PM: Mji Mkuu Dodoma kuthibitishwa kisheria
Written By CCMdijitali on Wednesday, July 27, 2016 | July 27, 2016
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma - Habari leo
SERIKALI inatarajia kupeleka bungeni muswada wa kuitambua Dodoma kama makao makuu ya nchi ili uweze kuthibitishwa kisheria.
Muswada huo utawasilishwa katika bunge la Septemba mwaka huu.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hayo jana mjini hapa wakati akizungumza na viongozi wa serikali, Taasisi, Watendaji na wananchi wa mkoa wa Dodoma kuelezea azma ya serikali kuhamia Dodoma.
Pia alitoa siku 14 kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuwasilisha mapendekezo ya awali namna watakavyopendekeza mpango wa serikali kuhamia Dodoma. Waziri Mkuu alisema katika bunge lijalo muswada wa sheria ya serikali kuhamia Dodoma utapelekwa bungeni ili azma ya Rais John Magufuli na serikali yake uwe na nguvu kisheria.
Pia aliendelea kueleza: “Kazi inayofuata serikalini baada ya tamko la Rais Magufuli la serikali kuhamia Dodoma katika bunge lijalo ni kuwasilisha muswada wa sheria bungeni kabla ya kuanzishwa sheria, maamuzi kadhaa yamefanywa ikiwemo mikakati ya serikali ili kuimarisha uhamiaji huo,” alisema.
“Uamuzi wa kuhamia Dodoma na kuufanya mji huo kuwa makao makuu ya serikali imekuwa ni ndoto ya baba wa taifa na kudumu wakati wote wa awamu za serikali zilizofuata na hadi sasa serikali ya awamu ya tano utatekelezwa,” alisema.
Waziri Mkuu aliendelea kubainisha kwamba, “Rais John Magufuli na Makamu wa Rais pamoja na viongozi wengine wa chama wamesimamia ndoto ya baba wa taifa, na sasa inakwenda kutimia.
Alisema maagizo ya Rais ya Serikali kuhamia Dodoma ni halisi na hakuna namna nyingine kwani maagizo yametolewa na ni wajibu wa kila mmoja wetu kuyaamini na kuanza kuyatekeleza.
Aliendelea kusisitiza kwamba, “Mimi tayari niko Dodoma nina ofisi, nina nyumba na hata ile kauli yangu ya miezi miwili niliyotoa jana mbele ya Rais wakati wa sherehe za mashujaa, ililenga kwa watumishi wengine walio chini yangu kujipanga kuhamia Dodoma lakini, mimi tayari nipo na nitaendelea kufanya shughuli zangu nikiwa hapa Dodoma.
Alisema wageni wote watakaotaka kukutana na viongozi wakuu wa nchi, wakiwamo makatibu wakuu, mabalozi na watendaji wengine itawabidi kufika Dodoma.
Amesema, “wageni wote watakaomtaka Waziri Mkuu, pamoja na Makamu wa Rais waje watukute Dodoma na hayo ndio maagizo ya Rais Magufuli,” alisema. Alisema wizara zote zina nyumba, mawaziri na makatibu wakuu wana nyumba na ofisi hapa Dodoma kwa hiyo haitakuwa kazi ngumu kwao kuhamia Dodoma.
Waziri Mkuu alisema, Rais anapotoa maelekezo lazima yatimizwe ni utaratibu uliojengwa kwa watumishi wa umma.
Atoa siku 14
Alitoa siku 14 kwa serikali mkoa wa Dodoma kukaa na taasisi zake hususani Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuandaa na kutoa mpango kazi wake na kuuwasilisha kwa Waziri Mkuu ili aone watakavyotekeleza mpango huo kwa haraka na ufasaha.
“Ndani ya siku 14 nipate proposal ya kwanza namna mtakavyotekeleza naagiza kiundwe kikosi kazi chini yenu kitakachowajumuisha makundi yote.Baada ya siku 14 nipate mpango wenu,” alisema.
Mabalozi kujenga ofisi Dodoma
Alisema mabalozi wameonesha nia ya kujenga ofisi zao Dodoma na wanaendelea kuzungumza nao ili makao makuu ya serikali yawe ni kweli na kutambulika kote na wakitoka nje ya nchi watue kwanza Dodoma.
Maagizo kwa CDA
Alisema CDA itambue eneo la makazi ya serikali kuu kwa maana ya ofisi za wizara na taasisi zake, makazi ya watumishi na huduma za biashara, elimu na taratibu zote za kisheria za kulitwaa zinatumika kwa haraka tayari kwa matumizi.
Pia kuwepo kwa mfumo moja wa upatikanaji wa viwanja vya matumizi mbalimbali na ujulikane uwe wazi bila urasimu na uwekwe kwenye mfumo wa kompyuta na uuzaji wa viwanja uwe hivyo uwe wa kielektroniki kuepusha udanganyifu wa madalali.
“Sitaki kusikia viwanja vinapatikana katika mfumo usio rasmi mpaka wapitie kwa wakuu wa mikoa, wilaya, meya na kumfanya kila mtu anatoa kiwanja,” alisema.
Pia alishauri serikali na taasisi zake na hasa zisizo za kibiashara zielekezwe eneo jipya la makazi rasmi ya serikali na sio kuwapa viwanja Dodoma huko ni kurudia makosa ya Dar es Salaam kwa kuchanganya serikali na biashara na kusababisha foleni.
Waziri Mkuu aliitaka CDA na serikali ya mkoa kuhakikisha wanatenga maeneo maalumu kwa ajili ya bandari kavu, kituo kikuu cha biashara, eneo maalum la wajasiriamali kuendelea kuongeza eneo la viwanda na huduma mbalimbali za biashara mahoteli, mabenki elimu na afya pamoja na kuongeza kasi ya kupima viwanja kwa ajili ya makazi, viwanda na taasisi.
Aliwataka Tanroads kukarabati barabara zilizopo chini na kubuni ringroads kwa ajili ya kuepusha foleni sizizo za lazima na kuzitaka taasisi nyingine kuboresha huduma kama mamlaka ya majisafi na majitaka.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema atahakikisha anawasilisha mapendekezo ndani ya siku 10.
Labels:
KITAIFA