Muonekano
wa Barabara wa Dodoma-Mayamaya yenye urefu wa KM 43.65 ikiwa katika
hatua za mwisho za ujenzi wake. Barabara hiyo inatarajiwa kukamilika
mwezi Novemba Mwaka huu.
Meneja
Mradi wa Barabara ya Dodoma-Mayamaya yenye urefu wa KM 43.65 Eng. Yusuf
Karera, akitoa maelezo ya hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara hiyo
kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa
(wa tatu kushoto), alipokagua ujenzi wake, Mkoani Dodoma.
Muonekano
wa tabaka la kwanza la Barabara ya Dodoma-Mayamaya yenye urefu wa KM
43.65 ambayo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akiweka
mchanga katika tabaka la kwanza la ujenzi wa barabara ya Dodoma-Mayamaya
yenye urefu wa KM 43.65 alipokagua mkoani Dodoma.
…………………………………………………………..
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka
Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya Sinohydro Corporation anayejenga
barabara ya Dodoma-Mayamaya yenye urefu wa kilometa 43.65 kukamilisha
ujenzi huo ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Akizungumza
mara baada ya kukagua barabara hiyo mkoani Dodoma na kuridhishwa na
ujenzi wake Prof. Mbarawa amesema kuwa barabara hiyo ni muhimu kwani ni
kiungo kikuu kwa watu wanaosafiri kati ya mkoa wa Dodoma, Manyara,
Arusha na nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika.
“Kamilisheni
kipande hiki kilichobaki haraka kwani barabara hii ni kiunganishi cha
nchi za Kaskazini na Kusini mwa bara la Afrika hivyo kukamilika kwake
kutasaidia kufungua fursa za kibiashara na kukuza uchumi wa nchi”,
amesema Waziri Mbarawa.
Amemtaka
mkandarasi huyo kuzingatia viwango bora vya ujenzi wa barabara kama
ilivyosainiwa kwenye mkataba na kuhakikisha thamani ya fedha katika
ujenzi huo unaonekana.
Naye,
Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Dodoma Eng.
Leonard Chimagu amemhakishia Waziri huyo kusimamia barabara hiyo kwa
mujibu wa sheria za barabara ikiwemo kuzuia wananchi wasivamie
miundombinu ya barabara na kuzuia mifugo kuswagwa kwenye barabara.
“Nahakikisha
nitasimamia sheria za barabara, kwani mradi huu ni mkubwa na Serikali
imetumia gharama kubwa katika ujenzi wake, hivyo ni lazima niutunze ili
kudumu muda mrefu”, amefafanua Eng. Chimagu.
Barabara
ya Dodoma – Mayamaya ni sehemu ya mradi mzima wa barabara ya Dodoma –
Babati yenye urefu wa kilometa 188.15 na umegharimu shilingi bilioni 40.