Home » » Serikali yakiri adha ya kuhamisha wafugaji

Serikali yakiri adha ya kuhamisha wafugaji

Written By CCMdijitali on Sunday, August 14, 2016 | August 14, 2016

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha

    Imeandikwa na Francisca Emmanuel, Rufiji | Habari Leo

SERIKALI imekiri kuwa utaratibu wa kuwahamisha wafugaji kutoka mkoani Mbeya kwenda Rufiji mkoani Pwani mwaka 2006, umeleta changamoto kwa kuwa hakukuwa na maeneo rasmi kwa ajili ya wafugaji hao.

Hivyo, imesema inaandaa utaratibu wa kugawa maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji ili kupunguza migogoro ambayo inasababisha uharibifu wa mali na watu.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha alipokuwa akizungumza na wakulima na wafugaji ambao walikuwa na mgogoro uliosababisha kukatwa mapanga ng’ombe 15 katika kijiji cha Mtunda A wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.

Ole Nasha alisema licha ya kuwepo kwa changamoto hiyo, wafugaji watakaogawiwa maeneo kwa ajili ya ufugaji hawatakiwi kuyaacha na kuingilia mashamba ya wakulima kwani ndio chanzo cha migogoro.

“Ni kweli mwaka 2006 wafugaji walitolewa Mbeya na kuambiwa kuwa eneo linalofaa kwa ajili ya ufugaji ni Rufiji. Walipofika huku hakukuwa na maeneo yaliyotengwa kwa ajili yao, lakini Serikali itaandaa utaratibu mpya kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji kupunguza migogoro hiyo,’’ alisema.

Pia alisema viongozi wa Serikali za Mitaa wamekuwa wakichangia kuongezeka kwa migogoro hiyo, kwamba wanapokea rushwa kutoka kwa wafugaji na kuwaruhusu wafugaji wengi kuingia kinyume cha taratibu, hivyo kuagiza Halmashauri kuhakikisha hakuna uingizaji wa watu na mifugo kinyume na sheria kwani wenye ruhusa ya kuwakubali watu kuingia kijijini ni wanakijiji wenyewe.

“Kwa miaka 10 sasa, wafugaji wamekuwa wakiingia katika eneo hili la Mtunda bila ya kufuata taratibu na sheria. Walioruhusiwa awali ni wafugaji sita lakini sasa wapo zaidi ya 600 hii inaonesha kuwa viongozi wa serikali za mitaa hawatambui wajibu wao na kwamba wanakijiji wana uwezo wa kuwakataa hawa wengine,’’ alisisitiza.

Aidha, aliwataka wafugaji hao kutokubali kuingia kwa maeneo ya watu kinyume na taratibu na kukemea watu kujichukulia sheria mikononi bali kufikisha malalamiko yao kwenye vyombo vya dola ili watakaokutwa na hatia wapelekwe jela.


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link