Wa kwanza kutoka Kulia anayeshuhudia tukio la makabidhiano hayo ni Mratibu Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za SMZ Mjini Dar es salaam Ndugu Issa Mlingoti Ali.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Meza akiuwasilisha msaada huo wa Mtambo wa mawasiliano ya Simu kwa mlengwa Mratibu Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za SMZ Mjini Dar es salaam Ndugu Mlingoti.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Joseph Abdulla Meza alisema jamii na hasa wananchi Wazalendo wenye uwezo wanapaswa kuendelea kujenga tabia ya kusaidia nguvu katika kupambana na changamoto zinazoikabili serikali pamoja na wananchi katika maeneo mbali mbali nchini.
Alisema mfumo uliozoeleza kwa kipindi kirefu sasa katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo ni ule uliotegemewa zaidi wa kupokea misaada kutoka Mashirika, taasisi na mataifa ya nje ya nchi.
Ndugu Joseph Abdulla Meza alitoa kauli hiyo wakati akipokea msaada wa mtambo maalum wa mawasiliano ya ndani { Inter call }kwa ajili ya Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za SMZ Mjini Dar es salaam uliotolewa na Uongozi wa Hoteli ya Kendwa Rocks Nungwi hafla iliyofanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema wakati umefika kwa wananchi wenyewe kurejesha ari iliyowahi kutekelezwa miaka ya nyuma katika nia ya kujenga nchi kwa kushirikiana kwenye Nyanja zote zinazohusika za kujenga Taifa lenye nguvu za Kiuchumi, maendeleo na ustawi wa Jamii.
{ Tumezoea kupokea misaada kutoka nje ya nchi lakini ni vyema tukapaswa kujenga tabia ya Wananchi wenyewe kusaidia changamoto zinazotukabili sisi pamoja na Serikali yetu “. Alisema Nd. Meza.
Katibu Mkuu huyo wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushukuru Uongozi wa Hoteli ya Kendwa Rocks kwa uamuzi wake wa kusaidia nguvu za kiuwezeshaji changamoto zinazozikabili baadhi ya Taasisi za Umma Nchini.
Mapema Meneja Mkuu wa Hoteli ya Kendwa Rocks Nd. Ali Ibrahim Kilupi alisema Taasisi yake imeamua kutoa Mtambo huo ili kuwasaidia watendaji wa Ofisi ya Uratibu wa shughuli za SMZ kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Nd. Kilupi alisema ufungwaji wa Mtambo huo wenye njia 24 za mawasiliano ya ndani pia utagharamiwa na Kampuni hiyo mara baada ya kupata maelekezo kutoka kwa Uongozi wa Ofisi hiyo muhimu iliyokuwa kiungo kati ya SMZ na washirika wake waliopo Tanzania Bara na Nje ya Tanaznia.
Akipokea msaada huo Mratibu Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za SMZ Mjini Dar es salaam Ndugu Issa Mlingoti Ali alisema inatia moyo kuona wafanyabiashara wanaanza kufahamu na kuheshimu maamuzi yaliyofanywa na Serikali ya kuanzisha Ofisi ya Uratibu Mjini Dar es salaam.
Nd. Issa alizitaka Taasisi, Mashirika na Watu wenye nia njema waendelee kuunga mkono juhudi za Serikali za kuanzisha Ofisi hiyo ambayo ni kiungo kati ya SMZ na Wananchi wanaopaswa kuitumia katika harakati zao za Kiuchumi na Kibiashara.
Mratibu Mkuu huyo wa Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za SMZ Mjini Dar es salaam aliwaomba Wazanzibari, Wananchi wa Tanzania Bara na hata wageni wa Mataifa ya Kigeni wanaoishi Tanzania kuitumia Ofisi hiyo kama kiungo wakati wanapohitaji huduma kupitia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamua kuanzisha Ofisi hiyo ya Uratibu kwa lengo la kuwapunguzia urasimu wa mawasiliano ya masafa kwa Watu, Taasisi na Mashirika ya nje ya Zanzibar yaliyopo Tanzania Bara.
Mtambo wa Mawasiliano ya Simu za Ndani { Inter Call } uliotolewa msaada ya Uongozi wa Hoteli ya Kendwa Rocks pamoja na ufungaji wake utagharimu jumla ya shilingi Milioni 3,200,000/-.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar