Home » » Kigwangalla: Lazima watu waumie kwanza

Kigwangalla: Lazima watu waumie kwanza

Written By CCMdijitali on Thursday, February 11, 2016 | February 11, 2016


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla



Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla amesema Watanzania hawana budi kukubali kuumia wakati huu ambao Rais John Magufuli anafanya mabadiliko kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Amesema hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Rais pamoja na mawaziri wake, zinalenga kuongeza uwajibikaji ili kuleta maendeleo nchini.


“Hakuna maendeleo bila mabadiliko ya kweli,” alisema Dk Kigwangalla katika mahojiano maalumu na Mwananchi mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita.


“Hatuwezi kutoka hapa kwenda pale bila kuwajibika, lazima tuumie. Safari za nje ni nzuri lakini kama hazina tija kwa nini ziwe nyingi kiasi hicho.

“Lazima kuwe na udhibiti na tujifunge mkanda ili tuweze kupata ustawi. Udhibiti ukianzia ngazi za juu, hata sisi (mawaziri) tutafuata nyayo za rais.”

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imekuja na mtindo tofauti, kwamba mabadiliko ni maumivu na siyo kitu cha starehe.


“Bila kuumia, hakuna mabadiliko. Lazima uende maili moja mbele kama kweli unataka mabadiliko,” alisema.


Kigwangalla alisema kufutwa kwa safari za nje, kufukuzwa na kusimamishwa kwa watumishi wa Serikali na mashirika ya umma ni sehemu ya mambo yanayofanywa na Rais pamoja na timu yake kuleta mabadiliko.

Tangu alipoapishwa Novemba 5 mwaka jana na baadaye kuteua baraza lake la mawaziri, Rais Magufuli na mawaziri wake wameshasimamisha au kufukuza watumishi 153 kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo kutowajibika ipasavyo, tuhuma za ufisadi na kukiuka maagizo.

“Utendaji kazi wa Serikali ya Rais Magufuli si nguvu ya soda,” alisema.

“Kitu kinachoifanya nchi kuwa bora ni wananchi kuamini kuwa kesho itakuwa bora zaidi kuliko jana. Kama wakipoteza matumaini wanakuwa hawana simile na wanaweza kufanya chochote.

“Hivi sasa watu wanaamini maisha yao yatakuwa bora kuliko leo wala jana. Jukumu la kuwafanya Watanzania kuwa na matumaini ni la Serikali. Tunaonyesha watu mikakati yetu na wanatuamini.”


Kuhusu safari za nje mbunge huyo wa Nzega Vijijini alisema: “Safari za nje katika Serikali iliyopita zilikuwa nyingi na kuitia hasara Serikali, hata faida yake haikuonekana. Alichokifanya Rais Magufuli ni kudhibiti safari za nje si kuzifuta.”

Alisema jambo hilo litasaidia kurejesha uwajibikaji ndani ya Serikali, huku akitoa mfano jinsi yeye alivyofunga geti la Wizara ya Afya, ili kuwaamsha watumishi wa wizara hiyo waliokuwa wamejenga utamaduni wa kuchelewa kazini.

“Awali ilikuwa ukienda wizarani unasota hata wiki mbili bila kuhudumiwa, lakini hivi sasa ukionekana tu unazungukazunguka unaulizwa shida yako,” alisema.


Kuhusu waliokumbwa na rungu la Rais Magufuli na kusimamishwa ama kufukuzwa kazi, Dk Kigwangalla alisema huo ni mwanzo wa kuamsha watu.


“Ni mwanzo wa kuwaamsha Watanzania na kubadilisha kifikra zao. Mabadiliko yoyote huanzia kwenye fikra za watu,” alisema.     


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link