Na Charles Charles
JUMAPILI iliyopita, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Meja Joseph Butiku aliwashangaa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kumkaribisha Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa, Edward Lowassa kuwa mwanachama wao.
Aidha, Butiku aliyewahi kuwa Katibu wa Rais kuanzia mwaka 1965 hadi 1985 wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwashangaa zaidi kwa kumteua Lowassa kuwa mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza kwenye mdahalo kuhusu umuhimu wa maadili katika kuimarisha amani, haki na umoja kuelekea uchaguzi mkuu ujao, Butiku alisema Lowassa ni kiongozi mwenye tuhuma za siku nyingi za ufisadi.
Alisema Lowassa na wenzake kadhaa ambao hakuwataja kwa majina, wamekijengea Chama Cha Mapinduzi (CCM) mazingira ya 'kunuka' kutokana na hulka yao ya kutoridhika, uchu wa madaraka na kutaka kujitajirisha kwa njia 'chafu" kwa kutumia 'kichaka' cha siasa.
Katika hali hiyo, Butiku alisema Lowassa na wapambe wake walipaswa kutoka siku nyingi ndani ya CCM.
"Waondoke (na Chadema) wapokeeni tu. Kama hukubaliani na msimamo wa mwenye nyumba (akimaanisha Katiba, Kanuni na Taratibu za CCM) unatoka na siyo kuchafua nyumba ya watu", alisema.
Akionyesha kuwa anajua mambo mengi, Butiku ambaye ni Meja wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) alisema pia watu 'wamenunuliwa' , jambo ambalo limefanyika pia kwa vyombo vya habari ili vifanye kazi ya matajiri hao.
"Tunajua (kwamba) wengi wamenunuliwa na wanaonunua vyombo vya habari hawafai kupewa (uongozi wa) nchi.
"Wamewanunua (mpaka) vijana wa vyuo vikuu, wanamwaga fedha kwa vijana wa pikipiki (au bodaboda) hadi wanakanyagana, kuumizana na kudhalilika. Ni bora walivyoondoka CCM na hata hivyo walivumiliwa kwa muda mrefu".
Akirejea historia ya tuhuma za ufisadi dhidi ya Lowassa mwaka 1995, Butiku alifichua kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ndiye alimshtaki mbunge huyo wa zamani wa Monduli, Arusha kwa Baba wa Taifa kwamba ni fisadi asiyefaa kuwa rais wa nchi hii.
"Hivi mnajua kuwa aliyemshtaki Edward (Lowasa kwa Mwalimu Nyerere) alikuwa Mwinyi, (wakati huo akiwa rais?)
"Unajua nchi hii bado changa sana. Mambo mengine unayaacha tu ili (Tanzania) isivurugike. Lakini ukiamua kuyasema mambo ya Edward (yanatisha) na mimi nayajua", alibainisha.
Naam! Hayo siyo maneno yangu ila yanatoka kinywani mwa Butiku, Katibu wa Rais na Mkuu wa Mkoa Mstaafu aliyeanza kazi wakati Lowassa akiwa mtoto wa chekechea.
Anaijua Tanzania na misingi yake kama anavyokijua chumba anacholala nyumbani kwake. Anawajua watu wengi walioanza kazi wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere, mmoja kati yao akiwa ni Edward Lowassa.
Anaijua vizuri CCM na sababu za kuundwa kwake kuliko Lowassa aliyekuja baadaye, tena akitokea chuoni kuja kufanya kazi akiwa hajui lolote wala chochote.
Namshukuru afande wangu Butiku kwa kusema yale ambayo, kwa namna yoyote ile kama ningeyasema miye wapambe wake wakiwemo ninaowajua vyema, wengine ni waandishi wa habari wakongwe wangenimwagia kila aina ya uzushi na matusi.
Nampongeza kwa kuwa amejitosa waziwazi kusema ukweli anaoujua, ule ambao kwa wengine utakuwa wa shubiri.
Sina sababu ya kuendelea kurejea kile kilichozungumzwa na Butiku, lakini hotuba yake angalau imeweza kuwafumbua macho baadhi ya wapambe wakubwa wa Lowassa, wale ambao kuna wengine wanatumika kama dodoki bila wao kufahamu.
Nimekuwa nikiandika mara kadhaa kuhusu uovu wa kutafuta urais unaofanywa na Lowassa, wapambe wake ama sasa na viongozi wa Chadema yenyewe.
Ingawa Butiku mwenyewe hakutaja gazeti, kituo cha redio au televisheni wala mwandishi wa habari 'aliyenunuliwa', ukweli kuhusu jambo hilo unajionyesha hata kwa taahira wa akili.
Ijumaa iliyopita kwa mfano, waandishi wa habari na watangazaji wa baadhi ya vyombo vya habari nchini, walikodiwa ndege maalum na Lowassa au kwa uwezeshaji wake kutoka Dar es Salaam hadi Mbeya ili wakaandike vizuri habari zake za kutafuta wadhamini.
Kutoka huko walipelekwa hadi Arusha, Mwanza na hatimaye visiwani Zanzibar utadhani ni watumishi wake mwenyewe.
Walipelekwa kwa usafiri huo wa gharama kubwa zaidi kuliko wote duniani, lakini pili walilipwa pia posho na huenda walikuwa wakilipiwa hadi malazi yao, chakula na hata vinginevyo.
Inawezekana walifanyiwa hayo yote kwa sababu, kikubwa anachohitaji Lowassa ni kuzuia baya lake lolote lisiandikwe wala kutangazwa na chombo chochote kile cha habari.
Wale wanaofahamu kuhusu suala hili watakuwa na kumbukumbu nzuri, kwamba hata wakati akitafuta wadhamini kwa ajili ya kuomba uteuzi wa kugombea urais kupitia CCM, Lowassa alikuwa 'akimiliki' na kuzunguka na timu maalum ya waandishi wa habari.
Alikuwa akizunguka nao kwa magari ya kifahari aina ya Landcruiser VX, na pia alikuwa akipaa nao kwa ndege kama ilivyokuwa kutoka Iringa hadi Songea, mkoa wa Ruvuma.
Mtu anayekuchukua kutoka Dar es Salaam na kuruka naye kwa ndege hadi Mwanza, ukasafiri kwa magari ya kifahari kutoka huko hadi Geita, Mara, Simiyu, Geita, Shinyanga, Tabora na kadhalika kwa gharama zake yeye hakika huwezi kuandika maovu yake ila kumpamba hata kwa uongo.
Haiwezekani akuzungushe kila mkoa huku akikulipia mahitaji yako yote kama mwanaye, anakulipa mpaka posho ya shilingi 100,000 kila asubuhi na kukukirimu kwa kila kitu halafu uandike maovu yake.
Kama mwandishi wa habari anafanyiwa hayo yote, halafu anayemkirimu anazunguka naye muda wote inabidi awe na roho ngumu kama ya paka ndipo aweze kuandika ukweli.
Ndiyo maana wakati wote wa kutafuta wadhamini ndani ya CCM, waandishi wa habari aliokuwa akizunguka nao hata siku moja hawakuandika maovu yake.
Walishindwa kuhabarisha kwa mfano namna watu, katika baadhi ya maeneo walivyokuwa wakigombea au kuhoji posho walizokuwa wakiahidiwa ili kwenda kumdhamini.
Hakuna aliyeweza kuandika ama kutangaza jinsi walivyokuwa wakisombwa na malori, tena ya kukodi wakitolewa takribani kila eneo la mkoa anaokwenda.
Mfano mmojawapo ni Mbeya ambako watu walisombwa namna hiyo kutoka wilaya zote za mkoa huo ambazo ni Mbarali, Kyela, Rungwe, Ileje, Momba, Mbozi, Chunya na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
Wapo waliotoka hadi nje ya Mbeya kwa kusafirishwa kutoka Rukwa, Njombe na Iringa huku alipokwenda Mwanza wakitolewa mpaka Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Kagera, Geita, Mara, Manyara, Arusha na wengine Kilimanjaro.
Pamoja na kusaka 'mafuriko' hayo ya 'kutengeneza', watu wamekuwa wakidanganywa vinginevyo ili 'kumbeba' tajiri huyo kwa gharama zake.
Kama alivyobainisha Butiku, harakati za Lowassa za kutaka kwenda Ikulu kwa gharama zozote zimewakumba hadi wanafunzi wa vyuo vikuu, waendesha bodaboda na makundi mengine kwa kuwalipa mamilioni ya fedha.
Pamoja na 'uchafu' wote huo kujulikana hadharani, vyombo kadhaa vya habari kamwe haviandiki au kutangaza chochote.
Ndiyo maana haishangazi kusikia kuwa baadhi ya wahariri wa magazeti, vituo vya redio na televisheni nchini wiki kadhaa zilizopita wamelipwa shilingi 1,000,000 kila mmoja.
Tunaambiwa fedha hizo wamelipwa ili wazuie taarifa zote za udanganyifu wa Chadema au Lowassa, na pia wahakikishe chama hicho na mgombea wake huyo wa urais wanapambwa kwa namna zote.
Mimi mwenyewe ni shahidi wa posho hizo za Lowassa kwa waandishi wa habari.
Niliitwa na kaka yangu huyo mwaka 2011 kwenda ofisini kwake, Mikocheni jijini Dar es Salaam ambako aliniambia, na hapa ninanukuu:
"Wewe ni mwandishi mzuri wa makala. Naomba unisaidie kunipamba kwenye magazeti ambapo, kila mwezi utakuwa unakuja hapa unachukua shilingi 300,000", aliniambia Lowassa kwa kinywa chake mwenyewe na kuongeza:
"Usiponikuta mimi utakuwa unamkuta sekretari wangu na atakupa, nitamwelekeza".
Kwa vile isingewezekana ofisini kwake kumwambia "hapana", kauli yangu kwake ilikuwa ya maneno manne tu: "Hakuna tatizo Mheshimiwa, nitafanya".
Nilipomwambia hivyo, Lowassa aliinama chini ambapo, kiasi cha dakika moja hivi baadaye aliinua macho yake na kunikabidhi shilingi 300,000 taslimu kama mfano, zote zikiwa noti za shilingi 10,000 kila moja.
Nilimpa mkono na kumwambia "nashukuru sana", lakini baada ya kumuuga na kuondoka sikurudi tena, na pia sikuwahi kuifanya kazi hiyo hadi leo.
Sikutaka kufanya hivyo kwa jeuri moja tu ambayo pia nimekuwa nikiisema mara nyingi.
Siwezi 'kununuliwa' na mtu kwa fedha zake ili nimuunge mkono, nimpambe magazetini au niwe 'mtumwa' wake kwa namna moja ama nyingine.
Naweza tu kumuunga mkono mtu yeyote kwa kuangalia hoja zake, sifa zake na uwezo wake wa kazi anayoomba kuifanya na siyo vinginevyo.
Ndiyo maana sikushangaa nilipopata habari kuwa baadhi ya wahariri wa magazeti, vituo vya redio na televisheni nchini wamehongwa shilingi 1,000,000 kila mmoja ili wampambe Lowassa katika harakati zake za kutaka awe Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Ndiyo maana sikushangaa kusikia Butiku naye amekemea jambo hili.
Katika hali hiyo na hata vinginevyo, wale wanaodhani kuwa Lowassa aliyeitwa fisadi alipokuwa CCM, tena kwa kiwango kikubwa zaidi na viongozi wa Chadema yenyewe atabadilika kwa kwenda katika chama chao.
Daima atabaki yuleyule na vilevile kama zamani hata iweje.
Mtu akizoea kula nyama ya nguruwe hawezi akaacha eti kwa sababu tu amehamia kijiji kingine!
Napatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244