Imeandikwa na Regina Kumba - Habari Leo
BARAZA la Wazee la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) limemuombea dua Rais John Magufuli awe na afya njema na aendelee kutumikia katika misingi inayompendeza Mungu.
Dua hiyo ilitolewa jana ikiongozwa na Mwenyekiti wa baraza hilo, Hashim Juma katika mkutano na waandishi wa habari uliokuwa na lengo la kueleza namna ambavyo hawaridhishwi na mwenendo wa utendaji kazi wa Rais Magufuli na yaliyojiri Zanzibar.
Hashim alisema pamoja na kwamba baraza hilo haliridhishwi na mwenendo wa Rais Magufuli, limeamua kumuombea dua kwa sababu rais mwenyewe aliomba kuombewa.
“Tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe afya njema, ampe maisha marefu na amjalie aongoze katika misingi anayopenda yeye, amina,” alisema Hashimu wakati akiongoza dua na wazee wengine kuitikia amina.
Hata hivyo, awali Hashim aliituhumu serikali ya Magufuli akisema inakandamiza upinzani na pia haendeshwi katika misingi ya kidemokrasia.
“Katika mkesha wa Krismasi mwaka jana, Rais aliomba tumuombee dua, kwa sababu ameomba mwenyewe na jambo hili la kuomba dua ni jambo kubwa, hatuna budi kumuombea,” alisema Hashim.
Alisema Rais Magufuli amekuwa na kauli tata ambazo amekuwa akizungumza hadharani lakini viongozi na wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameshindwa kukemea na wao hawawezi kukaa kimya.
Hashim alisema baraza hilo linamshauri Rais aunde kamati ya wazee wa kumshauri ambao atakutana nao walau mara nne kwa mwaka kutoka mikoa yote na ikizingatia jinsia.
Alisema baraza hilo linamshauri pia rais ashughulikie kupatikana kwa Katiba ya nchi, na mapambano dhidi ya ufisadi na rushwa, “bila kupatikana katiba mpya ufisadi ambao anaupiga vita hautaisha,” alisema Hashim.
Aidha baraza hilo lilimtaka rais kuingilia kati mgogoro wa wabunge wa upinzani waliosusa vikao vya Bunge ili warudi bungeni.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Lyimo (Chadema) alisema kurudi bungeni kwa wabunge wa Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) waliosusa vikao vya Bunge kunategemea maamuzi ya umoja huo.
Baraza la Wazee wa Chadema lamuombea JPM afya njema
Written By CCMdijitali on Tuesday, July 19, 2016 | July 19, 2016
Labels:
KITAIFA