By Nuzulack Dausen, Mwananchi
Dar es Salaam. Kasi ya utendaji wa Rais John Magufuli
imezidi kuibua matumaini mapya kwa Watanzania baada ya sehemu kubwa kuridhishwa
na utendaji wake katika siku 100 za mwanzo wa uongozi wake.
Ripoti ya utafiti mpya iliyotolewa jana imebainisha kuwa
katika siku hizo, takribani watu wanane kati ya 10 wameridhishwa na utendaji wa
jumla wa Dk Magufuli na wana matumaini atafanya vizuri siku zijazo.
Katika utafiti huo uliofanya na timu ya watafiti kutoka kampuni
mbili za utafiti za Infotrak Reserch & Consulting na Midas Touche’ East
Africa, Rais alipata wastani wa asilimia 84.1 ya alama zilizokuwa zinapima
utendaji wa ujumla.
Utafiti huo umehusisha sampuli ya watu 1,200 wenye umri wa
zaidi ya miaka 18 ikiwa ni uwakilishi wa Watanzania 24.25 milioni wa kundi hilo
na kufanyika katika kanda sita nchini ndani ya mikoa 15 ya Tanzania Bara na
Zanzibar.
Kanda hizo ni Pwani, Kanda ya Ziwa, Kaskazini, Kusini,
Zanzibar na Kati. Ripoti hiyo inabainisha kuwa Rais alipata wastani wa asilimia
81. 9 katika kigezo cha kuheshimu sheria na utawala bora, huku akipata asilimia
78.9 katika usimamizi wa uhuru wa habari na uhuru wa kutoa maoni.
“Katika kigezo cha urafiki kwa vyombo vya habari, Rais
Magufuli alipata wastani wa 76.1 ya alama zote wakati katika msisitizo katika
masuala ya kimataifa, ikiwamo Jumuiya ya Afrika Mashariki amepata wastani wa
asilimia 77.8,” inasema ripoti hiyo.
Kuhusu utafiti
Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ndiyo
iliyoomba kufanyika kwa utafiti huo uliohusisha mahojiano ya ana kwa ana kwa
kusaidiwa na mfumo wa kompyuta, ili kupata maoni yenye uwakilishi halisi juu ya
utendaji wa Serikali ya awamu ya tano ndani ya siku 100 za mwanzo. MCL
inachapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.
Matokeo ya utafiti yanabainisha kuwa Dk Magufuli huenda
ndiye rais aliyepata alama za juu za kukubalika zaidi baada ya uchaguzi
kutokana na watu tisa kati ya 10 kuonyesha kuridhishwa namna anavyoendesha
Serikali.
“Asilimia 9.6 pekee ya waliohojiwa ndiyo waliona kuwa Rais
haendeshi vizuri Serikali na sehemu kubwa ya kundi hili ni wale wenye umri wa
kati,” inasema ripoti hiyo ya utafiti uliofanyika kati ya Februari Mosi hadi
Februari 7 mwaka huu.
Rais Magufuli ameonekana kuaminika zaidi na akina mama ambao
asilimia 93.1 waliohojiwa wanaona anaiendesha vizuri Serikali dhidi ya asilimia
88 ya wanaume.
Umaarufu wa Rais unaonekana kushamiri zaidi vijijini ambako
asilimia 91.5 ya waliohojiwa kutoka maeneo hayo waliridhishwa na utendaji wake
dhidi ya asilimia 88.2 ya wakazi wa mjini.
Mikakati ya awali ya kiuchumi aliyoanza kuitekeleza Dk
Magufuli imezidi kumuongezea imani kwa wananchi ambapo watu nane kati ya 10
wanaamini kuwa atabadilisha hali mbaya ya kichumi nchini.
Ikumbukwe kuwa alipoingia tu madarakani Novemba 5, 2015,
Rais alianza kutekeleza mikakati migumu ya kubana matumizi ya fedha za Serikali
ikiwamo ya kupiga marufuku safari za nje hadi kwa kibali maalum na taasisi za
umma kutokodi kumbi za mikutano mahoteli badala yake watumie majengo ya
Serikali.
Njia hizo zilimpatia pia umaarufu nje ya mipaka ya nchi
kiasi cha mitandao ya kijamii kuibua kiunganishi kilichotamba katika mtandao wa
Twitter kwa kiingereza “@WhatWould Magufuli Do (MagufuliaAngefanyaNini)
kikihamasisha watu kufikiri kubana matumizi kabla ya uamuzi wa kutumia fedha.
Walipoulizwa wananchi katika kigezo hicho cha kudhibiti matumizi mabaya ya
fedha za umma, utafiti huo unabainisha kuwa watu tisa kati ya 10 wanaridhishwa
na utekelezaji wa ahadi hiyo huku asilimia kubwa wakiwa ni wenye umri kati ya
miaka 36 hadi 45.
Kwa muda mrefu rushwa na ufisadi vimekuwa jipu sugu
serikalini na Rais alianza kushughulikia suala hilo kwa kuwasimamisha kazi au
kutengua uteuzi wa vigogo wanaotuhumiwa kwa ufisadi, wakiwamo vigogo wa taasisi
nyeti kama Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
na Takukuru.
Katika swali la wananchi wanazionaje jitihada za kubaini na
kupambana na rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma, watu tisa kati ya 10
walionyesha kuridhishwa na mikakati ya Rais katika kutokomeza janga hilo.
“Watu tuliowahoji wanaona kwamba hatua alizochukua Dk
Magufuli hivi karibuni za kupambana na rushwa ni salamu kwa watumishi wazembe
na wabadhirifu,” inasema ripoti hiyo.
Hotuba ya Rais wakati wa ufunguzi wa Bunge la 11 aliyoitoa
Novemba 19 mwaka jana bado inaishi miongoni mwa wananchi licha ya kutolewa
zaidi ya miezi mitatu iliyopita kutokana na kukubalika zaidi na wananchi.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa asilimia 89.2 ya waliohojiwa
walikiri kuwa hotuba hiyo iligusa maeneo muhimu ambayo yamekuwa yakirudisha
nyuma maendeleo ya nchi.
Mbali na kupima mtazamo wa wananchi juu ya ahadi mbalimbali
za Serikali ya Awamu ya Tano, ripoti hiyo imeanika mtazamo wa wananchi juu ya
mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa katika sekta mbalimbali zikiwamo za elimu,
afya, uchumi, uzalishaji wa ajira, mapambano dhidi ya rushwa na miundombinu.
Matokeo hayo yanabainisha kuwa hadi sasa Serikali
imefanikiwa katika elimu kwa asilimia 47, afya (19.7), vita dhidi ya rushwa
(15.6), uchumi (3.3), miundombinu (2.7) na uzalishaji wa ajira asilimia 2.1.
Hata hivyo, Dk Magufuli kwa mujibu wa utafiti huo, amefanya vibaya zaidi katika
masuala ya utalii, upatikanaji wa maji safi na salama, uwezeshaji wa wanawake,
utatuzi wa mgogoro wa Zanzibar, ulinzi na usalama na madini.
Wananchi bado wanaona Rais anatakiwa aweke mkazo zaidi
katika masuala ya elimu, afya, ajira, uchumi, kilimo na kupunguza gharama za
maisha, kwa mujibu wa utafiti huo.
Katika kupima ubora wa uteuzi wa Baraza la mawaziri, wananchi
wamemkubali Rais Magufuli kwa kumteua Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu kwa
asilimia 90 huku wakikubali udogo wa baraza la mawaziri.