Home » » Marekani wampongeza Kikwete

Marekani wampongeza Kikwete

Written By CCMdijitali on Thursday, September 24, 2015 | September 24, 2015

Rais Jakaya Kikwete.

Imeandikwa na Mwandishi Maalum, Washingtong

VIONGOZI wa Marekani wamemmwagia sifa Rais Jakaya Kikwete kwa ujenzi na ulezi wa demokrasia, heshima kwa haki za binadamu na zaidi ya yote uheshimu wa Katiba, ambao unamwezesha kuondoka madarakani kwa mujibu wa Katiba na kukabidhi madaraka kwa Rais ajaye kwa hiari na kwa amani.

Sifa hizo zilitolewa juzi wakati wa ziara ya siku mbili ya Rais Kikwete, alipofanya mikutano mbalimbali na viongozi wa Serikali ya nchi hiyo na taasisi kubwa na muhimu zisizokuwa za Kiserikali katika mji huu mkuu wa Marekani.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony J. Blinken alimpongeza Rais Kikwete kuwa uamuzi wake wa kuheshimu Katiba ya Tanzania kwa kukabidhi madaraka ya uongozi wa nchi baada ya kumaliza vipindi viwili vya uongozi wake Alimwambia kuwa kwa uamuzi huo anatuma ujumbe mzito, dhahiri na unaosikika sana katika Bara zima la Afrika na Kanda ambako Tanzania ipo.

“Mafanikio yako ya uongozi yamekuwa ya kifani kabisa, hayana mfano katika Afrika ya leo. 

Umeacha historia kubwa na ya kudumu (legacy) ya kuheshimu demokrasia na Katiba ya nchi yako huku umeacha na kutuma ujumbe wa wazi kabisa kwa Bara zima la Afrika na katika ukanda ambako nchi yako ya Tanzania ipo,” alisema.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani mwishoni mwa mwaka jana, Blinken alikuwa Msaidizi wa Rais Barack Obama na Msaidizi Mkuu wa Baraza la Ushauri wa Usalama la Marekani.

Pia amepata kuwa Msaidizi wa Ushauri wa Usalama wa Makamu wa Rais wa Marekani na pia amepata kuwa mjumbe kwenye Baraza la Ushauri wa Taifa la Rais Bill Clinton. Rais wa Taasisi ya National Democratic Institute (NDI) ya chama cha Democratic, Ken Wallack, alimueleza Rais Kikwete kuwa kwa kuangalia yanayotokea duniani, anampongeza kwa msimamo wa kuheshimu katiba ya nchi.

“Unajiunga na kundi la viongozi wa kuheshimiwa sana katika Bara la Afrika ambao hawakuamini kuwa wao tu ndio wenye uwezo wa kuongoza,” alisema Wallack. Aidha, Rais wa Taasisi ya International Republican Institute (IRI) ya chama cha Republican, Balozi Mark Green, alimwambia Rais kuwa ameacha mfano kwao wa kupigania na kulea demokrasia duniani na hasa barani Afrika.

Balozi Green amepata kuwa Balozi wa Marekani nchini Tanzania wakati wa kipindi cha uongozi wa Rais Kikwete na alichangia kwa kiasi kikubwa jitihada za Serikali ya Rais Kikwete katika maendeleo. Aliyekuwa Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje Marekani aliyeshughulikia masuala ya Afrika, Johnnie Carson alisema Rais Kikwete ana kiwango kikubwa cha heshima nchini Marekani kwa jinsi alivyoongoza nchi na Serikali kwa miaka 10 iliyopita.

“Chini ya uongozi wako, Tanzania imeendelea kuonesha mfano usiokuwa na kifani katika ujenzi wa demokrasia na umeheshimu sana Katiba ya nchi yako. Sisi katika Marekani, tunakupongeza sana,” alisema Balozi Carson.

Balozi Carson ambaye sasa ni Rais wa Taasisi ya Amani katika Marekani ya United States Institute of Peace alisema Tanzania chini ya uongozi wa Rais Kikwete imeendelea kuwa rafiki mkubwa zaidi wa Marekani katika Afrika.

Akizungumza baada ya kutolewa sifa hizo, Rais Kikwete aliwaambia viongozi wa taasisi hizo maarufu duniani kuwa anawaheshimu wale ambao wanataka kuendelea na madaraka ya kuongoza nchi zao, kazi ya urais ni ngumu na mzigo mkubwa, ukiifanya miaka 10 inatosha.

“Isitoshe katika Tanzania tuna jadi sasa ya kuheshimu Katiba, unachaguliwa kwa miaka mitano na ukichaguliwa tena unaongeza mingine mitano. Baada ya hapo unawapisha watu wengine. Isitoshe ni jambo zuri kupata kiongozi mpya baada ya muda ambaye atakuja na mawazo mapya na aina mpya ya uongozi,” alisema Rais Kikwete.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link