Home » , » Mamilioni posho za madiwani kulipa walimu

Mamilioni posho za madiwani kulipa walimu

Written By CCMdijitali on Tuesday, September 20, 2016 | September 20, 2016


 MKUU wa mkoa Arusha Mhe. Mrisho Gambo akiongea na walimu wote wa shule za msingi 48 zilizopo ndani ya Halmashauri ya jiji la Arusha, waratibu elimu, wakaguzi elimu pamoja na maafisa elimu kata

 Mkuu wa wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Daqarro akiongea na walimu walioudhuria mkutano huo.

Imeandikwa na Veronica Mheta, Arusha | Habari Leo

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameamuru posho walizokuwa wakilipwa madiwani wa Jiji la Arusha, zinazofikia zaidi ya mamilioni ya fedha kwa ajili ya vikao, nauli, mafuta na vocha za simu, kubadilishwa matumizi na kulipa madeni ya walimu wanaodai zaidi ya Sh milioni 154.

Amesema kila mwalimu anastahili kusimamia mitihani na kupata posho na si baadhi ya walimu kusimamia mitihani hiyo mara kwa mara kama vile hakuna wengine.

Uamuzi huo wa Gambo aliutoa jana wakati alipozungumza na walimu wa shule za msingi na sekondari, walimu wakuu, waratibu wa elimu kata pamoja na wakuu wa vitengo mbalimbali za utumishi wa umma akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqqaro na Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia.

Gambo amesema fedha hizo zilizobadilishwa matumizi yake, zinatoka kwenye posho walizokuwa wakilipana madiwani hao kwenye sikukuu, ambazo Mkurugenzi wa Jiji aliyekuwepo kabla ya wa sasa na Meya walikuwa wakilipana Sh milioni moja kila sikukuu, Sh milioni 61.2 za simu, nauli Sh milioni 28 na gharama za mafuta ambazo wamekuwa walipwa madiwani hao kulingana na umbali, ikiwemo posho ya dereva anayetoka nje ya mkoa Sh 100,000 kwa siku na kulipwa kadri ya siku atakazokaa.

Amesema fedha hizo ni nyingi na hivi sasa zimesitishwa matumizi yake, badala yake madiwani hao watalipwa Sh 10,000 kama nauli kwa ajili ya kuja kwenye vikao vya Baraza la Madiwani na posho zao za vikao, ambazo pia zimepunguzwa.

Amesema haiwezekani walimu wadai zaidi ya Sh milioni 154 ambazo jiji linaweza kuwalipa kulingana na vyanzo vya mapato vya ndani, badala yake madiwani ndio wanufaike na fedha hizo huku kila sikukuu wakijilipa posho kubwa na watumishi wengine wakishindwa kutatuliwa kero zao na kuzungushwa tu.

“Haiwezekani walimu wawe wanaidai serikali zaidi ya shilingi milioni 154 wakashindwa kulipwa huku wakifanya kazi kwenye mazingira magumu halafu wengine wanakula raha…sasa nasema walimu walipwe fedha hizi ndani ya wiki mbili na fedha hizi walikuwa wakilipwa madiwani sasa nasema walimu walipwe madeni yao ikiwemo malimbikizo ya nauli na fedha za kupandishwa madaraja,” amesema Gambo.

Amewaagiza mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa jiji kuhakikisha wanakwenda kuangalia shule za sekondari na msingi na kuzikagua ili kujionea hali halisi sambamba na kuwaagiza wakuu wa shule mbalimbali za msingi na sekondari kuanisha ni nyumba ngapi zinahitajika kwaajili ya ujenzi wa nyumba za walimu.

Amewataka wakuu wa shule za sekondari na msingi kutoa nafasi kwa walimu wengine kusimamia mitihani na fursa nyingine zinazojitokeza badala ya kufanya upendeleo kwa baadhi ya walimu ikiwemo kupandishwa madaraja walimu wasiostahili kunakotokana na kujipendekeza kwa wakuu wa shule au kutoa rushwa ya ngono kupata fursa hizo.








 Kushoto ni mkurugenzi wa jiji la ArushaAthumani Kihamia akiwa anasikiliza kwa makini malalamiko ya walimu hao




 picha ya juu na chini ni walimu waliouthuria mkutano huo wa mkuu wa mkoa  uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa AICC uliopo mkoani Arusha 



Video :


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link