Imeandikwa na Halima Mlacha -Habari Leo
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha maslahi ya wanahabari na tasnia ya habari nchini vinalindwa na kupewa uhuru wa kutosha lakini kwa kutanguliza maslahi ya taifa.
Pia amebainisha kuwa Muswada wa Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari uko katika hatua za mwisho baada ya kushirikisha na kujumuisha mapendekezo ya wadau wa habari na kusisitiza kuwa endapo sheria hiyo itapitishwa itakuwa ni sheria bora itakayoijenga tasnia hiyo na itadumu kwa muda mrefu.
Amevitaka vyombo vya habari nchini kutumia fursa iliyopo kuibua matatizo yaliyopo kwenye jamii na hivyo Serikali kuvitumia kama sehemu ya kupatia taarifa na kuzifanyia kazi kwa maslahi ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Nape aliyasema hayo juzi usiku katika kipindi cha Siku 100 za Rais John Magufuli madarakani katika sekta ya habari, utamaduni, sanaa na michezo kilichorushwa na televisheni ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Alisema tangu Rais John Magufuli aingie madarakani amekuwa akiishi yale anayoyazungumza na hivyo ndivyo Serikali yake itakavyokuwa kwani hata yeye tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa Habari aliahidi kuijenga na kuilinda tasnia hiyo jambo ambalo ameapa kulifanikisha.
“Nawahakikishia wanahabari kwamba wako salama chini ya Serikali ya Awamu ya Tano na uongozi wake,” alisisitiza.
Alisema alipoanza kazi ya uwaziri, alikutana na makundi mbalimbali ya wadau wa habari wakiwemo wanahabari na wahariri wa habari lengo likiwa ni kukusanya na kuangalia mambo ambayo hayako sawa katika tasnia hiyo na kupokea maoni yao yaingizwe kwenye Muswada wa Sheria ya Habari.
Alisema kupitia maoni aliyoyakusanya kutoka katika makundi hayo ya wadau wa habari, mapendekezo yao yamefanyiwa kazi kwa kutumika kwenye muswada wa sheria hiyo ya habari ambayo iko katika hatua za mwisho na inatarajiwa kuwasilishwa bungeni.
Alisema sheria hiyo ya habari kwa kuzingatia mapendekezo hayo, itakuwa ni sheria nzuri, bora na itakayoijenga tasnia ya habari, na ni sheria itakayochukua muda mrefu kufanyiwa marekebisho kutokana na ubora wake.
Akizungumzia uhuru wa vyombo vya habari, alisema uhuru huo ulianza kupanuliwa tangu Serikali zilizopita ikiwemo ya Awamu ya Nne na umekuwa ukitekelezwa kwa kuzingatia sheria zilizopo za habari na maslahi ya taifa.
Alisema ndani ya Serikali ya Awamu ya Nne, uhuru wa vyombo vya habari nchini ulipanuliwa kwa wigo mkubwa ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika.
“Najua kumekuwa na malalamiko mengi hasa ndani ya siku hizi 100 za Mheshimiwa Rais, pale nilipolifungia gazeti la Mawio. Nilichukua hatua ile baada ya kupitia kwa umakini mwenendo mzima wa gazeti lile na kwa kweli lilikuwa na makosa na ndio maana hata baada ya hatua kuchukuliwa, Mawio wenyewe hawapigi kelele wanaopiga kelele ni wengine,” alisisitiza.
Alisema gazeti lile mwenendo wake wa uandishi ulikuwa hauendani na maadili ya uandishi wa habari na kukiuka sheria ya vyombo vya habari kupitia taarifa zake mojawapo ikiwemo ya kumtangaza kinyume cha Sheria ya Uchaguzi mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad kuwa ndiye Rais mteule wa Zanzibar.
Aidha, alisema pia alifuatilia mwenendo wa namna gazeti hilo linavyojibu barua za kulionya na kuonekana kama linajibizana na Msajili wa Magazeti na hata lilipoandika habari ya kumtangaza Maalim Seif kuwa Rais wa Zanzibar, majibu yake ya kujieleza yalikuwa ni ya kejeli na kiburi.
“Walipoandikiwa barua ya kujieleza kuhusu habari hiyo yenye uchochezi, walijibu eti wanaishangaa Serikali kwa nini inahoji wao kumtangaza mshindi Zanzibar, na kusisitiza kuwa walipaswa kupongezwa. Huu ni uhaini kutangaza Rais bila kuwa na mamlaka. Huu ni uchochezi na ndio maana tulichukua hatua,” alisema Nape.
Alisema pamoja na kwamba sheria iliyotumika kulifungua gazeti hilo inalalamikiwa akiwemo yeye mwenyewe kutoridhika nayo, ni vyema vyombo vya habari vitakatambua kuwa sheria hiyo bado ipo hadi pale utakapopitishwa Muswada wa Sheria ya Habari.
Alivitaka vyombo vya habari kuitekeleza kwa vitendo changamoto aliyoitoa Rais Magufuli wakati akizungumza na wazee hivi karibuni, kwa kuandika habari za utafiti zinazoibua masuala nyeti yanayohitaji kufanyiwa kazi na Serikali kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
“Hata mheshimiwa Rais Magufuli alisema tutumie vyombo vya habari kupata taarifa muhimu za kufanyia kazi. Ili Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk Magufuli ifanikiwe, ni lazima itoe uhuru wa kutosha kwa vyombo vya habari kufanya kazi zake,” alisema Nape.
Katika hatua nyingine, Nape amesema Serikali imejipanga kuhakikisha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linakuwa chombo cha kuaminika na linafanya kazi zake kuendana na kasi ya utendaji wa Serikali hiyo.
Aidha, amesema imepanga kuanza kulipa madeni yote ambayo shirika hilo na Shirika la Magazeti ya Serikali, Tanzania Standard Newspapers (TSN) wachapishaji wa magazeti ya Daily News, SpotiLeo na HabariLeo, inaidai Serikali ili mashirika hayo yajiendeshe kwa ufanisi.
Nape alisema katika kufanikisha azma hiyo tayari akiwa Waziri mwenye dhamana ameunda Bodi mpya ya TBC na Rais Magufuli ameshamteua Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Balozi Herbert Mrango baada ya Bodi iliyopita kumaliza muda wake kwa mujibu wa sheria.
“Tunataka TBC kuwa chombo cha umma kinachoaminika nchini kuanzia kwenye vipindi na taarifa za habari na matukio. Kila Mtanzania anaona kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano. Ni kasi kubwa hata taasisi zilizo chini ya wizara zetu ikiwemo TBC, tunataka ziende na kasi hiyo,” alisisitiza Nape.
Pamoja na hayo, Waziri Nape alisema Serikali inatambua kuwa shirika hilo linakabiliwa na tatizo la uchakavu wa mitambo na kukabiliwa na madeni makubwa ambayo taasisi za Serikali zinadaiwa na kuahidi kulifanyia kazi.
“Tayari Rais Magufuli ameagiza madeni yote ambayo TBC inadai taasisi za Serikali yaanze kulipwa pamoja na madeni ambayo Shirika la Magazeti la Serikali (TSN) linazidai taasisi hizo. Mashirika haya yanaidai Serikali fedha nyingi inabidi yalipwe ili yafanye kazi zake kwa ufanisi,” alisisitiza.