Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando
POLISI mkoani Rukwa inamshikilia Diwani wa Kata ya Izia, Manispaa ya Sumbawanga, Pascal Silwimba (41) kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)na mkewe Doris Karusu (36) baada ya kukutwa wakimiliki bunduki aina ya gobori bila kibali na bangi yenye uzito wa robo kilo .
Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema wanandoa hao walikamatwa Oktoba 13, mwaka huu saa tatu asubuhi baada ya msako mkali uliofanyika ndani ya soko kuu lililopo mjini Sumbawanga.
“Watuhumiwa ambao ni mume na mke, walikutwa wakimiliki bunduki aina ya gobori ambayo si tu haijasajiliwa lakini pia walikuwa wakiimiliki bila kibali pia walikutwa na bangi yenye uzito wa robo kilo… vitu hivi vimepatikana baada ya duka lao lililopo ndani ya soko kuu mjini …,” alieleza.
Kamanda Kyando alisema polisi mkoani humo imejipanga kupambana na uhalifu wowote na kutoa mwito kwa wale ambao wanatumia siasa kama kificho kuwa watafuatiliwa na kuchunguzwa bila kujali wadhifa alionao kisiasa.
Kamanda Kyando alisema watuhumiwa wote wawili wamekiri kupatikana na vitu hivyo dukani mwao na kwamba upelelezi wa awali kuhusu tuhuma hizo umekamilika ambapo watafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Imeandikwa na Peti Siyame, Sumbawanga | Habari Leo