Home » » Lowassa ataondoa umasikini nchi nzima kama jimboni ameshindwa kwa miaka 20?

Lowassa ataondoa umasikini nchi nzima kama jimboni ameshindwa kwa miaka 20?

Written By CCMdijitali on Friday, September 25, 2015 | September 25, 2015

 
 Mgombea Urais wa UKAWA 2015 Edward Lowassa alianza ziara ya kuingia mitaani Dar es salaam Aug 24 2015 ili kukutana na Wananchi.
 
Na Charles Charles

MGOMBEA wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa aliwaahidi Watanzania kuwa atawatoa katika kile alichosema ni umasikini na kuwafanya matajiri.


Akihutubia mikutano ya kampeni zake katika maeneo ya Chanika, Mbagala na Kigamboni jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Lowassa alisema Watanzania wamechoka kula mlo mmoja tu kwa siku badala ya mitatu.


"Mimi nauchukia sana umasikini. Nataka kila Mtanzania apate milo mitatu kwa siku", alisema Waziri Mkuu huyo wa zamani aliyejiuzulu Februari 8, 2008 kwa kashfa ya mkataba tata wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond Development LLC na kuongeza:


"Nataka kila mwenye baiskeli anunue pikipiki. Nataka kila mwenye pikipiki anunue gari. Nataka kila mwenye gari awe na matatu au anunue basi".


Kwanza ni ukweli kwamba hakuna binadamu yeyote duniani anayependa awe masikini, lakini inawezekana kwa watawa kama ilivyokuwa kwa hayati Mama Theresa wa Culcutta nchini India.


Sista huyo Mtaliano wa Kanisa Katoliki ambaye alifariki dunia mwaka 2007, alikula yamini ya kuishi maisha ya kifukara ili awasaidie binadamu wenzake wanaoishi kwa taabu.


Yeye alifanya hivyo kwa matakwa yake mwenyewe, lakini hakuwahi kuwa masikini ila alijitesa kwa sababu tu za kidini.


Nampongeza Lowassa kwa kusema anachukia maisha ya kifukara. Inawezekana ikawa ni kweli hasa kwa vile tayari amethibitisha kwa vitendo kuichukia hali hiyo.


Anatuhumiwa kuwa na fedha zisizolingana hata kidogo na kipato chake cha kazi. Anatuhumiwa kuwa mmoja kati ya Watanzania mafisadi, tuhuma ambazo zilitangazwa zaidi na viongozi wa Chadema yake ileile kuanzia Septemba 15, 2007.


Anatuhumiwa kutumia kila nafasi ya madaraka ya umma anayopata kujitafutia shilingi, yule ambaye Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndiye aliyekuwa Mtanzania wa kwanza 'kumnyoshea kidole' kuwa ni fisadi.


Pamoja na utajiri wake wote anaodaiwa kuutumia pia ili 'kununua' ugombea wa urais, Lowassa bado anatajwa kuficha ukweli wa mali ama vyanzo vyake vya mapato kwa kutotaja vyote.


Tayari nimeshasema kuwa sipendi pia umasikini kwa watu, lakini ninachotaka ni utajiri ambao kila mmoja ataupata kwa njia zote halali.


Sipendi utajiri utokanao na ubadhirifu wa mali ya umma, wizi wa aina yoyote, ulanguzi wa namna zote, ukwepaji wa kodi, ufisadi ama upatikanao kwa namna yoyote ile haramu.


Pamoja na kuchukia kwangu umasikini, lakini sikubaliani na uongo wa Lowassa kwamba eti anakerwa na hali hiyo kwa watu anaokuwa kiongozi wao na hasa waliompa kura zao.


Nimekuwa najionea maisha ya kifukara waliyonayo wananchi wa Monduli, jimbo ambalo kwa miaka 20 hadi mwaka huu limekuwa likiongozwa na mbunge anayeitwa Edward Lowassa.


Huyo ndiye anadanganya Watanzania eti kwamba akichaguliwa kuwa rais wao, wote watakuwa ni matajiri wa uhakika!


Alikuwa Mbunge wa Monduli tangu mwaka 1995 hadi 2015, lakini wananchi wa jimbo hilo ni mfano mzuri wa Watanzania masikini na malofa wa kutupwa.


Mtu anayebisha kuhusu ukweli huu aende katika vijiji vilivyopo huko ili akajionee mwenyewe.


Moja kati ya vielelezo halisi kuwa Watanzania wa Monduli ni masikini sana ni nyumba wanazoishi.


Licha ya Lowassa kudai eti akichaguliwa kuwa rais ataondoa nyumba zote za nyasi nchi nzima ndani ya siku 100, ukweli halisi ni kwamba ziko kwa wingi huko Monduli ambako amekuwa ni mbunge kwa siku 7,210!


Mbali na matembe na nyumba za nyasi, ufukara mwingine uliokithiri katika jimbo hilo unabainishwa na makundi ya vijana na watoto wanaoshinda kutwa nzima barabarani.


Hao kazi yao ni 'kujiuza' ili wapigwe picha na watalii, kisha wanalipwa kati ya shilingi 1,000 hadi 2,000 tu huku wakiwa wamejipaka masizi usoni kwao, kujifunga lubega au hata kuchomeka manyoya ya ndege vichwani.


Wanashinda wamejipanga kandokando mwa barabara. Wanashinda wakifuatilia watalii wa kizungu ili mradi wapigwe picha, lakini hivi leo anadai eti hapendi umasikini kwa wapiga kura wake!


Anataka kila Mtanzania apate milo mitatu, lakini wananchi wa Monduli hushindia mlo mmoja au pengine, wachache kati yao wanakunywa maziwa asubuhi na kushinda bila ya kula.


Kwa nini ameshindwa kuifanya kila familia ya jimbo hilo kuwa na nyumba za bati, matofali ya saruji au pengine ya kuchoma kwa miaka 20 aliyokuwa mbunge huko?


Hivi anawezaje kumaliza nyumba za nyasi nchi nzima kwa siku 100 na kushindwa huko Monduli kwa miaka hiyo yote?


Hivi anawezaje kumfanya kila Mtanzania anayemiliki baiskeli sasa anunue pia na pikipiki? Mbona wapiga kura wa Monduli karibu wote hawana kabisa hata hizo baiskeli tu?


Hivi anawezaje kumfanya kila Mtanzania anayemiliki usafiri wa pikipiki anunue gari?


Kama hata Japan ambayo ina viwanda lukuki vya pikipiki, magari na vifaa vingine vya elektroniki lakini imeshindwa kumfanya kila raia wake awe na bodaboda, gari angalau tu la mtumba au nyumba ya uhakika, yeye atawezaje kama siyo uongo ama utapeli wa kisiasa?


Sitaki kunyamaza kama Watanzania wanadanganywa waziwazi, lakini inakera zaidi kuona anayefanya hivyo ni mgombea wa urais aliyekuwa mbunge huku jimboni kwake kukinuka umasikini!


Siwezi kuvumilia uongo wa makusudi wa Lowassa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, lakini wakati wote alipokuwa na cheo hicho hata jimboni kwake alishindwa kuifanya kila familia iwe inakunywa angalau tu chai ya rangi.


Mbali na ahadi hizo za uongo, Lowassa ambaye sasa hata kuzungumza kwake inakuwa shida anachekesha pia hata kwa watu waliokosa upeo!


Mfano anaposema eti kila anayemiliki baiskeli atanunua pikipiki, kila mwenye pikipiki atanunua gari na kila mwenye gari anunue nyingine na kuwa na tatu au atanunua basi, hivi ni wapi duniani ambako watu wote wana uwezo huo wa maisha?


Kama kila mmoja atakuwa na pikipiki, magari au basi hapo nani atapanda la mwingine?


Nani atasafiria basi lake binafsi kwa mfano kutoka Morogoro, Tanga au Arusha kuelekea Mwanza, Mbeya ama Dar es Salaam akiwa ni yeye peke yake au na mkewe peke yao?


Kama kila mmoja atakuwa na bajaji yake, pikipiki, gari ama basi lake hapo nani atapanda la mwenzake?
Mwisho kabisa ni je, kama Lowassa eti anadai kuwa ataondoa umasikini nchi nzima, mbona umemshinda kule Monduli alikokuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 20?


Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link