Rais Jakaya Kikwete akiwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kabla ya kufungua mkutano wa wazee wa Dar es Salaam uliofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jana. (Picha na Ikulu).
MWENYEKITI wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amesema ujivuni wa fedha sio mali kitu, kwani mtu anaweza kununua watu wachache kwa tamaa na njaa zao, lakini hawezi kukinunua chama chote.
Pia, amesema wana CCM wasihofu kwani mtu anaweza kuwalipa watu wachache na kamwe hataweza kuwanunua Watanzania wote.
Akimtambulisha mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli kwa wanachama wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema uteuzi wa mgombea huyo umekipa sifa chama hicho.
Alisema uteuzi wa Dk Magufuli ni kama ulipangwa na Mungu na akaeleza kuwa ndio maana hata uchukuaji wake wa fomu, haukuwa na mbwembwe zozote wala hakutaka kuzungumza na waandishi wa habari kama walivyofanya wagombea wengine.
“Siku moja nilizungumza naye nikamuuliza wenzako wanachukua fomu za urais, mbona wewe hujaenda kuchukua, akanijibu hivi na mimi natosha kuwa Rais, nikamweleza wana CCM wenyewe wataamua kama unatosha ama hautoshi. “Siku moja akasema ana shida ya kuja kuniona, nikamwambia njoo, alivyokuja akaniambia masuala ya madeni ya makandarasi... lakini baadaye akasema mzee nimekuja kukuaga naenda kuchuka fomu, lakini sitazungumza na waandishi wa habari... sasa nikamhoji watu watakujuaje?” alisema Kikwete.
Aliongeza kuwa kesho yake akasikia Dk Magufuli amechukua fomu; lakini amewakimbia waandishi.
Alisema ndio maana kwenye vikao vya chama wakati wa uteuzi jina la Magufuli kuanzia Kamati ya Maadili, Kamati Kuu na kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa lilipenya kwa sababu ni mtu mwadilifu na akapita pia kwenye mkutano mkuu.
Rais Kikwete pia alitumia mkutano huo, kutaja sifa za mgombea huyo wa CCM kuwa ni mgombea mzuri aliyekamilika kila upande, kwani ni mwadilifu na mwaminifu kwa chama chake.
Sifa nyingine ya Dk Magufuli aliyoitaja ni kwamba ni mchapakazi hodari na hana kigugumizi kusema yale anayotekeleza kuwa anayafanya kutekeleza Ilani ya CCM.
Alisema mgombea huyo hakuwahi kuona aibu, kutaja mafanikio yake kuwa ni mafanikio ya CCM.
Pia, alisema mgombea huyo sio tajiri na hana fedha, ila anapenda kuona matokeo ya kazi anayofanya inapata mafanikio makubwa. Alisema Dk Magufuli anachukia uzembe, ubabaishaji na rushwa na ndio maana wala rushwa hawampendi mgombea huyo, kwa maana wanajua kiama chao kimekaribia.
“Niwaambie tu kwamba mgombea wetu ni sampuli nyingine, Watanzania mnataka nini zaidi ya huyu mtu, mnataka mtu wa namna gani? Alihoji Rais Kikwete.
Alisema kama Watanzania wanapenda nchi ipige hatua ni vyema wamchague Dk Magufuli, aweze kuwafikisha huko. Alisema Dk Magufuli anatosha na anafaa sana kuwa Rais wa tano wa Tanzania.
Magufuli: Sijawahi kushindwa
Kwa upande wake, akizungumza na wanachama hao wa CCM, Dk Magufuli alisema anatosha mbele, nyuma, kushoto na kulia kuwa Rais, hivyo aliwataka wana CCM kuwa wamoja ili kuleta ushindi.
Alisema kwa miaka 20 ambayo amekuwa naibu waziri na waziri serikalini, hajawahi kushindwa kutekeleza majukumu yake, jambo ambalo linampa imani kuwa ataweza kufanya kazi ya urais vizuri zaidi.
Alisema CCM ni chama kikubwa na kimeweza kuhimili mambo mengi muda mrefu na kina uwezo wa kuendelea kutawala ili mradi wanachama wawe na mshikamano katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye kampeni za uchaguzi.
“Mimi natosha na natosha kwelikweli,” alisema Dk Magufuli na kuongeza kuwa anazijua shida za Watanzania, hasa vijana, wanawake na aliahidi kuwa kamwe hawatawaangusha.
Imeandikwa na Shadrack Sagati
Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM tawala Dkt John Pombe Magufuli akiongea na wazee wa Dar es salaam leo Agosti 19, 2015 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.
Meza Kuu ikimfurahia Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM Dkt John Pombe Magufuli akiongea na wazee wa Dar es salaam leo Agosti 19, 2015 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Wazee wa CCM wa Dar es salaam akipeana mikono na Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM tawala Dkt John Pombe Magufuli baada ya kuongea na wazee wa Dar es salaam leo Agosti 19, 2015 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Wazee wa CCM wa Dar es salaam akipeana mikono na Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM tawala Dkt John Pombe Magufuli baada ya kuongea na wazee wa Dar es salaam leo Agosti 19, 2015 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam
Meza Kuu ikimfurahia Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM tawala Dkt John Pombe Magufuli akiongea na wazee wa Dar es salaam leo Agosti 19, 2015 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.PICHA NA IKULU