Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya Taifa ya CCM Zanzibar Balozi Seif Al Iddi akitoa Taarifa ya hali ya CCM ilivyo katika muelekeo wake wa safari ya ushindi katika uchaguzi Mkuu mbele ya vyombo mbali mbali vya Habari hapo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui.
Wapiga pich wa vyombo mbali mbali vya Habari wakiwa kazini kurikodi Taarifa ya safari ya CCM katika uchaguzi Mkuu iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya Taifa ya CCM Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Balozi Seif kati kati akijibu maswali ya wana Habari mbali mbali mara baada ya kutoa Taarifa ya safari ya CCM katika kushinda uchaguzi Mkuu aliyoitoa hapo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.
Wa kwanza kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Nd. Vuai Ali Vuai na kulia ya Balozi Seif ni Spika wa Baraza la Wawakilishi ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mh. Pandu Ameir Kificho.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Wananchi ,Wafuasi wa vyama vya Siasa , Waandishi wa Habari,Wasanii pamoja na Taasisi za kiraia Nchini wamepongezwa kwa jitihada walizochukuwa za kuifanya Nchi kuendelea kubakia katika hali ya amani na Utulivu ndani ya kipindi choche cha mchakato wa wagombea na maandalizi ya kampeni za uchaguzi zilizokuwa zikiendelea katika maeneo mbali mbali nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri u ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi wakati akitoa Taarifa ya hali ya CCM ilivyo katika kuelekea kwenye ushindi wa uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika kesho.
Balozi Seif alisema kazi kubwa iliyofanywa na washirika hao imewafanya Wananchi walio wengi kuelewa sera na ilani ya vyama vya Kisiasa na kupelekea kuwa watulivu muda wote licha ya baadhi ya Viongozi wa Kisiasa kuanza ishara ya kutaka kuparaganya Wananchi.
Alisema kutokana na harakati za maandalizi ya uchaguzi Mkuu kuanzia mchakato wa kura za maoni Chama cha Mapinduzi Mwaka huu kinatarajia kufanya vizuri zaidi baada ya kuridhika na mahudhurio makubwa ya Wanachama wake pamoja na Wananchi wakati wa kufuatilia Sera na Ilani zake.
Balozi Seif alifahamisha kwamba tathmini ya kina iliyofanywa na wataalamu wa Chama chake umeelezea kwamba CCM itashinda kwa zaidi ya asilimia 60% katika nafasi ya Urais wa Zanzibar na Asilimia 70% kwa nafasi za majimbo ya Zanzibar na kutarajia kuweka rikodi mpya tokea kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya Kisiasa Nchini Tanzania.
Alisema viongozi wa upande wa vyama vya upinzani wanaelewa vyema uwezo huo wa CCM kushinda uchaguzi hali iliyowafanya waanze kuingiwa na wasi wasi na kufikiria mawazo ya kutaka kushawishi vijana wao waandae mipango ya kufanya vurugu.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kampeni ya Taifa ya Uchaguzi ya CCM Zanzibar aliwaeleza Wana Habari hao kwamba Wananchi wa Zanzibar wamepata mafanikio makubwa katika miradi yao ya maendeleo na kiuchumi kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Alisema Ilani hiyo ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010 hadi 2015 imefikia utekelezaji wake kwa asilimia 98% kiasi kinachowafanya Wananchi wengi kuendelea kukiamini katika kuwaletea maendeleo yao.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Ilani ya Chama cha Mapinduzi inayoanzia mwaka huu wa 2015 hadi 2020 ambayo imenadiwa vyema kwa wananchi katika mikutano mbali mbali ya Kampeni imeonyesha ishara bora ya Matumaini kwa Wananchi walio wengi.
Akijibu swali kuhusu Changamoto endapo Kamati yake ya Kampeni ya Uchaguzi Taifa ya CCM ilipambana nayo Balozi Seif alielezea faraja yake kwamba kazi kubwa iliyofanywa ndani ya ilani mpya ndio iliyofanikisha kazi yao kuwa ya mafanikio.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Wananchi wote kujitokeza kwa wingi kuitumia haki yao ya kidemokrasia katika kupiga kura kwa kuwachagua Viongozi watakaowaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Aliwataka Wananchi wote wasivae sare wala vitu vinavyoonyesha alama za vyama vya siasa wakati wanapokwenda vituoni kupiga kura kwa vile kitendo hicho kitakwenda kinyume na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria za Uchaguzi.
Alisema Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi imejiandaa vya kutosha katika kukabiliana na vurugu zozote zitakazojitokeza wakati wa kupiga kura, Kuhesabu na kumalizia matokeo ya uchaguzi huo.
Chama cha Mapinduzi kilizindua Kampeni zake za Uchaguzi Tarehe 13 Septemba mwaka 2015 kwa upande wa unguja na Tarehe 15 Septemba kwa upande wa Pemba wakati Kampeni hizo zilizmalizia Tarehe 22 Oktoba kwa Pemba na Tarehe 23 Oktoba kwa Unguja.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
24/10/2015.