Home » » Ujenzi daraja la Salender kuanza Juni Mwakani - Rais Magufuli

Ujenzi daraja la Salender kuanza Juni Mwakani - Rais Magufuli

Written By CCMdijitali on Thursday, September 22, 2016 | September 22, 2016

Rais Dkt John Magufuli akimshukuru Balozi wa Jamhuri ya Korea hapa nchini Song Geum-Young mara baada ya kupokea picha ya mfano wa Daraja jipya la Salender.(Picha na Ikulu).

Habari Leo

UJENZI wa Daraja la Salender litakalounganisha eneo la Coco Beach na eneo Agha Khan kupitia baharini Jijini Dar es Salaam unatarajiwa kuanza Juni Mwakani baada ya Serikali ya Tanzania kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa fedha za ujenzi kutoka benki ya Exim ya Korea.

Rais Dkt John Magufuli amesema hayo leo mfupi baada ya kuzungumza na Balozi wa Jamhuri ya Korea hapa nchini Song Geum-Young, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Amesema ujenzi wa daraja hilo litakalokuwa na urefu wa kilometa 7 zikiwemo kilometa 1.4 zitakazopita baharini, unatarajiwa kukamilika mwaka 2020 na daraja hilo litasaidia kupunguza adha ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.

"Mchakato wa kulijenga hili daraja la Salender unaendelea vizuri kwa sababu hivi sasa kampuni ya Kikorea ambayo inafanya usanifu ipo kwenye hatua za mwisho na zabuni zinategemewa kutangazwa mwezi wa tatu Mwaka kesho na zitakwenda haraka, kwa hiyo mambo yakienda vizuri ujenzi unaweza kuanza mwezi wa sita, bahati nzuri fedha zote zipo na zimeshatolewa na Benki ya Exim ya Korea" Amesema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine Dkt Magufuli amemshukuru Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete kwa juhudi alizozifanya zilizowezesha kujengwa kwa hospitali ya Mloganzila kwa ufadhili wa Jamhuri ya Korea na kwamba hospitali hiyo itakuwa ya kisasa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema ujenzi wa Hospitali hiyo unatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu na kwamba tayari Madaktari na Wataalamu takribani 100 waliopata mafunzo nchini Korea na wenye ujuzi wa namna ya kutumia teknolojia inayowekwa kwenye hospitali hiyo wapo hapa nchini.

Rais Dkt Magufuli ambaye ameelezea nia ya Serikali ya Tanzania kufungua ofisi za Ubalozi Mjini Seoul nchini Korea ameongeza kuwa Serikali yake imedhamiria kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi kwa lengo la kuwaletea manufaa wananchi ikiwemo kutumia teknolojia na ujuzi wa nchi ya Korea katika ujenzi wa Meli.

Kwa upande wake, Balozi wa Korea hapa nchini Mhe. Song Geum-Young ametoa salamu za pole kufuatia maafa ya tetemeko la Ardhi yaliyotokea Mkoani Kagera na mikoa jirani, na ameahidi kuwa Korea itatuma timu ya wataalamu kuja kuona namna ya kusaidia.

Balozi Song Geum-Young pia amemhakikishia Rais Dkt Magufuli kuwa Korea itaendeleza na kuimarisha uhusiano wake na Tanzania na kwamba itatoa ushirikiano wa kutosha kufanikisha miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa hapa nchini ikiwemo ujenzi wa Daraja la Salender, Meli, Hospitali ya Mloganzila na mingineyo.

Wakati huo huo, Rais Dkt Magufuli amekuwa na mazungumzo na Balozi wa Urusi hapa nchini Yuri Popov ambapo viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria baina ya nchi hizo huku wakitilia mkazo katika kukuza biashara na uwekezaji.

Pamoja na hayo Balozi Yuri Popov amepongeza na kuelezea kufurahishwa na hatua zinazochukuliwa na Rais Dkt Magufuli katika kuimarisha uchumi huku akibainisha kuwa kwa hatua hizi anaamini ajenda ya kujenga uchumi wa viwanda itafanikiwa.

Rais Dkt Magufuli pia amepokea taarifa ya hali ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na katika mazungumzo yake na Mkemia Mkuu wa Serikali Prof. Samwel Manyele, amemtaka kuendelea kuimarisha utendaji kazi wa maabara hiyo ili kuongeza ufanisi wa majukumu yake ambayo ni kufanyia uchunguzi vielelezo vya makosa ya Jinai na usimamizi wa sheria za udhibiti wa kemikali na udhibiti wa vinasaba vya binadamu (DNA).
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link