Watanzania kufunzwa usindikaji gesi Japan
Written By CCMdijitali on Friday, August 26, 2016 | August 26, 2016
Imeandikwa na Mwandishi Maalumu, Nairobi | Habari Leo
KAMPUNI ya Japan imeahidi kutoa mafunzo kwa Watanzania ya kuwajengea uwezo katika sekta ya gesi, hususan usindikaji wa gesi kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi (LNG).
Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo ya Chiyoda Corporation, Tadashi Izawa alisema hayo jijini Nairobi, Kenya jana, alipokutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu anamwakilisha Rais John Magufuli kwenye Mkutano Mkuu wa Sita wa Kimataifa kuhusu Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Japan na Afrika (TICAD). Mkutano huo utakaofanyika Nairobi kwa siku mbili, unaanza leo.
Jana, Majaliwa alikutana na kuzungumza na viongozi wakuu mbalimbali wa kampuni za kibiashara za Japan waliopo Nairobi, akiwemo kiongozi huyo wa Kampuni ya Chiyoda. Katika mazungumzo yake na Majaliwa, Izawa alisema kampuni yao ya Chiyoda, itaangalia fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya gesi Tanzania.
Pia, alisema kampuni yao itatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu katika sekta ya gesi, hususan usindikaji wa gesi kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi (LNG).
“Tunao uzoefu wa muda mrefu, pia tunazo teknolojia za kuendeleza sekta ya gesi ikiwemo helium kwa mfano ujuzi wa kutenganisha gesi asilia na helium. Tumetekeleza miradi ya namna hii Qatar ambayo kwa sasa ni ya pili kwa uzalishaji wa gesi hiyo duniani ikitanguliwa na Marekani,” alisema Izawa.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo, yatafanyika mwakani na yatalenga vijana wasiopungua 10 kutoka Tanzania, waliohitimu shahada za uhandisi. Pia Waziri Mkuu alikutana na Makamu wa Rais wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Japan (JICA), Hiroshi Kato na kujadiliana mambo kadhaa yakiwemo ya nishati na miundombinu.
Kato alisema nia ya shirika hilo ni kuendelea kusaidia miradi mbalimbali nchini Tanzania na hasa katika sekta za afya, maji, kilimo na miundombinu, ambalo limekuwa likijihusisha nazo kwa muda mrefu sasa.
Labels:
BIASHARA