Home » » Yanga ni ushindi tu

Yanga ni ushindi tu

Written By CCMdijitali on Sunday, February 14, 2016 | February 14, 2016

Kikosi cha Yanga  1-0  Cercle de Joachim ya Mauritius
 
WAWAKILISHI wa Tanzania Bara katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Yanga wameanza vizuri michuano hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius katika mechi iliyochezwa jana.

Bao pekee la Yanga katika mchezo huo wa hatua ya awali lilifungwa na mshambuliaji wa kimataifa raia wa Zimbabwe Donald Ngoma dakika ya 17 akiunganisha krosi ya Juma Abdul.

Ushindi huo wa ugenini unaifanya Yanga kuwa na kazi nyepesi katika mchezo wa marudiano ambao unatarajiwa kuchezwa wiki mbili zijazo kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Awali kabla ya kuanza kwa pambano hilo kulikuwa na hofu kwamba huenda lingesogezwa mbele kutokana na mvua kubwa kunyesha na maji kujaa uwanjani lakini baada ya muda mambo yalikaa sawa na mchezo huo kuendelea.

Pamoja na mvua kuharibu ladha ya mchezo kwa wachezaji kuteleza mara kwa mara lakini Yanga walionesha soka safi na kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la wenyeji wao Cercle de Joachim, ambao safu yao ya ulinzi ilifanya kazi kubwa ya kuwadhibiti washambuliaji wa wageni wao.

Wenyeji Cercle de Joachim, pamoja na kufungwa bao la mapema lakini walionekana ni timu nzuri kutokana na uwezo mkubwa waliouonesha na kuwasumbua Yanga, na kipa Ally Mustaph ‘Barthez’ kufanya kazi kubwa ya kuokoa mashambulizi hayo.

Mshambuliaji Amissi Tambwe, atalazimika kujilaumu kwa kushindwa kuipa ushindi mnono timu yake baada ya kupoteza nafasi mbili za wazi katika mchezo huo ambao kama angezipata timu yake ingepunguza presha katika mchezo wa marudiano ambao utapigwa wiki mbili zijazo jijini Dar es Salaam.

Kocha wa Yanga Hans van der Pluijm, na msaidizi wake Juma Mwambusi, walionekana wakali kutokana na kusimama mara kwa mara kutoa maelekezo kwa wachezaji wao ili kulinda bao hilo lisirudi kutokana na kasi waliyokuwa nayo wapinzani wao.

Kipindi cha pili Yanga ilionekana kucheza kwa kujihami zaidi wakilinda bao lao huku wakifanya mashambulizi ya kustukiza ambayo mara kadhaa yalikuwa na madhara makubwa kwa we nyeji wao Cercle de Joachim, lakini hata hivyo waliyahimili.

Katika dakika ya 56 beki Abdul aliumia na kushindwa kuendelea na mchezo na nafasi yake ilichukuliwa na Patto Ngonyani ambaye aliweza kuumudu mchezo huo ingawa ulikuwa mchezo wake wa kwanza wa kimataifa tangu atue Yanga. Ushindi huo unaifanya Yanga kuhitaji anagalau sare katika mchezo wa marudiano ili waweze kusonga mbele raundi ya kwanza ambapo mechi zake zitapigwa kuanzia Machi mwaka huu.

Kikosi kamili cha Yanga kinachokwenda kambini Pemba :

Makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benedicto Tinocco.

Mabeki; Juma Abdul, Mbuyu Twite (DRC), Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Vincent Bossou (Togo) na Pato Ngonyani.

Viungo ni; Said Juma ‘Makapu’, Salum Telela, Thabani Kamusoko (Zimbabwe), Haruna Niyonzima (Rwanda), Simon Msuva, Issoufou Boubacar (Niger), Godfrey Mwashiuya na Deus Kaseke.

Washambuliaji ni; Malimi Busungu, Paul Nonga, Amissi Tambwe (Burundi) na Donald Ngoma (Zimbabwe).

BENCHI LA UFUNDI; Kocha Mkuu; Hans van der Pluijm (Uholanzi), Kocha Msaidizi; Juma Mwambusi, Kocha wa Makipa; Juma Pondamali

Daktari; Nassor Matuzya, Meneja; Hafidh Saleh, Mchua Misuli; Jacob Onyango na Mtunza Vifaa; Mohammed Mpogolo.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link