Na Mtafiti wa Kweli
SITAKI kumjadili mtu mwingine yeyote aliyekikimbia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa kisingizio chochote kile katika kipindi hiki cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani baadaye mwaka huu ila nitagusia watu wanane tu.
Hao ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Mbunge wa Segerea jijini Dar es Salaam, Dk. Makongoro Mahanga na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Singida, Mgana Msindai.
Wengine ni aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salalam kati ya mwaka 2007 – 2012, Sajenti John Guninita na aliyewahi kuwa Mbunge wa Nyamagana mkoani Mwanza na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha.
Watatu waliobaki ni wabunge waliomaliza muda wao katika bunge lililopita ambao ni Saidi Nkumba wa Sikonge, Tabora; Modestus Kilufi wa Mbarali katika mkoa wa Mbeya na Sioi Sumari aliyewahi kugombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki, Arusha mwaka 2012 na kusambaratishwa vibaya.
Wote katika ujumla wao, kila mmoja kwa kinywa chake mwenyewe alijitahidi sana kudai kwa mfano kuwa CCM imepoteza mwelekeo, haitendi haki tena kwa wanachama wake wanaoomba uteuzi wa kugombea urais, ubunge, udiwani na hata vinginevyo.
“Tulitaka tupate dereva ambaye pia ni fundi. Tulitegemea uamuzi wa haki ungetumika, (lakini) bahati mbaya Mwenyekiti wa Chama (au Rais Jakaya Kikwete) alipuuza mawazo ya wananchi”, alisema Mgeja alipokuwa akitangaza kuihama CCM na kwenda Chadema, Alhamisi ya wiki iliyopita.
Hata hivyo, Mgeja ambaye ni mmoja kati ya wafuasi kindakindaki wa Lowassa waliomfuata Chadema alishindwa, angalau tu kidogo kuwataja wananchi waliotoa mawazo na kisha kupuuzwa, na pia hakuweza kuyataja ni yapi kwa sababu alijua kwamba ni muongo.
Mbali na hilo, Mgeja anafahamu namna Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa mkoa wake wa Shinyanga alikokuwa mwenyekiti walivyofuatwa na magari, saa nne za usiku wa Julai 10 kutoka hotelini walikokuwa wamefikia, kisha wakapelekwa nyumbani kwa mbunge mmoja aliyemaliza muda wake kutoka mkoa wa Simiyu ambako, pamoja na mambo mengine walipewa maelekezo ya kufanya vurugu endapo jina la Lowassa lisingewasilishwa kwao, lakini wakayapuuza.
Bila shaka anajua hata vijana waliokuwa wakiandamana ili kushinikiza jina hilo liingizwe katika kile kinachoitwa ‘Tano Bora’ waliahidiwa fedha, na pia baadhi ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) waliopelekwa Saint Gasper Hostel Julai 11 walikwenda kuhongwa ili wafanye vurugu ukumbini baadaye mchana huo, lakini walipojaribu wakajikuta wanaumbuka.
Aidha, Guninita aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya na Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) hadi mwaka 1996 alipovuliwa vyeo vyote hivyo kwa utovu wa nidhamu, akakasirika na kuhamia Chadema kabla hajarudi na kuhama tena, Alhamisi hiyo akiwa pamoja na Mgeja naye hakubaki nyuma.
“CCM ya sasa imejaa viongozi wenye ubabe, dharau na majivuno. Wanapewa vyeo vya uyoga, wanatukana baba zao”, alisema akiwa anamlenga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Paul Makonda na kuongeza kwamba chama hicho kinachotawala hakina demokrasia.
Sitaki kurejea madai yaliyotolewa na Dk. Mahanga, Msindai na Nkumba kwa sababu ni yaleyale kuwa “CCM haitendi haki”, vinginevyo wanatumia kichaka cha Lowassa kuwa amenyang’anywa haki yake ya kugombea kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, madai yanayotengenezwa mezani kwa ajili ya maslahi ya mtu na genge lake.
Hizo ndizo kauli walizotunga na kukubaliana kwamba wazitumie kwa nguvu zao zote ili kuwadanganya Watanzania, lakini hasa wanachofanya ni kueneza uzushi, uongo, upotoshaji na kutumika kwa maslahi ya “Lowassa kwanza”, mambo mengine yanakuja baadaye.
Napenda nijulishe kuwa ukimwondoa Mgeja, wote waliobaki kwa maana ya Dk. Mahanga, Msindai, Guninita, Nkumba, Sioi na Kilufi waliingia kwenye kura za maoni za kutaka kugombea ubunge kwenye majimbo yao, lakini wote wakashindwa na kususia matokeo kwa sababu ya uchu wao wa madaraka.
Pamoja na kuwa Mbunge wa Segerea na pia Naibu Waziri kwa miaka 15 mfululizo tangu mwaka 2000, Dk. Mahanga ni mmoja wa viongozi waandamizi wa Serikali ya Awamu ya Nne waliokuwa na ‘gundu’ kwenye majimbo yao.
Alikuwa mbunge anayechukiwa kwa kiasi kikubwa na wapiga kura wa jimbo hilo na kulazimika kubadili njia ya kutoka na kurudi nyumbani kwake, sababu kubwa ikiwa ni kuzomewa katika baadhi ya vijiwe.
Mathalani, waendesha bodaboda wanaoweza kuitwa kuwa “zimepinda” katika lugha ya mjini walifikia mpaka hatua ya kufukuzana na gari lake barabarni huku wakimzomea, hivyo alichofanya ni kutafuta njia anakoweza kupita kwa amani na bila ya kutiwa aibu.
Ndiyo maana alipojitosa kwenye kura za maoni za kutaka kugombea tena ubunge, tena kwa ubishi licha ya kushauriwa mapema kuwa apumzike akaambulia kura kiduchu.
Katika mbio hizo mwaka huu, Dk. Mahanga alipata kura 2,381 na kushika nafasi ya tatu nyuma ya Scolastika Kivila, mama aliyepata kura 6,155 huku aliyeshinda akiwa ni Bonna Kaluwa ambaye aliibuka na kura 6,965.
Mbali na afisa huyo wa zamani wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kushindwa huko kwenye kura za maoni pia kulimkuta Msindai katika jimbo la Mkalama, mkoa wa Singida kwa kupata kura 3,908 huku mshindi akiwa ni Joseph Kiula aliyepata kura 5,223.
Kana kwamba haitoshi, Guninita mwenye umri wa miaka 56 alijitosa kugombea ubunge katika jimbo la Kilombero mkoani Morogoro, lakini akaambulia kura 165 tu na kushika nafasi ya nane kati ya wagombea 10 huku mshindi, Abubakari Asenga (32) akipata kura 9,629.
Mbali na Dk. Mahanga, Msindai na Guninita, mwingine aliyetupwa katika kura za maoni na kukimbilia Chadema anakodhani ataupata ubunge ni Saidi Nkumba.
Akiwa amejitosa ili kutetea nafasi hiyo kwa awamu nyingine, Nkumba alipata kura 3,236 tu huku akishindwa na George Kakunda aliyepata kura 4,109 katika jimbo la Sikonge, mkoa wa Tabora.
Aidha, Modestus Kilufi aliyekuwa amejitosa ili kutetea nafasi hiyo aliyokuwa nayo katika jimbo la Mbarali, mkoa wa Mbeya alishindwa baada ya kupata kura 7,114 huku mgombea mpya wa kiti hicho kupitia CCM, Haroun Mulla akiibuka na kura 8,556 na kudai chama hicho kwamba “hakitendi haki”.
Mwingine katika orodha hiyo ni Lawrence Masha, mbunge wa zamani wa Nyamagana aliyewahi pia kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na mmoja kati ya wapambe wakubwa wa Lowassa.
Habari zilizothibitishwa na baadhi ya watu wa karibu ya Lowassa zinasema kwamba Masha, kama rafiki yake huyo angeteuliwa kugombea urais kupitia CCM na hatimaye akashinda angempa ubunge wa kuteuliwa katika nafasi 10 za rais, kisha angemwingiza katika baraza lake la mawaziri.
Lakini alipokwama, Masha alijitosa kugombea ubunge huko Sengerema, hatua aliyochukua baada ya kugundua kuwa hakubaliki katika jimbo lake la Nyamagana ambalo lipo jijini Mwanza.
Licha ya kwenda Sengerema, Masha alishika nafasi ya nne akiambulia kura 3,254 tu huku mshindi wa mbio hizo katika jimbo hilo, William Ngeleja akizoa kura 15,845 na hicho ndicho kikasababisha akimbilie Chadema.
Aidha, Sioi Sumari ambaye pia alijaribu kugombea ubunge katika jimbo la Arumeru Mashariki kama alivyofanya mwaka 2012 naye alianguka tena.
Katika kura hizo za maoni za ndani ya CCM, kijana huyo ambaye ni mume wa binti mkubwa wa Lowassa alipata kura 4,038 huku John Sakaya akiibuka mshindi kwa kupata kura 12,729.
Kutokana na hali hiyo, Sioi aliamua kwenda Chadema kwa sababu ya uchu wake wa madaraka, na pia alifanya hivyo ili pengine asinyang’anywe mkewe ambaye ni mtoto wa Lowassa.
Naye kwa upande wake, Mgeja ambaye inabidi nitangaze kwanza maslahi kwamba ni mjomba wangu ilikuwa ikingojewa tu kuwa ni siku gani ataondoka ili kumfuata Lowassa.
Kati ya Wenyeviti wa CCM wa Mikoa yote iliyopo nchini, Mgeja alikuwa ndiye mpambe namba moja wa Lowassa akifuatiwa na Msindai, kisha anakuja aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Onesmo ole Nangole na Guninita.
Mgeja na Msindai kwa mfano walikuwa sambamba na Lowassa katika kila kijiji, mtaa, kata, tarafa, wilaya mpaka mkoa alipokuwa akitafuta wadhamini wakati wa kuchukua na kuruudisha fomu za kuomba kugombea urais kupitia CCM kati ya Juni 3 na Julai 2, mwaka huu.
Wote kwa pamoja walikuwa wakifanya hivyo kinyume cha maelekezo ya CCM, lakini inawezekana ‘walilewa’ fedha za Lowassa na hivyo wakajisahau kuwa ni viongozi wanaopaswa kuwa mfano wa kuheshimu Katiba ya Chama chao, kanuni, taratibu na miongozo mingine na kubaki ‘wakimwabudu’ yeye.
Wanafahamu vizuri kuwa Lowassa anayetaka urais kwa nguvu zake zote anatumia mamilioni ya fedha ili kuisaka nafasi hiyo, lakini kinachofanywa ni propaganda za kipuuzi zinazolenga kuwadanganya wananchi ikiwemo kukodi bodaboda, kuzilipia mafuta ‘sheli’ huku magari na wasindikizaji wengine nao ‘wakijazwa’ kwa malipo maalum.
Sitaki nitoboe ukaribu uliopo kati ya Lowassa na mjomba wangu Mgeja ambaye ni binamu yake na marehemu mama yangu mzazi, lakini naye namuomba asiendelee kuwadanganya Watanzania ili kukidhi matakwa yake ya kisiasa ama kiuchumi.
Inawezekana hakifahamu kile ninakichojua kuhusu undani wake kwa Lowassa, lakini inaudhi zaidi anapokuja na uzushi, uongo na upotoshaji mkubwa unaolenga ‘kumchafua’ Rais Kikwete kwa sababu tu anataka aendelee kumnyonya rafiki yake huyo, yule ambaye Februari 6, 2008 alijiuzulu uwaziri mkuu kwa kutajwa katika kashfa ya Richmond.
Sitaki pia niyaweke hadharani ninayoyafahamu kuhusu uongozi wake alipokuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga kwa sababu ni mjomba wangu, na pia ninafanya hivyo ili kumlindia heshima yake mwenyewe na hata Lowassa wake huyo, lakini nitashindwa endapo ataendelea kupotosha ukweli kwa makusudi.
Pamoja na kutotaka kumuumbua, lakini ninapenda nionyeshe angalau tu kidogo kuwa mjomba wangu huyo ni muongo linapokuja suala la maslahi yake.
Jumamosi iliyopita, Mgeja alinukuliwa na gazeti moja litolewalo kila siku nchini akikanusha ukweli wa kuwepo kwake Dodoma, siku tisa zilizopita ili kumpigania binti yake, Sinzo Mgeja apate ubunge wa Viti Maalum kupitia UVCCM.
“Mchakato huo ulikuwa ni wa kina mama. Nitawezaje kuingia kwenye mkutano huo? Labda mimi na Katibu (Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana tungebadilisha jinsia”, alisema kama alivyonukuliwa na gazeti hilo akimjibu Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aliyesema kuwa alikuwepo Dodoma kwa ajili hiyo.
Pamoja na kukanusha hivyo na kutoa kejeli, Mgeja alikuwepo Dodoma akiwaomba akina mama wamchague binti yake huyo ili awe Mbunge wa Viti Maalum, lakini aliposhindwa akachukia na kutohudhuria kikao cha NEC kilichofanyika Jumatano na Alhamisi za wiki iliyopita, kisha akaibukia Chadema ilipofika kesho yake.
Katika mbio hizo za kutafuta uwakilishi wa wananchi bungeni, Halima Bulembo aliyeshika nafasi ya kwanza kati ya wagombea 26 alipata kura 109 huku Sinzo akiambulia kura 42.
Nafahamu kuwa Dk. Mahanga naye alikuwa ni mmoja kati ya viongozi wa juu kabisa wa serikali waliokuwa ni wafuasi wakubwa wa Lowassa, lakini alikuwa akifanya hivyo kwa sababu aliamini kuwa ndiye rais wa tano wa nchi hii.
Sitaki pia kuyaweka wazi baadhi ya mambo yanayosemwa kuhusu naibu waziri huyo wa zamani, lakini tu ole wake naye iwapo ataanza kuwadanganya wananchi kama alivyofanya siku akitangaza kuwa anakwenda Chadema kumfuata Lowassa.
Kuhusu Msindai na Guninita, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Paul Makonda kwa mfano aliwahi kusema, na hapa ninanukuu:
“Yupo mtu anayewatumatuma hawa watu, amewafanya kuwa vibaraka (wake). Leo hii tutamjibu Msindai, Mwenyekiti (wa CCM wa Mkoa) wa Singida, kesho tutamjibu Guninita na keshokutwa tutamjibu nani (sijui) lakini nani aliyeko nyuma yao anayewatuma? Anaitwa Edward Ngoyai Lowassa...”
Sitaki kuwataja wote waliokwenda Chadema katika kipindi hiki cha mpito, lakini katika ujumla wao ama ni wapambe wa Lowassa mwenyewe ama ni wale walioshindwa kura za maoni za ndani ya CCM, hivyo walichofanya ni kutafuta kichaka ili kwenda kumalizia hasira au kuficha aibu kwa wake zao nyumbani, watoto wao na hata vinginevyo.
Mungu Ibariki Tanzania!
Napatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0787 088 870