Home » » Warioba: Msichague wasiojua historia

Warioba: Msichague wasiojua historia

Written By CCMdijitali on Thursday, October 1, 2015 | October 01, 2015

Mzee wa Chama Cha Mapinduzi, Joseph Sinde Warioba.



WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amehadharisha umma wa Watanzania kuepuka kumkubali na kumchagua kiongozi asiyejua historia ya nchi, ilikotoka na ilipo. Akieleza kushangazwa na kile alichokiita ‘wimbo’ kwamba CCM haijafanya chochote katika miaka 54 tangu ipate huru, aliwashangaa zaidi watu wanaotumia jina la Mwalimu Julius Nyerere, mwasisi wa taifa, huku wakimuona dira, lakini wakisisitiza kwamba, hakufanya chochote.

Jaji Warioba alisema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, mjini hapa. “Tusipojua historia yetu… kama kuna kiongozi anakuja hajui historia ya nchi hii, tusije tukamkubali,” alisema Jaji Warioba. Aliendelea kusema, “Mtu yeyote ambaye hajui historia hiyo, hana haki ya kuomba uongozi,” alisema.

Warioba alisema ikichukuliwa historia hiyo, na kuangalia hali ya mwaka 1985 na kuilinganisha na mwaka 1961, atabaini mambo yaliyofanyika. “Ukiangalia Tanzania ambayo Mkapa (Rais Benjamin) aliiacha mwaka 2005 ni tofauti kabisa na jinsi Mwinyi alivyoiacha mwaka 1995,” alisema.

Hata hivyo alisema, zipo changamoto kwenye elimu, afya, maji, kilimo, miundombinu, ufugaji, uvuvi ambazo alisema, baadhi zinatokana na mafanikio. “Kama ni kiongozi, angalia msingi uliopo, anza kujenga huo msingi usije ukadharau kila kitu,” alisema na kuhoji, “Mtu gani anaweza asitambue maendeleo.”

Aliwataka wananchi kuhakikisha wanachuja mambo ya kampeni wanayoyasikia. “Mtu asije kuua historia ya nchi hii, ni lazima tuilinde historia ya nchi hii,” alisisitiza. Magufuli mzalendo Warioba ambaye alisema Magufuli ndiye anayefaa kuwa Rais kutokana na uzalendo wake wa kuhimiza amani, alieleza maeneo ambayo nchi ilipitia hadi kufika hatua hii ambayo hayapaswi kubezwa.

“Amekuwa (Magufuli) akisisitiza sana amani…sasa hasa vijana mnisikilize. Kwa sababu amani ililetwa na vijana, inalindwa na vijana, wazee huwa hawafanyi vurugu, akina mama huwa hawafanyi vurugu,” alisema na kuongeza kuwa kulinda amani ni lazima kufahamu ilivyokuja.

Akihimiza umma kuepuka kutenganishwa na mchakato, Jaji Warioba alieleza namna vijana na wazee walivyokutana katika miaka ya 1950 wakaunda Chama cha Tanu na kumchagua Mwalimu Nyerere awe kiongozi akiwa na umri wa miaka 32.

Alisema vijana hao ndiyo walioleta amani kwa kuunganisha watu wa makabila, dini zote likapatikana taifa moja na kuondoa ubaguzi wa kikabila na kiimani. Warioba aliendelea kusema vijana hao ndiyo waliounda Muungano wa Tanzania.

Aliwaambia vijana ndiyo taifa la leo na viongozi wa kesho. “Uchaguzi ni utaratibu wa kupata uongozi na siyo kututenganisha,” alisema Jaji Warioba. Alisema nchi ina kila sababu ya kumchagua Magufuli kwa kuwa ni mzalendo, anayehubiri amani muda mwingi.

“Wengine wanaona kama ni utani,” alisema Jaji Warioba na kusisitiza kuwa anaamini Magufuli ataunganisha na kuimarisha umoja wa nchi. Uadilifu, ufisadi Aidha, Jaji huyo mstaafu alisema kipindi hiki panahitajika mtu mwadilifu kutokana na ufisadi kuwa tatizo kubwa nchini.

Alisema anaamini Magufuli ndiye mwenye uwezo huo. Alimsifu namna ambavyo aliongoza wizara ya Ujenzi na kufanya kiwango cha rushwa katika wizara hiyo kupungua. Alitoa ushuhuda kwamba mwaka 1996, Rais Mkapa alimpa heshima ya kuwa mwenyekiti wa tume ya kuchunguza rushwa, ambayo miongoni mwa iliyobaini, rushwa kubwa ilikuwa kwenye sekta ya ujenzi.

Lakini, alisema tangu Magufuli alipoanza kuongoza wizara hiyo, rushwa imepungua katika sekta ya ujenzi. 

Alieleza kushangazwa na wapinzani, ambao alisema, anachoona CCM ndiyo inayofanya kazi kwao kwa kuwa wapiga debe anaowaona huko ni wa kutoka CCM.

Akihimiza wananchi kuhakikisha Oktoba 25 wanapiga kura, Jaji Warioba alisema, watu wengine kauli wanazotoa, ni za kujiandaa kukataa kura. Mkutano huo uliofurika watu, ulihudhuriwa na wanasiasa wakongwe, licha ya Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Warioba, ulihudhuriwa pia na Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela.

Wakongwe wengine waliohudhuria ni Pancras Ndejembi na Job Lusinde. Kimbisa: Magufuli hadaiwi fadhila Mwenyekiti CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa, alisema mgombea wa chama hicho, Dk John Magufuli hana deni la fadhila kwa kuwa hakuna mtu au kikundi cha watu watakaodai kwamba ndiyo waliomfikisha hapo.

“Hana deni la Kamati Kuu, nilikuwapo hakuna mjumbe wa kamati kuu atakayedai yeye ndiye yeye, nilikuwepo NEC hakuna aliyembeba… Halmashauri Kuu hana deni, Mkutano Mkuu hana deni. Nani anamdai Magufuli?,” alihoji Kimbisa. Wananchi wa Tanzania watamdai Magufuli fadhila.

“Naomba mumchague ili mpate muda wa kumtaka awalipe aliyowaahidi. Kimbisa alisema Magufuli ni mfuatiliaji na si mkali kama inavyodhaniwa na watu. Alihoji akifuatilia mishahara ya wafanyakazi, kwa watu wanaokula fedha , alihoji kama huo ni ukali au ufuatiliaji?

Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Malecela aliwashukuru wakazi wa Dodoma akisema mkoa huo kila wakati kunapokuwa na uchaguzi, huwa ni namba moja. “Wewe mwana Dodoma tunakuomba kazi yako iwe ni kumtafutia Magufuli kura kuanzia leo hadi Oktoba 25,” alisema.

Alisema katika safari ya kumpeleka Ikulu Magufuli, ni lazima wana Dodoma wawe mstari wa mbele, ikizingatiwa aliteuliwa mkoani hapa. Alisisitiza kuwa kura nyingi lazima zitoke hapa.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link