Home » » Maalim Seif awatisha wafuasi wa Lipumba

Maalim Seif awatisha wafuasi wa Lipumba

Written By CCMdijitali on Saturday, August 8, 2015 | August 08, 2015


Maalim Seif Sharif Hamad

Na Waandishi Wetu - Habari Leo

 WAFUASI wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na pia mwenyekiti mwenza wa muungano wa wapinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Profesa Ibrahim Lipumba, wameanza kushughulikiwa na kutakiwa kuchagua moja; kuendelea kuwa ndani ya chama hicho au kutoka.

Ingawa Profesa Lipumba alipojiuzulu uenyekiti, alisema ataendelea kuwa mwanachama wa CUF, lakini Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wanachama waliokuwa wakimuunga mkono, kuamua moja, kubaki ndani ya chama hicho kama alivyoamua mchumi huyo mashuhuri duniani, au kutoka.

“Profesa Lipumba kajiuzulu CUF, wale waliojiunga CUF kwa sababu ya Profesa, wanayo fursa ya kuamua kubaki CUF au kutoka,” alisema Hamad juzi usiku, saa chache baada ya kiongozi huyo mkuu wa chama hicho, kujiuzulu.

Kauli zingine

Mbali na kuwataka wanaomuunga mkono Profesa Lipumba kuamua kutoka ndani ya chama hicho au kubaki, wakati kiongozi wao akiwa ameweka wazi kuwa hana nia ya kutoka katika chama hicho, Maalim Seif alitoa kauli zingine kuashiria kutohitaji hata uanachama wa Lipumba ndani ya CUF.

“Kama ni treni inayokwenda Mwanza, ikifika Morogoro abiria watashuka, lakini wengine watapanda, ikifika Kaliua watashuka abiria lakini wengine watapanda,” alisema Maalim Seif alipofanya ziara ya ghafla katika Makao Makuu ya CUF, Buguruni jijini Dar es Salaam juzi usiku.

Hamad amewahakikishia wanachama wa chama hicho waliokuwa wamezingira ofisi hiyo, kuwa uamuzi wa Profesa Lipumba kujiuzulu wadhifa wake hautausambaratisha Ukawa na CUF, ambayo kwa sasa haina Mwenyekiti wala Makamu Mwenyekiti, lakini akasema imeendelea kubaki katika mikono salama.

Alisema akiwa Katibu Mkuu na viongozi wenzake waliobaki, watahakikisha kwamba chama hicho kinafikia malengo ya kuanzishwa kwake, ambayo ni kuhakikisha kinakamata dola.

Alisema mwishoni mwa wiki hii, chama hicho kitaanza vikao vyakekuzingatia hatua iliyotokea, ili wachukue uamuzi thabiti wa kukiongoza chama hicho na kuhakikisha kinabaki katika mikono salama, hadi hapo uchaguzi wa kumtafuta Mwenyekiti utakapofanyika.

Ukawa

Akizungumzia Ukawa, Hamad alisema baada ya hatua hiyo ya Profesa Lipumba, alizungumza na viongozi wakuu wa umoja huo, akiwemo Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema), James Mbatia (Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi) na Emmanuel Makaidi (Mwenyekiti wa NLD) pamoja na mgombea urais wa umoja huo, aliyekatwa na Kamati ya Maadili CCM, Edward Lowassa na wamehakikishiana kuwa hawatarudi nyuma.

“Tumehakikishiana kwamba Ukawa upo na umeimarika zaidi na hatutarudi nyuma… Tumeona kwa namna unavyoungwa mkono na wananchi walio wengi, Magufuli (mgombea urais wa CCM) Ikulu ya Magogoni hataiona,” alidai Maalim Seif.

Alimpongeza Profesa Lipumba kwa kuwaachia wananchi wa Tanzania Ukawa, ambapo yeye Profesa ndiye aliyekuwa muasisi na Mwenyekiti wa wenyeviti wa vyama vinavyounda umoja huo.

Hata hivyo, hakuzungumzia hatua ya Umoja huo kumsimamisha Lowassa, kuwa mgombea urais, huku wakijua alishiriki kupinga harakati za umoja huo wakati ulipoasisiwa katika Bunge Maalumu la Katiba, mwaka jana.

Wasomi

Hatua ya Lipumba, iliyochukuliwa baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, kujiuzulu huku wote wakilalamikia kukiukwa kwa maadili ndani ya umoja huo, imechukuliwa kwa tafsiri tofauti na wasomi nchini.

Mhadhiri katika Idara ya Siasa na Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana, alisema Ukawa inatafunwa na dhambi inayotokana na kutoheshimiwa kwa matakwa ya viongozi wakuu na hivyo itaendelea kuwatafuna.

Alisema si jambo la kawaida kwa kiongozi aliyetumikia chama hicho kwa muda mrefu kufanya uamuzi wa kujiondoa ghafla, ingawa hiyo ni haki yake ambayo ameifanya baada ya kujitafakari na kuona uamuzi huo unafaa.

Kwa mujibu wa Dk Bana, kitendo cha mtu mmoja kuwa mkubwa baada ya kuingia kwa wiki moja ndani ya vyama vinne, akimaanisha Lowassa, na kuvuruga utaratibu wa vyama hivyo, Profesa Lipumba ameonesha kusimamia misingi ya haki na demokrasia.

“Lipumba atabaki katika historia kwamba alikuwa kiongozi wa CUF mwenye msimamo na asiyeyumbishwa katika kusimamia misingi na haki ndani ya chama cha siasa,” alisema Dk Bana.

Kifo cha Ukawa

Alisisitiza kuwa ikiwa Profesa Lipumba na Dk Slaa wangekuwepo na kusimama katika kampeni, kungekuwa na mchakato mzito lakini Ukawa bila watu hao wawili, ni mwanzo wa kumeguka na anaamini kuwa baada ya uchaguzi, Ukawa haiwezi kuendelea.

Alisema tatizo kubwa kwa Ukawa ni kubadili lengo kuu la kutetea na kusimamia Rasimu ya Pili ya Katiba, iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katika, Joseph Warioba.

Alisema kwa sasa wamebadili na kutafuta madaraka kwa kuiondoa CCM madarakani ili kushika dola, jambo ambalo halikuwa lengo lao, hivyo kimkakati haikuwezekana kukaa vizuri. “Mbaya zaidi wanachama wa vyama hivyo vinavyounda Ukawa hawaelewi kuhusu Ukawa na (umoja huo) imebaki kuwa wenye kumilikiwa na viongozi wakati wanachama ndiyo wapigakura wao,” alisema Dk Bana.

Bana alisema vyama hivyo vimesahau kuwa chama lazima kimilikiwe na wanachama ndipo kitakuwa madhubuti lakini wao dhamira yao imebaki kwa viongozi pekee.

Alisema haiwezekani Lowassa kuwa juu ya vyama vinne vya siasa na kufafanua kuwa hiyo ni kusigina demokrasia, jambo linaloifanya CCM ipumue kwani kazi kubwa ya chama cha siasa kwenye kampeni ni kujibu mapigo.

Shehe ampongeza

Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salim, alimpongeza Profesa Lipumba kwa uamuzi huo, kwani ameonesha uadilifu na kuheshimu utu wake na maamuzi yake kama alivyosema hayakuheshimiwa na Ukawa.

Alisema Profesa Lipumba amejijengea heshima ya kulinda utu kwani aliona kuna mambo yatakayovunja utu wake na kueleza kuwa ni dalili mbaya kwa wanaUkawa wengine kuwa makini kwa kuwa wahenga walisema, ‘mwenzako akinyolewa wewe tia maji’.

Kwa mujibu wa Shehe Alhadi, kwa sasa ni vigumu kuwafafanulia Watanzania malengo yao, kwani mwanzo waliona Ukawa inaweza kuleta faraja kwa kuonesha uwezo wa kuongoza nchi, lakini ni wazi hawawezi kufanya lolote katika nchi hii kutokana na wenyewe kutoelewana.

Dk Bisimba

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema Profesa Lipumba amefanya uamuzi wake na ni haki kufanya maamuzi hayo, kwa kuwa sababu inayodhaniwa ya Lowassa kuingia Ukawa, inaweza isiwe kweli.

Alisema kama dhamira yake Profesa Lipumba imemsuta kama alivyosema, ni jambo zuri na ameonesha ujasiri katika kusikiliza dhamira yake na kuifanyia kazi kwa lengo la kulinda heshima yake.

Kwa upande wake, Mtafiti Mwandamizi wa Masuala ya Uchumi kutoka REPOA, Dk Abel Kinyondo, alisema Ukawa wamemtumia Lowassa kama chambo cha kuvuta watu wengi, jambo ambalo alisema ni mbinu moja ya kushinda uchaguzi.

Lakini akaonya kuwa, siasa ni zaidi ya kushinda uchaguzi, na kusema ni vyema Ukawa wakatafakari uamuzi wao kwani jambo hilo linauweka umoja huo njia panda.

“Kwa kumpata Lowassa wanaweza kushinda uchaguzi, lakini je, maadili na sheria, Ukawa inasimamia wapi?” alihoji.

Wanachama wa zamani

Baadhi ya waliokuwa wanachama wa CUF, wameelezea hofu yao kuhusu uwezekano wa chama hicho kusambaratika. Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, walisema kitendo alichokifanya aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, kinaweza kuleta athari kubwa kwa chama hicho kwani alikuwa muhimili muhimu wa chama hicho.

Abdallah Miraji, ambaye alikuwa mwanachama wa chama hicho na sasa ni mgombea mwenza wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa chama cha ADC, alisema amefanikiwa kufanya kazi na Lipumba kwa muda mrefu sana na lengo lake la kuondoka katika chama hicho hakuanza karibuni, bali amekuwa akitamani kuondoka muda mrefu.

Alisema Lipumba alijitahidi sana kuwa mvumilivu kwa kipindi chote alichokuwepo katika nafasi yake ya uwenyekiti, akiamini kuwa chama hicho kuna siku kitasaidia kuleta mabadiliko hapa nchini.

“Naona kama Lipumba amekata tamaa baada ya kuvumilia kwa muda mrefu na ameona uwezekano wa kuwasaidia Watanzania haupo ndio maana kaamua kuiacha nafasi hiyo,” alisema Miraji.

Aliongeza kuwa kuwa kiongozi katika CUF lazima uwe mvumilivu kwani kuna watu wanajinufaisha wao wenyewe bila kujali nani ana umuhimu na nia nzuri na chama hicho. “Chama kina watu wabinafsi, lazima wajiangalie na kukubali kuacha kujinufaisha wao wenyewe kwa maslahi ya chama la sivyo chama lazima kisambaratike,” alionya Miraji.

Alisema ni vyema Lipumba akajiangalia upya kwani bado anahitajika sana katika siasa za Tanzania. Shoka Juma, ambaye aliwahi kuwa Mbunge kupitia chama hicho na sasa ni mwanachama wa ADC, alisema CUF ina watu wenye sauti na wengine wanashindwa kabisa hata kuzungumza kama Lipumba.

Alisema Lipumba alikuwa akitamani sana kuwa na uamuzi lakini aliikosa nafasi hiyo licha ya kuwa mvumilivu kwa kipindi kirefu.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link