Home » » Kikwete: Elimu yetu ni bora, inakubalika popote duniani.

Kikwete: Elimu yetu ni bora, inakubalika popote duniani.

Written By CCMdijitali on Monday, September 7, 2015 | September 07, 2015

Rais Jakaya Kikwete
 
Rais Jakaya Kikwete, amesema madai kuwa elimu inayotolewa Tanzania ni duni, ni potofu kwani wahitimu wake wanakubalika duniani.

Rais Kikwete alitoa kauli alipokuwa akihutubia Mkutano Mkuu wa Nane wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Badala yake Rais Kikwete alisema tatizo liko kwenye kuwaandaa wahitimu kukidhi matakwa ya soko la ajira la ndani na la kimataifa.

“Elimu yetu ni bora na inakubalika popote duniani...wahitimu wanaweza kufanya kazi katika nchi yoyote, kinachotakiwa ni kuwapatia ujuzi wa kutosha kukidhi matakwa ya soko la ajira,” alisisitiza Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo.

Takwimu zinaonyesha kwamba vijana wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka nchini ni kati ya 800,000 hadi milioni moja na wanapigania nafasi za ajira zisizozidi 60,000 katika sekta ya umma na nafasi takribani 300,000 katika sekta binafsi.

Rais Kikwete alisema serikali inajitahidi kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuvutia wawekezaji na kuomba mchango wa kila mdau kutumia fursa na rasilimali zilizopo nchini kuzalisha mali na kuongeza ajira katika sekta ya umma na sekta binafsi.

Aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa kila anayestahili kulipa kodi afanye hivyo na kusisitiza kuwa serikali haiko tayari kuona watu wanakwepa kulipa kodi.

Akitoa mfano, alisema kama wadau wa sekta ya usafiri wa ndege wanaona kodi wanazotozwa ni kubwa, ni vyema wakakaa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakubaliane, lakini siyo kuchukua uamuzi wa kutolipa kodi.

Kuhusiana na mapambano ya rushwa alisema Tume ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (PCCB) ijizatiti vya kutosha kwa weledi na kwa mujibu wa sheria ili uwapo ushahidi wa kuiridhisha mahakama kumtia hatiani mshtakiwa.

“Mnapokwenda mahakamani mkashidwa mara kwa mara, kazi hii ya kupambana na kuzuia rushwa halitafanikiwa,” alisema Rais Kikwete.

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mali Asili na Utalii, Dk. Adelhelm Meru, alisema ingawa utalii unazidi kuimarika na kuchangia pato la taifa, unakumbwa na tatizo la ujangili unaoangamiza tembo na faru.

CHANZO: NIPASHE
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link