Home » » UN yapongeza uchaguzi Tanzania

UN yapongeza uchaguzi Tanzania

Written By CCMdijitali on Saturday, October 31, 2015 | October 31, 2015


KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Kimoon, ametuma salamu za pongezi kwa Watanzania, Serikali na vyama vya siasa, kwa namna walivyoshirikiana katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu na kumpata Rais Mteule wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.

Taarifa ya Ki-moon iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari, imeeleza kuwa Katibu Mkuu huyo amepongeza namna uchaguzi huo ulivyofanyika katika utaratibu mzuri na kwa amani na uwajibikaji mzuri walioonesha Watanzania. Akifafanua uwajibikaji huo, Kimoon amesema hatua ya Watanzania ya kupiga kura na kusubiri matokeo ya uchaguzi huo kwa amani, ni uthibitisho thabiti wa dhamira yao ya kujenga mfumo wa kidemokrasia, kulinda amani na ustahimilivu.

Salam za Odinga Mbali na Ki-moon, salamu zingine za pongezi zimetoka kwa Kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) cha nchini Kenya, Waziri Mkuu mstaafu wa nchi hiyo jirani, Raila Odinga kwenda kwa Watanzania na kipekee kwa Dk Magufuli, ambaye ni rafiki yake wa karibu. Katika salamu zake, Odinga ambaye ni Kiongozi wa Upinzani nchini humo, amesema Watanzania wengi wamemchagua Dk Magufuli kuongoza nchi yao na kusimamia hatma yao kwa miaka mitano ijayo kutokana na uwezo na uadilifu wake.

“Tafadhali pokea pongezi zangu za dhati, kwa niaba yangu na kwa niaba ya ODM na Wakenya. Naipongeza CCM kwa ushindi mkubwa na muungano wa vyama vya upinzani, kwa mapambano mazuri. “Ushindi wako ni matokeo ya kujitoa kwako bila kuchoka katika kutumikia nchi yako na chama chako. Pia ni mafanikio makubwa ya kampeni zako za kipekee,” amesema Odinga katika salamu hizo.

Amesema ukubwa na ubora wa kampeni za Dk Magufuli, umedhihirisha kukomaa na ubora wa demokrasia ya Tanzania na kuongeza kuwa, Dk Magufuli anaingia madarakani, wakati kukiwa na matarajio makubwa ya Watanzania kwake na kutoka kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. “Nakushauri uweke kipaumbele katika kudumisha umoja na ustahimilivu wa Watanzania na kuendeleza na kuongeza nguvu katika ushirikiano wa Afrika Mashariki na demokrasia ndani ya Bara la Afrika.

“Sisi Wakenya siku zote tumekuwa pamoja na Watanzania kwa historia, desturi na urafiki na ni matumaini yangu kuwa tunu hii ya kihistoria, itaimarisha ushirikiano kati ya nchi zetu mbili, chini ya uongozi wako,” amesema Odinga katika salamu hizo. Waangalizi waridhika Pongezi zingine zimetoka kwa Kiongozi wa Waangalizi wa Kimataifa kutoka Jumuiya ya Madola, Rais mstaafu wa Nigeria, Goodluck Jonathan, ambaye amesema mchakato wa Uchaguzi Mkuu umekuwa wa haki.

Kauli hiyo ya Jonathan ni sehemu ya mfululizo wa matamko ya waangalizi wa kimataifa yaliyoonesha kuridhika na mchakato mzima wa Uchaguzi Mkuu uliomalizika Jumapili iliyopita kwa Watanzania kupiga kura na kuhitimishwa jana kwa Dk Magufuli kukabidhiwa cheti na NEC, kuthibitisha ushindi wake.

Wengine waliokwishatoa tamko, ni waangalizi wa Jumuiya ya Ulaya (EU), waliosema uchaguzi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa umeendeshwa vizuri, ingawa kumekuwa na kasoro chache zilizosababisha baadhi ya wanasiasa kutilia shaka uhuru wa tume za uchaguzi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar.

Mwangalizi Mkuu wa Umoja huo wa Ulaya, Judith Sargentini, alisema waangalizi wa umoja huo waliofikia 141 waliotembelea vituo 625 vya upigaji wa kura, wataendelea kusalia nchini hadi Novemba 15 wakijihusisha na majukumu kadhaa ikiwamo kukutana na vyama vya siasa, maofisa wa uchaguzi wa asasi za kiraia. 

Waangalizi wengine kutoka nchi za Maziwa Makuu, nao walisema wameridhishwa na kutosheka na hali ya utulivu na kukomaa kwa demokrasia nchini, wakati wote wa kampeni licha ya kuwepo na tofauti za kisera.

Mkuu wa msafara wa waangalizi hao kutoka Wizara ya Mambo ya Nje nchini Kenya, Balozi Zachary Mumbuli, alisema lazima Watanzania wahakikishe wanapiga kura baada ya kumaliza kampeni kwa utulivu.

Alisema katika uangalizi wao, wameridhika kuwa maandalizi pia yako vizuri na nchi hizo 12 zinazounda Jumuiya ya Maziwa Makuu (ICGLR), wamepata mengi ya kujifunza hasa kufanyika kwa kampeni kwa utulivu licha ya tofauti za kisiasa. Balozi Mumbuli aliwasihi Watanzania kuendelea kukaa kwa utulivu na amani, kwani uchaguzi ni suala la muda hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha nchi inabaki kuwa kielelezo kwa nchi nyingine.

Alisema baada ya kuangalia mchakato mzima wa uchaguzi, wametosheka na hali ilivyo na kusisitiza kwamba kila mwananchi ahakikishe anakuwa mlinzi wa usalama wa kisiasa wa nchi, kwa kuwa bila usalama huo, ni dhahiri hakutakuwa na biashara na uchumi wa nchi na kila mmoja utaathirika. Akitambulisha wajumbe wa kundi hilo la waangalizi, Balozi Mumbuli alisema miongoni mwao, kuna viongozi wa vijana kutoka nchi za Maziwa Makuu, ambao waliokuja kuangalia mchakato wa Uchaguzi Mkuu unavyoendelea nchini, jambo ambalo limekuwa likifanyika kwa nchi zote wanachama wanapokuwa na uchaguzi.

Alisema jukumu kubwa ni kuendeleza jamii kwa kuwaunganisha vijana, akinamama na wafanyabiashara kwa kuhusisha sera za kisiasa na maendeleo ya makundi hayo, ili kustawisha nchi kwani biashara pasipo na usalama ni vigumu. *Uchaguzi wa Zanzibar Pamoja na kuridhika na Uchaguzi Mkuu, waangalizi hao na Umoja wa Mataifa, walitoa angalizo lao kuhusu kufutwa kwa Uchaguzi wa Zanzibar, kulikosababishwa na hitilafu ikiwemo ya kura kuzidi idadi ya wapigakura katika vituo vya kupigia kura.

Katibu Mkuu wa UN, Ki-moon katika taarifa yake, ametaka hitilafu yoyote iliyojitokeza katika mchakato wa uchaguzi wa Zanzibar, ufanyiwe kazi kwa kufuata sheria zilizopo kwa amani na kwa uwazi. “Katibu Mkuu amewataka wadau wote wa uchaguzi wa Zanzibar kuwa watulivu, waepuke ushawishi wowote wa kufanya vurugu na kujizuia kutoa matamko yoyote yanayoweza kuzidisha sintofahamu,” ameeleza Katibu Mkuu huyo wa UN. Rais mstaafu wa Nigeria, Goodluck Jonathan, alitaka suala la Zanzibar litatuliwe mapema na kwa amani ili kuepusha vurugu za kisiasa zinazoweza kujitokeza.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link