Home » » Bei ya mafuta nchini yashuka

Bei ya mafuta nchini yashuka

Written By CCMdijitali on Wednesday, September 7, 2016 | September 07, 2016

    Imeandikwa na Mwandishi Wetu | Habari Leo

 Mkurugenzi Mkuu, Felix Ngamlagosi
BEI za jumla na za rejareja za mafuta katika mikoa yote nchini, isipokuwa mkoa wa Tanga, imeshuka ukilinganisha na bei za mwezi uliopita, taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (Ewura) imeeleza.

Taarifa ya Ewura iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu, Felix Ngamlagosi inaeleza kuwa bei za rejareja kwa petroli imepungua kwa Sh 65 sawa na asilimia 3.50, dizeli Sh 63 sawa na asilimia 3.43 na mafuta ya taa bei imepungua kwa Sh 86 sawa na asilimia 4.88.

Taarifa hiyo ya Ewura ilisema kwamba bei za jumla, zimepungua pia na mwezi huu petroli itauzwa kwa Sh 65.31 kwa lita sawa na asilimia 3.63, dizeli Sh 63.39 sawa na asilimia 3.72, na mafuta ya taa Sh 85.93 sawa na asilimia 5.20.

“Kushuka kwa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia na kupungua kwa gharama za usafarishaji wa bidhaa za mafuta hayo kuja nchini, ndizo sababu kuu zilizochangia kushuka kwa bei za mafuta katika soko la ndani hapa nchini,” alisema Ngamlagosi.

Bei mpya za rejareja ambazo zitaanza kuuzwa leo katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa petroli itakuwa ni Sh 1,840, dizeli Sh 1,747 na mafuta ya taa Sh 1,673.

Bei za jumla katika Mkoa wa Dar es Salaam petroli itauzwa Sh 1,731.51, dizeli Sh 1,639.29 na mafuta ya taa Sh 1,565.43 kwa lita.

Katika mji wa Arusha, petroli itauzwa kwa Sh 1,923, dizeli Sh 1,831 na mafuta ya taa Sh 1,757 wakati katika mji wa Mwanza petroli itauzwa kwa Sh 1,989, dizeli Sh 1,897 na mafuta ya taa Sh 1,823.

Mkoani Kigoma katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, petroli itauzwa kwa Sh 2,070, dizeli Sh 1,978 na mafuta ya taa Sh 1,904 wakati mkoani Kagera katika manispaa ya Bukoba petroli itauzwa kwa 2,054, dizeli Sh 1,962 na mafuta ya taa Sh1,888.

Kuhusu bei kwa Mkoa wa Tanga, taarifa hiyo ilieleza kuwa bei za jumla na za rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli katika mkoa huo zimeongezeka kidogo, ikilinganishwa na toleo la bei za mafuta hayo lililopita ukilinganisha na mwezi uliopita.

Kwa mwezi huu, bei za rejareja kwa petroli imeongezeka kwa Sh 50 kwa lita sawa na asilimia 2.64 na dizeli Sh 19 sawa na asilimia 1.03. Bei katika manispaa ya Tanga, petroli itauzwa kwa Sh 1,932, dizeli Sh 1,822 na mafuta ya taa Sh 1,753. Bei za jumla mkoani humo kwa petroli itauzwa kwa Sh 1,823.63 kwa lita, dizeli Sh 1,714.15 na mafuta ya taa Sh 1,644.59.

Ngamlagosi alisema kwa kulinganisha mwezi uliopita na bei za mwezi huu, bei za jumla zimeongezeka kwa petroli Sh 49.61 kwa lita sawa na asilimia 2.80 na dizeli Sh 18.57 sawa na asilimia 1.1.

“Ongezeko hili la bei limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kupokea mafuta mapya ya petroli na dizeli ndani ya mwezi wa Agosti 2016, ambayo yalitarajiwa kupokewa mwezi wa Julai 2016 na pia kutokupokea mafuta mapya ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kutoka meli ya MT.NEVASKA LADY ndani ya mwezi wa Agosti,” alisema Ngamlagosi.

Mkurugenzi mkuu huyo wa Ewura alisema kampuni za mafuta, zipo huru kuuza bidhaa za petroli kwa bei ya ushindani, mradi tu bei hizo ziwe chini ya bei kikomo, kama ilivyokokotolewa na fomula iliyopitishwa na Ewura na ambayo ilichapishwa katika gazeti la Serikali la mwezi Februari mwaka huu.

Ngalamgosi alisema wanunuzi wahakikishe wanapatiwa stakabadhi ya malipo, inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.

Alisema stakabadhi hiyo ya malipo, itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta, endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yenye kiwango cha ubora kisichofaa.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link