Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati)
akizungumza wakati wa Kikao cha kujadili taarifa ya Kamati iliyoundwa na
Profesa Sospeter Muhongo mwezi Februari mwaka huu ili kutathmini
migogoro kati mgodi wa Acacia NorthMara na wananchi wanaozunguka
mgodi huo, kilichofanyika wilayani Tarime. Kushoto kwake ni Mkuu wa
wilaya ya Tarime, Glorious Luoga na wa Pili kushoto ni Mbunge wa Tarime
Vijijini, John Heche.
Baadhi ya wananchi wilayani Tarime, wakimsikiliza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) wakati wa Kikao cha kujadili taarifa ya Kamati iliyoundwa na Profesa Sospeter Muhongo mwezi Februari mwaka huu ili kutathmini migogoro kati mgodi wa Acacia NorthMara na wananchi wanaozunguka mgodi huo, kilichofanyika wilayani Tarime.
Wajumbe wa Kamati iliyoundwa na Profesa Sospeter Muhongo mwezi
Februari mwaka huu ili kutathmini migogoro kati mgodi wa Acacia
NorthMara na wananchi wanaozunguka mgodi huo, wakiwa katika kikao
cha kujadili taarifa ya Kamati hiyo, kilichofanyika wilayani Tarime.
Katibu wa Kamati iliyokuwa kutathmini migogoro kati ya Mgodi wa Acacia
NorthMara na wananchi wanaozunguka mgodi huo, Mhandisi John Shija
kutoka Wizara ya Nishati na Madini, akisoma taarifa ya Kamati hiyo mbele
ya wananchi na viongozi mbalimbali wilayani Tarime. Kushoto kwake ni
Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje na kulia kwake ni
Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Ziwa Victoria Magharibi, Mhandisi
Juma Sementa.
Na Teresia Mhagama
Wananchi mbalimbali wilayani Tarime wamekubali mapendekezo
yaliyotolewa na Kamati iliyoundwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo mwezi Februari mwaka huu ili kutathmini migogoro kati
mgodi wa Acacia NorthMara na wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Hayo yalibainika wakati wa Kikao kilichokuwa kikijadili taarifa ya Kamati
hiyo kilichofanyika wilayani Tarime, kikiongozwa na Waziri wa Nishati na
Madini na kuhudhuriwa na baadhi ya wananchi, Madiwani, Mbunge wa
Tarime Vijijini, Mkuu wa wilaya ya Tarime, Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Tarime Vijijini, watendaji wa Mgodi, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya
na Kamati iliyokuwa ikitathmini kero hizo.
Profesa Muhongo alisema kuwa Mapendekezo hayo ya Kamati
yalipatikana baada ya kuhoji wananchi 4,400 kutoka vitongoji 80 vya
Halmashauri husika huku hadidu za rejea zikiwa 16.
“Mapendekezo yote mliyoyatoa yamekubaliwa sasa kinachofuata ni nyinyi
Kamati kupita katika kila kitongoji na kuwaeleza wananchi kuhusu maamuzi
yaliyofikiwa mkizingatia pia baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa katika
kikao hiki na Wawakilishi wa wananchi kama Mbunge na Madiwani,”
alisema Profesa Muhongo.
Awali Katibu wa Kamati hiyo, Mhandisi John Shija kutoka Wizara ya Nishati
na Madini, alisema kuwa Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe 27 ambapo
wataalam wa Serikali walikuwa 19, wawakilishi wa mgodi 4 na wawakilishi
wa wananchi kupitia Ofisi ya Mbunge wa Tarime vijijini wakiwa 4.
Mhandisi Shija alisema kuwa Kamati ilipewa hadidu za rejea 16 ambapo
baadhi ya hadidu hizo zinahusu masuala ya fidia ya ardhi, athari za mgodi
kwa mazingira, binadamu na mifugo, uvamizi wa mgodi unaofanywa na
vijana, askari wanaolinda mgodi kunyanyasa wananchi na wachimbaji
wadogo kupatiwa maeneo ya kuchimba madini.
“Katika kuyachunguza masuala yaliyomo kwenye hadidu za rejea, Kamati
ilipitia taarifa mbalimbali na kuwahoji wananchi, pia ilikutana na viongozi wa
mgodi wa NorthMara, Wilaya, Watendaji wa Halmashauri, Kata, Vijiji na
kukagua shughuli za Mgodi na maeneo yanayozunguka Mgodi,”alisema
Mhandisi Shija.
kuhusu maeneo ambayo Mgodi uliwaambia wananchi wasiyaendeleze
huku maeneo hayo yakifyekwa wakati wa uthamini, Kamati ilipendekeza
kuwa Mgodi ulipe fidia ya mazao yaliyofyekwa na fidia ya usumbufu.
“ Kwa kuwa kwa mujibu wa sheria, fidia ya usumbufu ni asilimia 8 ya fidia
kuu (Fidia ya mazao), Kamati inapendekeza mgodi ulipe fidia hiyo kwa
kiwango cha asilimia 50 badala ya Nane,” alisema mmoja wa Wajumbe wa
Kamati hiyo.
Kuhusu wananchi ambao walikataa kufanyiwa uthamini katika maeneo ya
MjiniKati na Nyabichune wilayani Tarime, Kamati ilipendekeza kuwa mgodi
ufanye tathmini ndani ya wiki Tatu kwa mujibu wa hali ya mwaka 2012, na
wananchi hao wakiendelea kukataa, Serikali itawafanyia uthamini na
kuutaka Mgodi uwalipe kwa mujibu wa viwango vya serikali.
Aidha kuhusu suala la wananchi kujenga katika eneo la Mgodi kwa lengo la
kujipatia faida, Kamati ilipendekeza kuwa wananchi hao wasilipwe
chochote kwa kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria ambapo Kamati
iliasa Mamlaka husika kuendelea kusimamia sheria ili masuala hayo
yasiendelee kujitokeza.
Vilevile kuhusu madhara waliyopata wananchi kutokana na shughuli za
mgodi kama vile milipuko, vumbi, maji, na mifugo kufa kwa madai ya maji
yaliyochafuliwa kutokana na shughuli za mgodi, Kamati ilipendekeza kuwa
malalamiko yenye ushahidi yapelekwe mgodini ili yafanyiwe kazi ikiwa ni
pamoja na kulipwa fidia zao na ikishindikana yapelekwe kwa Kamishna wa
Madini.
Naye Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje alisema kuwa,
kuhusu suala la Wachimbaji wadogo wa madini kutengewa maeneo ya
uchimbaji, Wizara ya Nishati na Madini imebainisha eneo la ukubwa wa
kilometa za mraba 7.69 katika kijiji cha Kewanja wilayani Tarime ambalo
linaweza kutoa leseni ndogo za uchimbaji madini zipatazo 76.
“ Aidha kuna maeneo mengine yaliyotengwa kwa ajili ya wachimbaji
Wadogo kama eneo la Ilujamate wilayani Misungwi lenye ukubwa wa hekta
147, eneo la Nyangarata wilayani Kahama lenye hekta 1074 na eneo la
Ibogelo mkoani Tabora lenye hekta 6,527 hivyo tunashauri wachimbaji
wadogo wa madini wajitokeze katika kuomba maeneo hayo ya uchimbaji,”
alisema Mhandisi Samaje.
By MICHUZI BLOG