Home » » Uhamiaji wasafishwa Dar na Kilimanjaro

Uhamiaji wasafishwa Dar na Kilimanjaro

Written By CCMdijitali on Wednesday, February 24, 2016 | February 24, 2016

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga

Na Habari Leo

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga ameagiza watumishi wa Idara ya Uhamiaji walioko katika viwanja vya ndege vya kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam na Kilimanjaro (KIA), wahamishwe na kupelekwa maeneo mengine nchini, wakiwemo wale wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Katika maagizo ya waziri huyo, amesisitiza kuwa anataka kuwepo na mabadiliko makubwa katika vitengo mbalimbali vya idara ya uhamiaji ili kuboresha huduma na kuimarisha uadilifu katika vitengo hivyo.

Aidha, utafiti uliofanywa hivi karibuni, umeonesha kuwa matatizo ya rushwa katika idara ya uhamiaji, yanashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na asilimia 30, asilimia 20 ni uongozi mbovu na asilimia 20 ni matumizi mabaya ya madaraka.

Kitwanga alitoa maagizo hayo Dar es Salaam jana, alipozungumza katika kikao cha ndani na viongozi wa idara ya uhamiaji na viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wakiwemo Wakuu wa Idara na Vitengo vya Wizara.

Pamoja na watumishi hao wa Idara ya Uhamiaji wa viwanja hivyo vya ndege kutakiwa kuhamishwa, wengine walioagizwa na waziri huyo kuhamishwa ni kutoka Kitengo cha Pasipoti, Uhasibu, Hati za Ukaazi na Kitengo cha Upelelezi, vyote vya Makao Makuu ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam.

Aidha, ameagiza pia kuwa Wakuu wote wa Vitengo vya Upelelezi vya wilaya zilizopo jijini Dar es Salaam, Tunduma, Mtukula, Holili na Kasumulo, wahamishiwe maeneo mengine, wakiwemo watumishi wote waliokaa kwa zaidi ya miaka mitatu katika vituo hivyo.

“Hatua hii inayochukuliwa ni mwanzo tu wa mabadiliko makubwa yatakayofanywa katika Idara ya Uhamiaji ili kuboresha huduma zinazotolewa na Idara hii ambayo ni moja ya Idara muhimu za Serikali,” alisisitiza Kitwanga.

Alisema katika kuisafisha idara hiyo, uangalifu mkubwa utachukuliwa ili kuhakikisha kuwa hakuna mtumishi anayeonewa wala kupendelewa, lengo likiwa ni kuvunja mtandao wa wapokea rushwa na wasiowajibika.

Alisema kutokana na utafiti uliofanywa hivi karibuni, umeonesha kuwa matatizo ya rushwa katika Idara ya Uhamiaji yanashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na asilimia 30, asilimia 20 ni uongozi mbovu na asilimia 20 ni matumizi mabaya ya madaraka.

Aidha, alisema asilimia 15 inahusisha vitendea kazi, mifumo hafifu ya kufanya kazi, asilimia 10 huduma mbovu na asilimia tano ukabila na upendeleo.

Aliwataka viongozi na watumishi wote katika idara hiyo kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya kazi na kuepuka vitendo vya kupokea rushwa na kusaidia wahamiaji haramu na wauza dawa za kulevya.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link