Home » » Siku za malori Dar zahesabika

Siku za malori Dar zahesabika

Written By CCMdijitali on Sunday, July 3, 2016 | July 03, 2016

Malori yakiwa kwenye foleni katika Barabara ya Mandela, Dar es Salaam hivi karibuni. (Picha ya Maktaba).

Habari Leo

UCHAMBUZI wa Rais John Magufuli kuhusu gharama za ujenzi wa reli ya kisasa, kuwa kilometa moja itagharimu kati ya dola za Marekani milioni 3.5 mpaka milioni nne, umedhihirisha namna siku za foleni za malori katika jiji la Dar es Salaam, zinavyohesabika.

Akizungumza juzi baada ya kumkaribisha mwenyeji wake, Rais wa Rwanda, Paul Kagame Ikulu Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema kama hakutakuwa na matatizo ya ufisadi na utoaji wa hongo wa asilimia kumi ili kupata mradi huo; kilometa moja ya reli hiyo ya kisasa itagharimu si zaidi ya dola hizo za Marekani milioni nne.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, tuta la reli inayotumika sasa ndilo litakalotumika kwa ajili ya reli hiyo ya kisasa, hivyo mkandarasi hatokuwa na kazi ya kujenga tuta jipya na jambo linalofanya gharama hizo kuwa hata chini ya dola za Marekani milioni 3.5 kwa kilometa moja.

Katika uchambuzi huo, Rais Magufuli alisema tayari serikali imetenga dola za Marekani milioni 460 sawa na Sh trilioni moja, ambazo kwa hesabu za haraka, fedha hizo zinatosha kujenga zaidi ya kilometa 115 za reli hiyo.

Kwa hesabu hizo, fedha hizo zilizopitishwa na Bunge, zitawezesha mkandarasi kujenga reli hiyo mpaka eneo la Ruvu mkoani Pwani, ambako ni kilometa 70 kutoka jijini Dar es Salaam na kufika mpaka hata Chalinze, ambako ni kilometa 109 kutoka Dar es Salaam.

Malori kuishia Ruvu

Hesabu hizo na kwa uchambuzi huo, Rais Magufuli atakuwa ametuma ujumbe mkali kwa wamiliki wa malori ya usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam, kwenda mikoani na katika nchi mbalimbali zinazopitishia mizigo yake katika bandari hiyo.

Ujumbe huo unatokana na dhamira yake aliyoitoa Aprili 16 mwaka huu, wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kwanza ya juu (Flyover) Tanzania, ambayo ujenzi wake ulishaanza katika makutano ya barabara za Mandela na Nyerere eneo la Tazara, kwa ufadhili wa Serikali ya Japan.

Katika hafla hiyo, Rais Magufuli alisema reli hiyo ya kisasa itakapofika Ruvu, kutajengwa bandari kavu kubwa katika eneo hilo ambayo ikikamilika, mizigo yote inayoshuka bandari ya Dar es Salaam, itasafirishwa kwa reli mpaka katika bandari hiyo.

Hatua hiyo ikifikiwa, ambayo kwa uchambuzi wake wa juzi, fedha zilizotengwa zinatosha kuifikia, Rais Magufuli alisema malori yote yanayochukua na kupeleka mizigo katika bandari hiyo, yataishia katika bandari kavu ya Ruvu na kupigwa marufuku kuonekana katika Jiji la Dar es Salaam.

Aidha alisema ili kuepuka wizi wa mizigo, kutafungwa kamera katika njia yote ya reli hiyo ya kisasa mpaka Ruvu, ili kontena linaloshushwa katika Bandari ya Dar es Salaam, lifuatiliwe mpaka katika bandari hiyo.

Barabara za pete

Katika uwekaji huo wa jiwe la msingi, Rais Magufuli alisema Mfuko wa Barabara utatoa fedha za kujenga barabara za pete, zitakazoongeza kasi ya kupunguza msongamano kama si kuumaliza.

Alionya kuwa fedha hizo za Mfuko wa Barabara hazitakiwi kutumika kulipana posho, bali kutengeneza barabara hizo za pete katika halmashauri na kuagiza makandarasi wanaotoa asilimia 10 kwa ajili ya rushwa, wasipewe zabuni bali watafute makandarasi wazuri.

Alisema kilometa 27 za barabara hizo za pete, zimeanza kujengwa na kwa kuwa wabunge wa Dar es Salaam waliopita walisema sana, waliongezewa kilometa nyingine 86 za barabara hizo za pete, zitakazojengwa kwa lami kwa fedha za mfuko huo.

Adhabu kali, msongamano

Katika kudhihirisha dhamira yake ya kuondoa malori hayo, Rais Magufuli aliagiza halmashauri za Dar es Salaam kuweka sheria itakayokataza kupitisha magari yenye tani zaidi ya 56 katika barabara hizo, yakiwemo malori ili barabara hizo zilizokusudiwa kutumika na magari madogo, zisiharibiwe na magari yenye uzito mkubwa.

Akizungumzia miradi hiyo ya kupunguza msongamano, ikiwemo barabara za juu ikiwemo ya Ubungo, Rais Magufuli alisema zitapunguza hasara iliyokuwa ikitokea kwani katika utafiti wa mwaka 2013, ulionesha kuwa Jiji la Dar es Salaam pekee katika mwaka huo lilipoteza Sh bilioni 411.3 katika msongamano wa magari.

Mbali na hasara hiyo iliyooneshwa katika utafiti, Rais Magufuli alisema inawezekana msongamano wa magari Dar es Salaam umesababisha baadhi ya watu kufa kwa kuchelewa kufikishwa hospitalini, baadhi ya ndoa kuvunjika kutokana na kuchelewa kufika nyumbani na kushindwa kujieleza.

Mabasi ya haraka

Akizungumzia hatua zingine za kupunguza msongamano katika jiji hilo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipokuwa akihitimisha Mkutano wa Tatu wa Bunge la 11 wiki hii, alitangaza kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa Awamu ya Pili na Tatu wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART).

Kwa mujibu wa Majaliwa, awamu hizo zitahusu barabara ya Mbagala na Gongo la Mboto, ili wananchi wa maeneo hayo waanze kufaidi huduma hizo za mabasi yaendayo haraka.

Alifafanua kuwa awamu hiyo ya tatu na nne, ni sehemu ya awamu sita za mradi huo utakaohusisha barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 130.3 katika jiji hilo.

Maeneo ya Dar es Salaam ambayo yameshaanza kunufaika na Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka ni pamoja na maeneo ya barabara kuu kutoka Kimara Mwisho hadi Kivukoni. Mengine ni yanayopakana na barabara ya Kawawa kuanzia Morocco hadi Magomeni Mapipa na Barabara ya Msimbazi, Kariakoo hadi Gerezani.

Miongoni mwa manufaa hayo ni pamoja na mabasi hayo kutumia muda mfupi usiozidi dakika 45 kwa safari ya kutoka Kivukoni hadi Kimara na kuwezesha abiria kuwahi kwenye shughuli zao za kila siku.

Kabla ya mradi huo kuanza, Waziri Mkuu Majaliwa alisema safari ya aina hiyo ilikuwa inatumia zaidi ya saa mbili. Manufaa mengine ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wanaoishi karibu na barabara ya DART, imebainika wameacha kutumia magari yao binafsi na kuanza kupanda mabasi hayo na kuokoa fedha nyingi za kununulia mafuta ya vyombo vyao vya usafiri.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link