Home » » Singapore kuboresha Bandari ya Dar

Singapore kuboresha Bandari ya Dar

Written By CCMdijitali on Thursday, April 28, 2016 | April 28, 2016

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Singapore, Dkt. Koh Poh Koon (kulia kwake) na ujumbe wake, Ofisini kwake bungeni mjini Dodoma Aprili 27, 2016. Kulia ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Singapore, Dkt. Koh Poh Koon (kulia ) na ujumbe wake kabla ya mazungumzo yao , Ofisini kwake bungeni mjini Dodoma Aprili 27, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 Habari leo

WAZIRI wa Biashara na Viwanda wa Singapore, Dk Koh Poh Koon amesema wamepanga kutumia Bandari ya Dar es Salaam kuwa kiunganishi cha biashara kati ya nchi hiyo na mataifa mengine ya Afrika Mashariki (EAC).

Dk Koon aliyasema hayo jana wakati alipomtembelea Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ofisini kwake mjini Dodoma, na kwamba Singapore ipo tayari kutoa fursa kwa wataalamu wa Tanzania kwenda kufanya kazi katika Bandari ya Singapore ili kupata uzoefu utakaosaidia uendeshaji wa bandari za Tanzania.

Dk Koon ambaye ameambatana na wafanyabiashara wakubwa wapatao 40, alimweleza Waziri Mkuu kwamba Kampuni ya Hyflux ya Singapore, imeanza kuwekeza nchini kwa kujenga eneo maalumu la uchumi mkoani Morogoro, ambako ndani ya kipindi cha miaka mitano wanatarajia kujenga miundombinu wezeshi ya kuweka viwanda vya kati, maeneo ya biashara na nyumba za makazi zipatazo 37,000.

“Jiwe la msingi la mradi huo litawekwa tarehe 29 Aprili 2016 na Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage,” alisema waziri huyo wa Singapore.

Mbali na ushirikiano katika sekta ya biashara na uwekezaji, Dk Koon alimweleza Waziri Mkuu kwamba nchi yake itaisaidia Tanzania kujenga uwezo wa kiufundi katika maeneo mbalimbali ya menejimenti na uendeshaji wa bandari na ufundi katika sekta ya gesi na mafuta.

“Hadi sasa makampuni ya Singapore yaliyowekeza nchini ni pamoja na Pavillion Energy ambayo imewekeza kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.2 katika sekta ya gesi na inatarajia kuwekeza zaidi dola za kimarekani bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa kinu cha kuchakata gesi (LNG plant) kitakachojengwa mikoa ya Kusini kwa ubia na makampuni ya gesi kutoka Ulaya na Marekani,” alifafanua.

Alisema Kampuni ya PIL ya Singapore inatarajia kuwekeza Dola za Marekani milioni 400 kwa ajili ya kuanzisha kituo cha kutoa huduma kwa kampuni ya gesi. Alisema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa hayo pamoja na kuweka mikakati ya kuinua uchumi na kupanua wigo wa biashara.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Majaliwa aliishukuru Serikali ya Singapore kwa uwekezaji unaofanywa na kampuni zake nchini na kwa misaada ya kiufundi ambayo wameitoa kwa Tanzania katika nyanja mbalimbali.

Ili kusaidia juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kukuza uchumi, Waziri Mkuu amezikaribisha kampuni nyingine za Singapore kuja nchini kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda, mahoteli, kilimo na nishati.

Alimuahidi Dk Koon kwamba Tanzania ipo tayari kukamilisha mazungumzo ya kusaini Mkataba wa Kuvutia na kulinda uwekezaji baina ya nchi mbili na Mkataba wa Kuepuka kutoza ushuru mara mbili ili kuvutia uwekezaji zaidi kutoka Singapore.

Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka Watanzania kutumia fursa ya ushirikiano kati ya Singapore na Tanzania, kuanzisha biashara mpya zitakazowanufaisha wote.

Alisema Singapore ina uwezo mkubwa kibiashara pamoja na uzoefu wa siku nyingi kwenye uendeshaji wa bandari hivyo Tanzania itapata nafasi ya kujifunza namna ya uendeshaji katika sekta hizo.

Alisema Tanzania imefungua milango ya uwekezaji kwa wafanyabiashara wa Singapore, kuja kuwekeza katika sekta za viwanda, usafiri wa anga na kwenye Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo Nje (EPZ).
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link