KARIBU robo tatu ya viongozi wakuu wa Chadema Wilayani hapa, walijiuzulu nyadhifa zao jana na kutangaza kuhamishia nguvu zao kwa mgombea ubunge wa CCM, Stephen Wasira.
Imeandikwa na Ahmed Makongo,BundaWamedai wanafanya hivyo kutokana na kukerwa na kitendo cha makao makuu ya Chadema, kumpitisha Esther Bulaya kuwa mgombea ubunge jimboni humo, licha ya kuwa alishika nafasi ya tatu katika kura za maoni.
Bulaya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), alihamia Chadema hivi karibuni na moja kwa moja kwenda kujaribu siasa za majimbo, akianzia Bunda kwa tiketi ya chama chake kipya.
Aidha, aliyekuwa mshindi katika kura za maoni, lakini akaondolewa na vikao vya chama, Pius Masururi, pia ametangaza kuhamia CCM. Waliojiengua Chadema na kundi kubwa la wanachama ni Mwenyekiti wa jimbo hilo, Samuel Alfred, Katibu Mwenezi wake, Emmanuel Malibwa na Katibu wa Chadema wilayani Bunda, Rita Itandilo.
Wakizungumza jana katika Hoteli ya Green Garuden mjini hapa, viongozi hao walisema wameamua kujivua nyadhifa zao ili wabaki wanachama wa kawaida kwa kuwa viongozi wao wa Mkoa, Kanda na Taifa wamekiuka Katiba ya chama hicho.
“Kwa kile kilichotokea kupitia uongozi wetu wa mkoa, kupitia Katibu wetu wa Chama Mkoa Chacha Heche na Mwenyekiti wetu wa Mkoa, wameshindwa kujua jimbo la Bunda msemaji wa chama au mkoa ni nani, wao badala ya kufuata katiba, wameshindwa kujua katiba inasemaje kuhusu malalamiko yoyote.
“Wao hawakuona katiba inasemaje na kanuni za chama zinasemaje na taratibu zinasemaje, kuhusu malalamiko yoyote kama yalikuwepo ili waweze kuyafanyia kazi, badala yake kilichofanyika ni udhalilishaji.
“Mimi ni mwachama mwaminifu wa Chadema, nimekitumikia chama kwa kipindi cha miaka zaidi ya kumi, lakini leo Bunda imekuwa shamba la bibi, maamuzi ya mtu ndiyo yanayokuja kulitengeneza jimbo la Bunda, Kamati Tendaji ya jimbo la Bunda ilifanya uteuzi wake wa awali kupitia kura za maoni.
“Walimaliza kura za maoni wakaenda kwenye kamati tendaji, mimi kama Katibu wa Wilaya naletewa mapendekezo ya kamati tendaji ndiyo ninayafanyia maamuzi, nilichukua majina ya wagombea nikayapeleka kwenye tume kwenda kuyatambulisha, lakini kilichotokea Mkoa na Kanda na Naibu Katibu Mkuu wakatoa maelekezo mengine mbadala, akaletwa mtu ndani ya ofisi yangu bila kunishirikisha wala hata kupewa barua ya kunitambulisha.
“Lakini kilichofanyika huyo aliyeletwa akaanza kunielekeza, lakini mimi kama Katibu wa Wilaya ninayejua utaratibu nilikataa. Kilichotokea nikiingia ofisini kwangu pale naonekana kama mimi ni mgeni au mtu anayehitaji huduma pale, na kilichotokea wakachonga muhuri mwingine wakatengeneza muhuri ndani ya muhuri mwingine,” alidai.Samwel Alfred alisema;”Mimi ndiye Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Bunda, nimeamua kujiuzulu kwa sababu kuna vitu vilivyonikera baada ya kuona kuna watu wanavunja Katiba.
“Cha kwanza tulipiga kura za maoni wakapatikana washindi watatu wakiwemo wawili ambao wamekitumikia chama, lakini cha ajabu wakarudisha jina la mshindi wa tatu (Esther Bulaya), hawakuvunja Katiba?
Cha ajabu aliyerudishwa hakuonyesha ushirikiano na viongozi waliokuwepo, kwa kuhofia kuwa walikuwa kambi nyingine kwamba watasababisha ashindwe,” alisema. Aliongeza kuwa pia kwa upande wa wagombea udiwani, wagombea waliopendekezwa na kamati tendaji pia majina yao yalibadilishwa na viongozi wa mkoa, kanda na hata taifa.
“Mimi kama kiongozi niliyepigania chama hiki niliyepata kesi nyingi nimekaa magereza, nimenyanyaswa nimepigwa na nimedhalishwa sana, leo hii nimeamua kujiuzulu, lakini siyo kwamba naondoka peke yangu naondoka na makamanda wakiwemo wajumbe wa Kamati ya Utendaji na Katibu wa Vijana (Bavicha), kwa hiyo robo tatu ya kamati tendaji yote tumejiuzulu.
Katibu Mwenezi wa Jimbo, Malibwa alisema; “Sijaondoka peke yangu kama mnavyoona hapa ndugu waandishi wa habari tunao viongozi wote wa kata 20 za jimbo la Bunda, wakiwemo wenyeviti wa kata, makatibu wa kata, kwa ujumla kamati ya utendaji yenye watu 17, mimi mwenezi, mwenyekiti wangu na wajumbe wengine tumeondoka wamebaki watu watatu tu,” alisema.