Home » » Balozi Seif Ali Iddi aweka Jiwe la Msingi , Ujenzi wa Nyumba za Askari Polisi wa Wilaya ya Micheweni Mkoni,Kaskazini Pemba.

Balozi Seif Ali Iddi aweka Jiwe la Msingi , Ujenzi wa Nyumba za Askari Polisi wa Wilaya ya Micheweni Mkoni,Kaskazini Pemba.

Written By CCMdijitali on Sunday, September 6, 2015 | September 06, 2015


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifungua Pazia kuashirika kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Nyumba ya Kuishi Askari Polisi wa Wilaya ya Micheweni Mkoa wa
Kaskazini Pemba.
 Balozi Seif akikagua moja ya vyumba Kumi vilivyomo ndani ya jengo linalojengwa kwa ajili ya makaazi ya Askari Polisi Wilaya ya Micheweni Kisiwani Pemba.
 Baadhi ya Makamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba wakifuatilia hotuba ya Balozi Seif hayupo pichani ambapo wa kwanza kutoka kulia ni 
OCD Wilaya ya Micheweni Kamanda Haji Miraji na anayefuatia 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba RPC Moh’d Shehani.
 Baadhi ya Vijana wa Vikundi vya Polisi Jamii vya shehia zilizomo ndani ya Wilaya ya Micheweni walijumuika katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba ya Askari wa Wilaya
hiyo ambapo Mgeni Rasmi alikuwa 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.
 Balozi Seif akihutubia Makamanda, wapiganaji wa Jeshi la Polizi na Vikundi vya Polisi Jamii mara baada ya kuweka Jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba ya Askari wa Wilaya ya Micheweni.
Balozi Seif alivipongeza vikundi vya Polisi Jamii vya Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa uamuzi wao wa kukubali kusaidiana na Jeshi la Polisi katika ulinzi wa amani wa maeneo yao.
Picha na – OMPR – ZNZ.

 Press Release:-

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Heshima ya Jeshi la Polisi Nchini Tanzania itaendelea kuwepo endapo ujenzi wa Nyumba za Makazi ya askari wa Jeshi hilo utaimarishwa na
kuendelezwa katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.

Alisema ukosefu wa nyumba za kuishi Polisi katika maeneo wanaopangiwa kufanya kazi ndio unaopelekea baadhi ya askari hao kuamua kukodi nyumba na kuishi Mitaani.

Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizungumza na Makamanda, Askari wa Jeshi la Polisi, Vikundi vya Polisi jamii na Wananchi mbali mbali mara baada ya kuweka Jiwe la msingi la Nyumba ya kuishi Askari
inayojengwa katika Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema mfumo uliopo hivi sasa kwa baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi kuishi katika maeneo ya Kiraia unasababisha muhali kwa askari hao wakati wanapolazimika kuchukuwa hatua za kisheria dhidi ya Watu
waofanya makosa ambao wanakuwa katika mazingira ya pamoja wakati wote.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wananchi wa Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba kupitia Vikundi vyao vya Ulinzi Shirikishi na Polisi Jamii kwa uamuzi wao wa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuanzisha Ujenzi wa Nyumba hiyo ya kuishi Askari Polisi Wilaya ya Micheweni.

Balozi Seif aliwaasa watendaji wa Jeshi la Polisi Nchini kuendelea kusimamia sheria kikamilifu kwa kuzingatia maadili mema wakati wa kutatua matatizo yanayoisumbua Jamii katika Maeneo yao.

Alisema ipo tabia ya baadhi ya askari wa Jeshi hilo kupendelea kuwabeba watu maarufu,wenye uwezo na hata baadhi ya wageni wanaowekeza vitega uchumi Nchini kwa kuzingatia kupata kitu kidogo jambo ambalo ni kwenda kinyume na maadili yao ya kazi.

Alisema tabia hiyo mbaya inayolalamikiwa na Wananchi walio wengi ni sehemu na aina ya ufisadi unaofaa kuepukwa kwa nguvu zote kwa vile umekuwa ukisababisha vurugu na hata migogoro miongoni Jamii.

Katika kuunga mkono ujenzi huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliahidi kugharamia ukamilishaji wa vyumba vya kulala Wageni katika Jengo hilo na kuuomba Uongozi wa Jeshi hilo kufanya
thathmini itakayomsaidia kuelewa gharama zitakazohitajika katika kukamilisha vyumba hivyo.

Akitoa Taarifa ya Ujenzi wa Nyumba ya kuishi Askari wa Wilaya ya Micheweni Kamanda wa Upelelezi na Makosa ya Jinai wa Wilaya ya Micheweni Mkaguzi wa Polisi { Insector } Fakih Yussuf Mohammed
alisema mradi huo umekuja kutokana na ufinyu wa Makaazi uliokuwa ukiwakumba askari wa Jeshi hilo kwa kipindi kirefu sasa.

Mkaguzi wa Polisi Fakih alisema matunda ya Falsafa ya Polisi Jamii imeanza kutoa matunda kwa vile ujenzi wa nyumba hiyo ulioanza Mnamo Tarehe 1 Septemba mwaka 2014 pia umeshirikisha wananchi wa shehia 27 zilizomo ndani ya Wilaya hiyo.

Kamanda Fakih alifahamisha kwamba Wananchi hao wamejitolea kusaidia usafishaji wa eneo hilo, kuchangia baadhi ya gharama vikiwemo vifaa na saruji vilivyogharimu zaidi ya shilingi Milioni 8.5 wakiwemo pia Wananchi wengine waliojikubalisha kukopesha baadhi ya vifaa vya ujenzi wa Nyumba hiyo.

Alisema wakati Jeshi la Polisi Makamu Makuu likibeba jukumu la gharama hizo tayari limeshalipa Deni la Shilingi Milioni 16,000,000/- zilizotokana na mikopo mbali mbali ambapo askari wa Jeshi hilo nao pia
wamechangia Bati 50 ili kuendeleza ujenzi huo.

Kamanda Fakih Yussuf Mohammed alifafanua kwamba ujenzi wa nyumba hiyo unaotarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi Milioni 34.1 utakuwa na uwezo wa kuhudumia askari Kumi wenye Familia pamoja na askari 20 wasio na familia.

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Omar Khamis Othman alisema Wilaya ya Micheweni ilikuwa nyuma sana kiulinzi jambo ambalo limesababisha kuchangia kutokea kwa migogoro mingi ya uvunjifu wa amani.

Mh. Omar alisema yapo matokeo mbali mbali yaliyojitokeza katika vipindi tofauti na kusababisha uvunjifu wa amani pamoja na migogoro ya kijamii z ikiweno Karafuu.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Kaskazini Pemba aliuomba Uongozi wa Jeshi la Polisi Nchini kufikiria njia ya kuongeza watendaji wa Jeshi hilo ndani ya Wilaya hiyo kwa lengo la kusaidia kukabiliana na changamoto za
Bandari Bubu na matukio ya uvunjifu wa amani.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanbzibar
6/9/2015.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link