Nape Nnauye, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM |
Kwa ufupi
Nape, anayewania ubunge wa Jimbo la Mtama, jana mchana aliamriwa na maofisa wa Takukuru kufika ofisi zao baada ya kutoka kuchukua fedha benki ya NMB eneo la Misonobarini mkoa Lindi.
By Waandishi Wetu, Mwananchi
Lindi. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amefafanua sakata lake la kuchukuliwa na askari wa Takukuru kwa mahojiano muda mfupi baada ya kuchukua fedha benki, akisema alikuwa akielekea kulipa mawakala.
Nape, anayewania ubunge wa Jimbo la Mtama, jana mchana aliamriwa na maofisa wa Takukuru kufika ofisi zao baada ya kutoka kuchukua fedha benki ya NMB eneo la Misonobarini mkoa Lindi.
“Ninadhani hawa jamaa walipotoshwa. Mimi nimekwenda zangu benki kuchukua fedha, lengo langu ni kuwalipa mawakala,” alisema Nape jana jioni alipopigiwa simu na Mwananchi kutoa ufafanuzi wa sakata hilo.
“Wakaja hawa jamaa, wakajitambulisha kuwa wanatoka Takukuru, wakaniuliza ‘mbona ninachukua fedha nyingi kipindi hiki?’ Nikawaambia ‘nakwenda kulipa mawakala, na fedha zenyewe ni hizi Sh3.6 milioni’.
“Basi, tukatoka taratibu tukaenda ofisini kwao, ni karibu tu na benki. Wakanihoji hata haikumalizika nusu saa, niliwaambia nataka kulipa mawakala wangu, tena fedha zenyewe hazitoshi, wako zaidi ya 100.”
Nape aliongeza kusema kuwa walimkamata na akawaambia kuwa yeye ni mwadilifu.
“Halafu ninyi, mnaacha marushwa makubwa makubwa huko, watu wanahonga halafu mnamvizia Nape masikini kwa Sh3mil?,” alisema.
Nape alielezea kufadhaishwa na tukio hilo akidai kuwa limetengenezwa kwa ajili ya kumchafua hasa kwa kuwa leo kuna kura za maoni, lakini akasema anaamini yeye ni msafi.
Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Lindi, Stephen Chami alikiri kumhoji Nape, lakini akasema walijiridhisha kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kulipa mawakala.
“Unajua tuna watu wetu, kwenye maeneo mbalimbali hasa kipindi hiki cha uchaguzi, tumeweka watu wetu maeneo mengi, tunataka kukomesha rushwa,” alisema.