Home » » Ugunduzi wa Mtanzania kutumika maabara

Ugunduzi wa Mtanzania kutumika maabara

Written By CCMdijitali on Sunday, September 18, 2016 | September 18, 2016

   Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma | Habari Leo

SERIKALI itaanza kutumia kwenye maabara za shule kifaa kipya cha sayansi maalumu ambacho mvumbuzi wake ni Mtanzania, Ernest Maranya (36).

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo wakati Maranya akitambulisha kifaa hicho mbele ya jopo la wataalamu kutoka Tamisemi.

Maranya, ambaye ni mlemavu wa kusikia, alisema uvumbuzi huo umehakikiwa na kuthibitishwa na japo la wataalamu kutoka vyuo vikuu na taasisi za utafiti kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi chini ya uratibu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na kusajiliwa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa hati namba TZ/P/14/00372.

“Kifaa kimelenga kuwa nyenzo ya majaribio ya awali ya kisayansi kikilenga Idara za Utafiti wa Mambo ya Anga kuwa na kifaa kinachoweza kuhakiki mienendo, tabia, matokeo na mahesabu ya utendaji wa vitu vyote vya anga kama vimondo, sayari, mwezi, nyota, sumaku za asili na zisizo asilia na tabia za nishati ya mvutano ya anga," alisema.

Jafo alisema ugunduzi huo ulifanywa kwa mara ya kwanza na mwanasayansi wa kale, Isaac Newton lakini wa Maranya umeonesha kuibua vitu vingi zaidi na akawataka wananchi kuthamini ugunduzi wa wenzao.

Aliwaagiza wataalamu wa wizara yake na wale wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha kifaa hicho kinaanza kutumika shuleni pamoja na kumpatia mhusika hati miliki. Alisema wanaweza kufunga kifaa hicho kwenye shule kongwe huku akiwataka wataalamu wa Wizara hiyo ya Elimu na Tamisemi, wahangaikie suala hilo kwani ugunduzi huo unaweza kuchukuliwa na wazungu na kuubadilisha na kusema wamegundua wao.

“Angalau tuanze na shule 20 ili wanafunzi wafanye masomo kwa vitendo, jambo hili ni kubwa na ni vitu adimu vya kisayansi, ni wajibu wa wataalamu ndani ya miaka mitano kuhakikisha kitu kikubwa kinafanyika kutokana na ugunduzi huu,” alisema.

Mkuu wa Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi (Veta), Kanda ya Kati, Ramadhani Mataka, alisema Tanzania ina vipaji vingi lakini haviendelezwi kutokana na mfumo wa elimu uliopo nchini.

Dk Jane Namseda ambaye ni mtaalamu wa lugha, Ofisi ya Rais Tamisemi, alisema mgunduzi huyo amekuja na kitu kizuri hajakipika wala hajaota ndoto na kwamba utafiti moja unafuatia utafiti mwingine. Mtaalamu wa Idara ya Elimu kutoka Tamisemi, Benjamin Oganga, alisema kupingana katika utafiti si dhambi na ndicho kitu kinachotakiwa kufanyika.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link