Home » » Gavana: Pato la taifa limeongezeka

Gavana: Pato la taifa limeongezeka

Written By CCMdijitali on Friday, September 30, 2016 | September 30, 2016

Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu

Imeandikwa na Sophia Mwambe | Habari Leo

UKUAJI wa pato la taifa katika nusu ya kwanza ya mwaka ya Januari mpaka Juni, umeongezeka na kufikia asilimia 6.7 kutoka asilimia 5.7 kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2015.

Hayo yamesemwa Dar es Salaam na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ukuaji wa pato la taifa kwa robo na nusu mwaka 2016.

Alisema shughuli zilizochangia ukuaji huo wa uchumi kwa kiasi kikubwa kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2016 ni uchukuzi na uhifadhi wa mizigo asilimia 16.0, ujenzi asilimia 10.7, na kilimo asilimia 10.3.

”Kilimo kimepiga hatua kubwa kwa nusu ya kwanza ya mwaka huu, ambapo kimekua kwa asilimia 10.3 wakati kilishuka kwa asilimia 8.4 kwa nusu ya kwanza ya mwaka jana,” alisema Ndulu.

Aliongeza kuwa sekta zilizoonekana kukua zaidi katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016 ni uchukuzi na uhifadhi wa mizigo ambao umekuwa kwa asilimia 17.4, uchimbaji wa madini na gesi umekuwa kwa asilimia 13.7, mawasiliano umekuwa kwa asilimia 13.0 na sekta ya fedha na bima ambayo imekuwa kwa asilimia 13.0.

“Sisi tunaamini kwa kuangalia hali ya ukuaji wa pato la Taifa kwa nusu ya kwanza ya mwaka pamoja na viashiria ya uchumi mpaka sasa, ni mategemeo yetu kwamba lengo la ukuaji wa pato la taifa kwa asilimia 7.2 kwa mwaka 2016 litafikiwa,” aliongeza.

Akizungumzia mauzo ya nje, alisema utalii unachangia kuongezeka kwa pato la taifa. Alisema idadi ya watalii imeongezeka kutoka watalii 1,075,541 na kufikia milioni 1.1 mwaka huu ambayo imechangia pato kuongezeka kwa asilimia 5.8.

Aliongeza kuwa usafirishaji wa mizigo nje ya nchi umeongezeka, ambapo Uganda umeongezeka kwa asilimia 22.3, Rwanda 7.5, Malawi 14, Burundi 5.8 na Zambia 3.7 huku Kongo ikionekana kushuka kutokana na kushuka kwa thamani ya fedha ya Afrika Kusini.

Ndulu alisema uuzwaji wa bidhaa za viwandani nje ya nchi, umeendelea kukua kwa kasi na mauzo yameongezeka kwa asilimia 12.6, jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa fedha za kigeni.

Akizungumzia ukuaji wa pato la taifa katika robo ya pili ya mwaka, alisema kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), hali ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania imeendelea kuwa ya kuridhisha.

Katika robo ya pili ya mwaka 2016, ukuaji wa Pato la Taifa unakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 7.9 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 5.8kwa kipindi kama hicho mwaka 2015.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link