Home » » RELI YA KISASA NCHINI KUANZA KUJENGWA MWEZI DESEMBA

RELI YA KISASA NCHINI KUANZA KUJENGWA MWEZI DESEMBA

Written By CCMdijitali on Sunday, August 14, 2016 | August 14, 2016

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema ujenzi wa reli
ya kisasa (standard gauge) unatarajiwa kuanza mwezi Desemba mwaka huu na kama ilivyo
miradi mikubwa unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu na utajengwa kwa awamu nne ili
kuharakisha kukamilika kwake.

Waziri Prof. Mbarawa amesema Prof. Mbarawa ametoa kauli hiyo leo, wakati wa Mkutano wa
Sita uliowakutanisha  Mawaziri wa Sekta ya Uchukuzi wa nchi za Tanzania, Rwanda na
Burundi, uliofanyika jijini Dar es Salaam ambapo amesema lengo la mkutano huo ni kuangalia
namna bora ya kupunguza vikwazo kwenye sekta hiyo baina ya nchi hizo.

Amesema kuwa ushirikiano baina ya nchi za Afrika Mashariki katika ujenzi wa reli hiyo
utachochea kasi ya usafirishaji wa mizigo na shughuli za kibiashara na hivyo kuinua uchumi wa
nchi hizo.

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati), akizungumza na viongozi mbalimbali wa sekta ya uchukuzi (hawapo pichani), katika Mkutano wa Sita wa Kamati ya Mawaziri wa nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi uliofanyika jijini Dar es salaam. 
Kulia ni Waziri wa Uchukuzi wa Burundi Eng. Jeon Ntunzwenidana na kushoto ni Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi ya Tanzania Dkt. Leonard Chamuriho.

“Kama mnavyojua Serikali imetenga kiasi cha shilingi Trilioni moja kwa ajili ya kuanza
kutekeleza mradi huo na wenzetu nao watatafuta fedha katika nchi zao ili kukamilisha ujenzi
wake”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.


Aidha Prof. Mbarawa amebainisha kuwa kila nchi itatekeleza mradi wa kujenga reli ya kisasa
kwa sehemu yake hivyo ni wajibu wa kila nchi kukamilisha mradi huo ili kuchochea maendeleo
yanayotokana na Sekta ya Uchukuzi.


Amesema kwa upande wa nchi ya Tanzania reli hiyo itaanza kujengwa kuanzia Dar es Salaam-
Tabora-Isaka hadi Mwanza yenye urefu wa KM 1,219 ambayo ndiyo uti wa mgongo wa reli
yenyewe. Sehemu nyingine ni kutoka Tabora-Mpanda- Kalemela; Tabora-Uvinza hadi Kigoma.


Katika kuunganishwa na nchi ya Rwanda na Burundi, Waziri Mbarawa amesema ujenzi wa reli
hiyo itajengwa kuanzia Isaka-Rusumo mpaka Kigali na Keza mpaka Musongati.



 Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho akifafanua jambo kwa viongozi mbalimbali wa sekta ya uchukuzi (hawapo pichani), katika Mkutano wa Sita wa Kamati ya Mawaziri wa nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi uliofanyika jijini Dar es salaam. Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa.

Naye Waziri wa Uchukuzi wa nchi ya Burundi Eng. Jeon Ntunzwenidana amefurahishwa na
Serikali ya Tanzania katika jitihada zake za kuharakisha ujenzi wa reli hiyo na amesema Serikali
ya Burundi itakamilisha ujenzi huo haraka ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na huduma za
kibiashara baina ya nchi hizo.


Waziri Prof. Mbarawa amesaini makubaliano ya uboreshwaji wa sekta ya mawasiliano, reli na
barabara baina ya nchi za Tanzania, Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Demokrasia ya
Congo (DRC).


Zaidi ya trilioni 16 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa reli ya kisasa nchini Tanzania yenye
takribani urefu wa KM 2,600.


 Viongozi wa Sekta ya Uchukuzi wakijadiliana kuhusu changamoto mbalimbali za sekta
hiyo katika Mkutano wa Sita wa Kamati ya Mawaziri wa nchi za Tanzania, Rwanda na
Burundi uliofanyika jijini Dar es salaam.


 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya Mkutano wa Sita wa Kamati ya Mawaziri wa
nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi uliofanyika jijini Dar es salaam.



Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia)
pamoja na mawaziri kutoka nchi shiriki wakisaini makubaliano ya uboreshwaji wa sekta
ya mawasiliano, reli na barabara baina ya nchi za Tanzania, Rwanda, Burundi, Uganda
na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).

Habari na Michuzi Blog
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link