Home » » Serikali yaanza kuuza tanzanite kwa mnada

Serikali yaanza kuuza tanzanite kwa mnada

Written By CCMdijitali on Monday, August 15, 2016 | August 15, 2016

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe

    Imeandikwa na Veronica Mheta, Arusha - Habari Leo

SERIKALI imeanzisha utaratibu wa kuuza madini aina ya tanzanite kwa mnada ili kudhibiti wizi na utoroshaji wa madini hayo na kuongeza pato la taifa.

Utaratibu huo wa mnada ulitangazwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe, wakati wa mnada wa kwanza wa madini hayo uliofanyika kwenye ofisi za madini Kanda ya Kaskazini mkoani hapa.

Kwa mujibu wa Mdoe, mnada wa tanzanite utadhibiti kwa kiasi kikubwa utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi kwani wafanyabiashara wakubwa watapata fursa ya kuacha kununua madini hayo kwa njia za panya.

Katika mnada huo, wanunuzi wakubwa wa tanzanite 37 walishiriki na kampuni tano zilishiriki katika mnada huo kati ya 180 zinazochimba madini hayo katika eneo la Mirerani. Mdoe alitaja wachimbaji walioshiriki katika mnada huo ni Tanzanite One/Stamico, Tanzanite Afrika/ J. S Magezi, Chusa, Kulian Laizer and Partiners na Franone Mininga and Gems.

Katika mnada huo uliofana, Kampuni ya TanzaniteOne ilifanikiwa kuuza gramu 293,173.17 na kupata Sh bilioni 7.3 ambapo serikali ilipata mrabaha wa Sh milioni 367.4.

Kampuni ya Franone iliuza gramu 24,860 ambapo ilipata zaidi ya Sh milioni 235 wakati kampuni ya Chusa, Laizer and Friends na Tanzanite Africa ziliondoa madini yake katika mnada huo kutokana na wanunuzi kutofikia bei waliyokuwa wanahitaji.

Mdoe alisema mnada huo utawezesha wachimbaji wadogo kukutana na wafanyabiashara wa kimataifa na kuongeza bei ya tanzanite ambayo imeshuka kutokana na utoroshaji wa madini ambayo yanauzwa na wezi hao kwa bei ya kutupa.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera aliwahakikishia wachimbaji usalama na kuwataka kufanya kazi zao za uchimbaji bila wasiwasi. Aidha aliwataka wachimbaji hao kujitokeza kwa wingi katika minada itakayoendelea ili kukutana na wafanyabiashara wakubwa wa tanzanite kutoka ndani na nje ya nchi.


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link