Home » » UCHAMBUZI: SIKU 100 ZA JPM, Kigwangalla: Kasi ya Magufuli inalenga mabadiliko ya kweli

UCHAMBUZI: SIKU 100 ZA JPM, Kigwangalla: Kasi ya Magufuli inalenga mabadiliko ya kweli

Written By CCMdijitali on Saturday, February 13, 2016 | February 13, 2016

Dk Hamisi Kigwangalla akiapishwa na Rais John Magufuli kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Kwa ufupi

Ni Naibu Waziri ambaye alianza kazi saa chache baada ya kuapishwa na Rais kushika wadhifa huo, kwa kufanya ziara za ghafla hospitali za Mwananyamala na Amana

"Jana Dk John Magufuli alitimiza siku ya 100 tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndani ya siku hizo amefanya mambo mengi yaliyopongezwa na kukosolewa na watu wa kada"


By Fidelis Butahe, Mwananchi fbutahe@mwananchi.co.tz


Jana Dk John Magufuli alitimiza siku ya 100 tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndani ya siku hizo amefanya mambo mengi yaliyopongezwa na kukosolewa na watu wa kada mbalimbali.

Baada ya kuingia madarakani Novemba 5, mwaka jana, Rais Magufuli alitangaza hatua kadhaa za kubana matumizi yasiyo ya lazima, ikiwamo kufuta safari za nje na kupiga marufuku vikao vya kazi vya taasisi na mashirika ya umma kufanyika mahotelini.

Achana na kubana matumizi, rungu lake pia liliwasomba watu zaidi ya 70, wakiwamo watumishi na wajumbe wa bodi za mashirika au taasisi husika wakidaiwa ama kushindwa kuwajibika au kusimamia maeneo yao.

Walioangukiwa na ‘rungu’ hilo ni watumishi na viongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Wizara ya Uchukuzi.

Rais Magufuli ambaye kwa sasa ameteka sehemu kubwa ya mjadala nchini na nje ya nchi kutokana na kasi yake, alihutubia Bunge na kuahidi kutumbua majipu yote sugu, akimaanisha kushughulikia kuziba mianya ya ufisadi, urasimu na rushwa inazofanywa na watumishi wa Serikali wasiokuwa waaminifu wanaoshirikiana na wafanyabiashara kuhujumu mapato ya nchi.

Akizungumzia utendaji kazi wa Rais Magufuli, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla anasema kasi hiyo inalenga kurejesha uwajibikaji, kuondoa mazoea kazini, kuwataka Watanzania kukubali maumivu ili kuendana na kasi hiyo ya kuliletea taifa mabadiliko.

Yafuatayo ni mahojiano kati ya Dk Kigwangalla na mwandishi wa gazeti hili.


Swali: Unauzungumziaje utendaji kazi wa Rais Magufuli, watu wanasema kuwa ni nguvu ya soda, unasemaje kuhusu madai hayo?

Jibu: Kasi yake si nguvu ya soda maana kazi anayoifanya inaonekana. Wapinzani wanalalamika kwa sababu Serikali imebadilika na inafanya kazi kwa mtindo tofauti ambao unapendwa na wananchi.

Hapa namaanisha rais, Waziri Mkuu na mawaziri kuwa watendaji zaidi kunawafurahisha wananchi. Kitu kinachoifanya nchi kuwa bora ni wananchi kuamini kuwa kesho itakuwa bora zaidi kuliko jana.

Wananchi wakipoteza matumaini wanakosa uvumilivu, wanaweza kufanya chochote.

Chini ya Serikali ya Rais Magufuli watu wanaamini maisha yao yatakuwa bora kuliko leo wala jana. Jukumu la kuwafanya watanzania kuwa na matumaini ni la Serikali. Tunaonyesha watu mikakati yetu na wanatuamini. Tunasema jambo kwa kumaanisha na tunaaminiwa.

Swali: Unazungumziaje watumishi wa umma kufukuzwa au kusimamishwa kazi, je ni sahihi na ni kweli taratibu zinafuatwa?

Jibu: Huo ndio mwanzo wa kuwaamsha Watanzania. Anachokifanya rais na watendaji wake ni kubadilisha muundo wa kifikra wa Watanzania. Mabadiliko yoyote huanzia kwenye fikra za watu.

Siku hizi watu wanafunga biashara zao mapema kwa sababu ya kuhamasika na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu. Mfano mimi nilifunga getu pale wizara ya afya baada ya kubaini wafanyakazi wanachelewa, tangu wakati huo mpaka sasa watu wanawahi kazini.

Anachokifanya rais na mawaziri wake ni kuchukua hatua ya moja kwa moja kwa watu watakaobainika kuwa si waadilifu au kushindwa kazi na kuweka wengine watakaofanya kazi kwa mtindo utakaoleta tija kwa wananchi.

Baadhi ya watu wanalalamikia utendaji kazi huu kwa sababu majibu yanayotumbuliwa ni ya rafiki zao, wao wenyewe au ndugu. Rais aendelee kutumbua majibu ili watu watoke katika usingizi. Watu wanapaswa kutambua kuwa zama hizi ni tofauti, yaani ukikosea asubuhi unafukuzwa jioni. Watu waheshimu kazi katika ofisi za umma.

Si kwamba wote wanafukuzwa, wapo wanaosimamishwa kazi au kuwekwa pembeni na kufikishwa mahakamani. Hakuna aliyeonewa wala kusingiziwa.

Mfano Wizara ya Afya tulimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Taasisi ya Ocean Road baada ya kubaini kuwa naye ana hospitali inayotoa huduma kama za taasisi hii. Huu ni mgongano wa kimaslahi maana unaweza kukuta hospitali yake ina dawa kuliko zilizopo Ocean Road.

Hatuwezi kumfukuza kazi tutachunguza kwanza. Mkibaini mnaweza kumuweka kando kwa maana ya kutokuwa kiongozi tena, ila kazi ataendelea nayo kama kawaida na mshahara wake utakuwa ule ule.

Swali: Kuna madai kuwa Baraza la Mawaziri la Rais Magufuli limepunguza gharama za Serikali una maoni gani?

Jibu: Gharama zimepungua kwa asilimia kama 40 hivi. Serikali iliyopita ilianza na mawaziri kama 60 hivi ila Rais Magufuli kaanza na mawaziri 34 tu. Najua atakuwa na changamoto ya kulaumiwa na marafiki na jamaa kutokana na kutowateua katika Serikali yake. Ninachokiona ameteua watu wachache watakaofanya kazi, ameunganisha wizara ili kupunguza gharama na itifaki katika mawizara.

Watu wana tazama hizi gharama kwa mitindo mingi, wapo wanaohoji idadi ya makatibu wakuu ambao binafsi naona wamepungua.

Mimi ninachofahamu, ukiwa na mawaziri na naibu mawaziri wengi maana yake umeongeza gharama. Kama ukiunganisha wizara na ngazi ya chini ukawaacha wataalamu kufanya kazi zao utapunguza gharama.

Mfano wizara ya Afya, kuna waziri wawili na Katibu Mkuu wa Afya na wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Makatibu hawa wawili hawana manaibu na kwa kufanya hivyo unakuwa tayari umepunguza gharama.

Kwa mtindo uliokuwa zamani, maana yake Wizara ya Afya ingekuwa na waziri na naibu waziri na ile ya Maendeleo ya Jamii nayo ingekuwa na mawaziri wawili na makatibu wakuu wawili.

Kitendo cha Wizara ya Afya kuunganishwa na ile ya Maendeleo ya Jamii maana yake Rais Magufuli kapunguza idadi ya mawaziri wawili na makatibu wakuu wawili, hapo maana yake hata magari yaliyopaswa kutumiwa na watu hao nayo hayatatumika tena.

Hakutakuwa na gharama za matengenezo ya magari jambo ambalo wakati nikiwa mbunge nilikuwa nikilisema sana. Kuunganisha wizara hizi kumepunguza posho walizopaswa kulipwa madereva wa mawaziri na wasaidizi wao maofisini.

Wapo wanaosema kuwa na makatibu wakuu hakujapunguza gharama! Napingana na mtizamo huo kwa sababu itifaki ya kumhudumia katibu mkuu si kama ya kumhudumia waziri maana Katibu Mkuu hana msaidizi, mlinzi, msaidizi wa ofisini, wahudumu wa ofisini na nyumbani.

Swali: Nini faida kwa Rais Magufuli kudhibiti safari za nje na nini hasara?

Jibu: Kudhibiti safari za nje ni jambo zuri ninaliunga mkono. Tunapunguza matumizi kwa kiasi kikubwa maana tumejifunza katika Serikali iliyomaliza muda wake, ambayo safari za viongozi zilikuwa nyingi na kuitia hasara Serikali. Hata faida yake hatukuiona.

Rais Magufuli anataka kudhibiti safari za viongozi na watumishi wa umma. Anachuja na kushauriwa na watu wake wa karibu kutokana na umuhimu wa safari husika. Hii inasaidia kuleta uwajibikaji kwenye serikalini, binafsi napenda uwajibikaji na ndio maana nilifunga mageti pale wizarani.

Naamini hatuwezi kupata ustawi bila kuwajibika. Hatuwezi kusonga kutoka hapa tulipo kwenda mbele bila kuwajibika na katika hilo lazima tuumie.

Safari za nje ni nzuri lakini kama hazina tija kwanini ziwe nyingi kiasi hicho. Lazima kuwe na udhibiti na tujifunge mkanda ili tuweze kupata ustawi. Udhibiti ukianzia ngazi za juu hata sisi wa chini tutafuata nyayo za rais.

Serikali inafanya kazi kwa vitendo, kufika kwa wananchi ili waone kazi tunazozifanya. Siku za hivi karibuni ilikuwa ukienda wizarani unasota hata wiki mbili bila kuhudumiwa lakini kwa sasa watumishi wanaheshimu ofisi na wanawahudumia wananchi.

Huo ndiyo wajibu wa kazi. Ukitizama kwa makini utabaini kuwa Serikali imekuja na mfumo tofauti hivyo lazima watu wabadilike, wabanwe na wadhibitiwe. Tutaumia mwanzoni tu. Hivi sasa ni vigumu kwa mfanyakazi wa Serikali kuingia ofisini saa tatu asubuhi.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link