Home » » Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Nd. Jabu Khamis Mbwana azikwa leo Kaskazini Pemba.

Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Nd. Jabu Khamis Mbwana azikwa leo Kaskazini Pemba.

Written By CCMdijitali on Tuesday, September 8, 2015 | September 08, 2015

 Mhe Jabu Khamis Mbwana alipoapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya na rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la mapinduzi, Dr A|li Mohamed Shein wakati wa uhai wake.

Press Release:-

Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Nd. Jabu Khamis Mbwana aliyefariki Dunia
usiku wa kuamkia leo baada ya kuugua kwa muda mfupi amezikwa Kijiji
kwao Kiuyu Mbuyuni Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Marehemu Jabu Khamis Mbwana alikuwa akisumbuliwa na homa kwa takriban
wiki moja iliyopita.

Umati Mkubwa wa Wananchi, waumini wa Dini ya Kiislamu, Viongozi wa
Kiserikali pamoja na Vyama vya Siasa wakijumuika pamoja na Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi walihudhuria mazishi ya
Kiongozi huyo aliyekuwa na Fani ya Tasnia ya Habari.

Marehemu Jabu Khamis Mbwana alizaliwa mwaka 1958 na kupata elimu ya
msingi katika skuli ya Kiuyu Mbuyuni na baadaye elimu ya Sekondari
katika Skuli ya Fidel Castrol Chake chake Pemba.

Alijiunga na mafunzo ya Uandishi wa Habari katika Chuo cha Habari
Tanzania { TSJ } na kupata Stashahada ya fani hiyo mwaka
1984 ambapo aliajiriwa kazi ya Afisa wa Habari Wilaya ya Miucheweni.

Marehemu Jabu KhaMIS Mbwana Aliamua kuingia katika ulingo wa Siasa na
kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika
Vipindi viwili kuanzia kwamba 1985 hadi mwaka 1995.

Utumishi wake makini uliozingatia maadili na nidhamu kwa Jamii
ulimuwezesha kuteuliwa kuwa Afisa Tawala wa Wilaya ya Micheweni Mkoa
wa Kaskazini Pemba mwaka 1996.

Mwaka 2006 Marehemu Jabu Khamis Mbwana aliteuliwa na Rais wa Zanzibar
kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chake chake, Wilaya ya Mkoani na hadi kufariki
kwake alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Micheweni.

Nd. Jabu alikuwa Mfanyakazi hodari, shupavu, aliyejiamini katika
utumishi wake na mwenye mashirikiano na watendaji wenzake wa Serikali
na alimthamini kila mtu katika Uongozi wake.

Akiwasilisha salamu za Rais wa Zanzibar kwenye maziko hayo Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba 
Dr. Ali Mohammed Shein amepokea kwa mshituko taarifa ya Kifo cha Msaidizi wake
katika Wilaya ya Micheweni Nd. Jabu Khamis Mbwana.

Alisema kifo hicho hakikuacha pengo wala msiba kwa familia pekee bali
kwa Taifa zima jamii ikikumbuka ushupavu wa ndugu Jabu wakati wa uhai
wake katika kusimamia haki na uadilifu.

Balozi Seif aliyepokea simu kutoka kwa Rais wa Zanzibar muda huo wa
mazishi aliitaka familia ya marehemu pamoja na marafiki kuwa na moyo
wa subra katika kipindi hichi kifupi cha msiba.

Mauti yanapomteremkia Mja hakuna ardhi wala mbingu inayhoweza kuzuia
au kukinga jambo hilo. Na hivyo ndivyo wajibu huo ulivyomkuta 
Ndugu Jabu Khamis Mbwana.

Mauti yanakata starehe ya Dunia, hayana kinga na kamwe hayazoeleki
jambo linaloiwajibikia kila nafsi kujiandaa na haki hiyo.

Marehemu Jabu Khamis Mbwana ameacha familia ya vizuka Watatu na
watoto 17. Mwenyezi Muungu ampe safari njema Marehemu Jabu. Amin.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
8/9/2015.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link