Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe Mrisho Mashaka Gambo na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa akizungumza na waandishi wa habari leo 31 August 2016.
Na Mwandishi Wetu - Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa amesema kesho hapatakua na maandamo yeyote katika Mkoa huu na kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida.
Mhe. Gambo ameyasema hayo mapema leo alipokua akizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kwamba Kamati ya Ulinzi na Usalama imejipanga kikamilifu kuhakikisha amani ya Mkoa huu inaendelea kuwepo na kudhibiti viashiria vyote vya uvunjifu wa amani vitakavyojitokeza.
Amewatoa hofu wananchi na kuwataka kuendelea na shughuli zao kama kawaida pia amewahakikishia amani na utulivu na kuwataka kuendelea kumuunga Mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujituma na kufanya kazi kwa maendeleo ya Nchi yetu.
Pia ameelezea dhana ya wanajeshi wa JWTZ kuadhimisha miaka 52 ya Jeshi kwa kufanya usafi siku ya kesho kwamba ni utaratibu wa kawaida na wanaunga mkono agizo la Rais wetu la kuwataka watu wote kufanya usafi katika maeneo yao ili kujikinga na maradhi.