mwezi Januari mwaka 2016 skuli hiyo inaanza kutoa huduma baada ya kupatiwa vikalio kwa kuchukuwa wanafunzi katika mfumo uliopo wa mikondo miwili.

Ujenzi wa Skuli ya Msingi ya Tomondo wenye jengo lenye madarasa manne na Ofisi ya Mwalimu Mkuu ulioanza Tarehe 13/5/2015 na kutarajiwa kukamilika Tarehe 20/9/2015 unakisiwa kugharimu jumla ya shilingi Milioni 120,000,000/- hadi kukamilika kwake.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibarf
21/8/2015
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link