Balozi Seif akimkabidhi Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma Madawati 50 akikamilisha madawati 100 aliyoahidi kwa skuli ya Msingi Mahonda yaliyogharimu shilingi Milioni 16,000,000/-.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma akipokea msaada wa mashine moja ya Fotokopi na Kompyuta Mbili kutoka kwa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi alizoahidi kuipatia skuli ya Msingi Mahonda.
Kulia ya Waziri wa Elimu Mh. Riziki ni Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi Mahonda Bibi Kazija Moha;d Makame na wa kwanza kutoka kushoto ni Mke wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Mama Asha Suleiman Iddi.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi ametoa wito kwa Watu wenye uwezo ndani na nje ya Nchini kuelewa kwamba bado wana wajibu wa kuendelea kuchangia upatikanaji wa Madeski ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuijengea mazingira bora ya miundo mbinu sekta ya Elimu Nchini.Alisema upatikanaji wa madeski utakaokidhi mahitaji halisi katika skuli mbali mbali za msingi na sekondari utatoa fursa nzuri kwa wanafunzi kuendelea kusoma kwa utulivu na umakini zaidi.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito huo wakati akikabidhi Jengo la Madarasa Manne la Skuli ya Msingi ya Mahonda baada ya kulifanyia matengenezo makubwa yaliyogharimu Shilingi Milioni 20,000,000/-.
Katika hafla hiyo Balozi Seif pia alikabidhi madeski 50 kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma kukamilisha ahadi aliyotoa ya madeski 100 kwa Skuli ya Msingi ya Mahonda yaliyogharimu jumla ya shilingi Milioni 16,000,000/-.
Sambamba na hayo Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda akakabidhi Mashine Moja ya Fotokopi na Kompyuta Mbili kwa Skuli hiyo zenye gharama ya shilingi Milioni 4,700,000/-.
Alisema jamii inapaswa kuona umuhimu wa Elimu kwa kuongeza nguvu za kuimarisha Sekta hiyo ili kujenga Taifa lililo bora litakaloweza kukidhi mahitaji halisi ya mabadiliko ya teknolojia ya kisasa ya mawasiliano inayokwenda kwa kasi Duniani.
Balozi Seif alifafanua kwamba wataalamu wa sekta zote wa kijamii, kiuchumi na maendeleo watapatikana na kutosheleza katika Tasisi za umma na hata binafsi iwapo huduma za kielimu zitaimarika katika miundombinu yake.
Akipokea msaada huo mkubwa wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma alimpongeza Balozi Seif kwa moyo wake wa uzalendo wa kutekeleza ahadi anazokuwa akitoa.
Waziri Riziki alisema uungwana wa Balozi Seif katika kuchangia maendeleo umemuepusha katika kundi la watu wanaoahidi na kushindwa kutekeleza ahadi zao kitu ambacho ni dhambi katika maandiko na maamrisho ya Dini.
Mheshimiwa Riziki Pembe Juma aliwaomba Viongozi wa Kamati ya Skuli, Waalimu na Wanafunzi kuhakikisha kwamba msaada uliotolewa wa madeski, Kompyuta na Jengo lao wanavitunza kwa lengo la kuendelea kutoa huduma kwa kipindi kirefu kijacho.
Mapema Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi ya Mahonda Bibi Kazija Moh’d Makame alisema kitendo cha Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif cha kuahidi na kutekeleza ahadi katika kipindi kifupi kimeleta faraja kwa wadau wa skuli hiyo.
Mwalimu Kazija alisema jengo la madarasa Manne la Skuli ya Msingi Mahonda lilikuwa Binti Marehemu kiasi kwamba lilileta usumbufu kwa Wanafunzi waliokuwa wakilitumia katika kipindi kirefu kilichopita.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
19/9/2016.