Home » » Ntibenda atoa mpya akikabidhi ofisi

Ntibenda atoa mpya akikabidhi ofisi

Written By CCMdijitali on Tuesday, August 23, 2016 | August 23, 2016

 

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Daudi Felix Ntibenda, akimkabidhi rasmi hati ya makabidhiyano ya ofisi kwa Mkuu wa Mkoa mpya wa Arusha Mrisho Mashaka Gambo,makabidhiyano hayo yalifanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa,Agosti 20,2016.
John Ngunge | Nipashe

ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda, ametoa mpya baada ya kukabidhi ofisi kwa Mkuu wa Mkoa mpya, Mrisho Gambo, kwa staili ya aina yake.

Ni kawaida kwa waandishi wa habari na wapiga picha kuhudhuria makabidhiano ya ofisi kwa viongozi mbalimbali wapya na wale wanaoondoka, lakini kwa Ntibenda jana haikuwa hivyo.

Licha ya shauku ya waandishi mbalimbali wa habari kutaka kushuhudia tukio hilo, waliishia nje ya ofisi hiyo ya Mkuu wa Mkoa baada ya kuambiwa kuwa shughuli hiyo haiwahusu.

Kitu kingine cha kushangaza kwenye makabidhiano hayo ni muda mfupi sana uliotumiwa na Ntibenda kukabidhi ofisi hiyo, tofauti na muda ambao umekuwa ukitumiwa kwenye shughuli za aina hiyo.

Ntibenda alikabidhi ofisi hiyo 'chap chap' jana asubuhi na kuondoka, huku akiwaambia waandishi wa habari kuwa wanakaribishwa nyumbani kwake mkoani Kigoma.

Ilikuwa majira ya saa 2:00 asubuhi jana, Ntibenda ambaye hakuonekana kuwa katika hali ya uchangamfu, alitinga maeneo ya mkoa na baada ya kuingia alikwenda kwenye ofisi yake ya zamani akiwa ameongozana na mrithi wake, Gambo.

Baada ya kukabidhiwa ofisi, Gambo alianza kazi kwa kukutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na pamoja na mambo mengine, walijadili kuhusu Mwenge wa Uhuru unaowasili wilayani Ngorongoro ukitokea mkoani Mara.

Baada ya kikao hicho, Gambo alitoa taarifa ya ujio wa Mwenge wa Uhuru huku akionya watu watakaoubeza au kutishia amani ya kuupokea.

Alisema mwenge ni kielelezo cha Uhuru wa Tanzania, hivyo si vizuri kuubeza au kutishia amani ya mapokezi yake.

Aliwaomba wananchi kujitokeza kwa mwingi maeneo yote mwenge huo utakakokimbizwa katika wilaya zake saba.


Gambo alisema moja ya kazi kubwa ambayo itafanywa na Mwenge wa Uhuru ukiwa mkoani hapa ni kutembelea, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi 57 yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 12.9.

Alisema miradi hiyo inatekelezwa kwa kushirikisha nguvu za wananchi, fedha toka serikali kuu, halmashauri, wahisani na taasisi mbalimbali zilizopo mkoani hapa.


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link