Home » » Serikali yakanusha kuanza kuajiri

Serikali yakanusha kuanza kuajiri

Written By CCMdijitali on Sunday, October 2, 2016 | October 02, 2016

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika utumishi wa Umma, Xavier Daudi

Imeandikwa na Hellen Mlacky | Habari Leo

SEKRETARIETI ya Ajira katika utumishi wa Umma imesema serikali bado imesitisha ajira mpya wakati huu ikiendelea kufanya uhakiki wa watumishi wake pamoja na kupitia upya miundo yake.

Imesema kazi hiyo haijakamilika na kutaka wanaopenda kuajiriwa katika utumishi wa umma kusubiri mpaka pale watakapotangaza kukamilika kwa shughuli ya uhakiki.

Kauli hiyo imetolewa na katibu wa sekretarieti hiyo, Xavier Daudi jana wakati akikanusha taarifa ya tangazo la nafasi za kazi zaidi ya 1,000 serikalini lililosambaa mitandaoni.

“Kama mnavyofahamu serikali ilitoa taarifa ya kusitisha kwa muda ajira mpya serikalini kwa ajili ya kufanya uhakiki wa watumishi wake pamoja na kupitia upya miundo yake, hivyo mpaka sasa mambo hayo yanaendelea na hayajakamilika kwa maana usitishwaji wa ajira bado unaendelea,” alisema.

Katibu huyo aliwataka wadau wote kuvuta subira kipindi hiki wakati uhakiki wa watumishi hewa unapoendelea kufanyika na utakapokamilika na taarifa rasmi ya nafasi wazi za kazi serikalini itatolewa na mamlaka husika hivyo wasikubali kupotoshwa na watu wachache .

Alisema kikundi cha watu kwa makusudi wameamua kusambaza taarifa za uongo katika mitandao ya kijamii kuanzia Septemba 29 kuwa Sekretarieti ya ajira imetangaza nafasi hizo za kazi zaidi ya 1000, zikiwemo za Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Mtendaji Mkuu wakala wa Misitu Tanzania (TFS ) .

Daudi alisema mtu aliyeanzisha uzushi huo aliingia kwenye tovuti ya Sekretarieti ya ajira na kuchukua matangazo ya Julai 9, mwaka jana, kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili ambayo yalikuwa na jumla ya nafasi 599 na lingine lilikuwa na nafasi za kazi 513.

Aliwataka wananchi kupuuza taarifa kama hizo za uzushi zinapotokea kwani matangazo ambayo hutolewa na Sekretarieti hiyo ni lazima yaonekane kwenye tovuti yake ya www. ajira.go.tz au portal ya ajira ambayo ni portal. ajira.go.tz .


KUKANUSHA TAARIFA YA TANGAZO LA NAFASI ZA KAZI ZAIDI YA 1000 SERIKALINI LILILOSAMBAA MITANDAONI

Kama mnavyofahamu hivi karibuni Serikali ilitoa taarifa ya kusitisha kwa muda Ajira mpya Serikalini kwa ajili ya kupisha zoezi la uhakiki wa Watumishi wake pamoja na zoezi la kupitia upya miundo yake, mazoezi haya mpaka sasa yanaendelea na hayajakamilika hivyo zoezi la usitishwaji wa Ajira bado linaendelea.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida kuna mtu ama kikundi cha watu kwa makusudi wameamua kusambaza taarifa za uongo tarehe 29 Septemba, 2016, inayodai ''Sekretarieti ya Ajira kutangaza nafasi wazi za kazi zaidi ya 1000'' ikiwataka watanzania wenye sifa na uwezo kujaza jumla ya nafasi wazi za kazi 1,101. Aidha, taarifa hiyo imebainisha kuwa nafasi hizo ni kwa ajili ya Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii na Mtendaji Mkuu Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na kuzisambaza katika baadhi ya mitandao ya kijamii ikiwemo ''Facebook na WhatsApp'' huku wakijua taarifa hiyo haina ukweli wowote, hali ambayo imeleta usumbufu kwa jamii na Serikali kwa ujumla.

Napenda kuwajulisha kuwa mtu aliyeanzisha uzushi huo aliingia kwenye tovuti ya Sekretarieti ya Ajira na kuchukua matangazo ya mwaka jana yaliyotolewa tarehe 9 Julai, 2015 kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili yaliyokuwa na Kumb.Na. EA.7/96/01/H/56 ambayo yalikuwa na jumla ya nafasi za kazi 599 pamoja na tangazo lenye Kumb.Na. EA.7/96/01/H/57 lililokuwa na nafasi wazi za kazi 513. Alichofanya mtu huyo mwenye dhamira mbaya ni kuyafanyia mabadiliko katika tarehe za kutangaza, ambapo matangazo yote mawili yalikuwa yametolewa na Taasisi hii kwa niaba ya waajiri wanne tofauti ambao ni Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Baada ya kugundua upotoshaji huo, Ofisi yangu jana tarehe 30 Septemba, 2016 ilitoa taarifa za awali za kukanusha. Kutokana na unyeti wa suala hili bado nimeona kuna umuhimu wa kukutana na nyie moja kwa moja kama wadau muhimu katika utoaji wa taarifa ili muweze kutambua uzushi huo ambao umezua taharuki kwa jamii na kuleta usumbufu mkubwa kwa Wananchi, ili muweze kufikisha taarifa sahihi kwa Wananchi.

Aidha, kutokana na taarifa hizi za kupotosha Umma tunaomba mtusaidie kuwataarifu wananchi kuzipuuza taarifa hizi, kwa kuwa Matangazo yote ambayo hutolewa na Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni lazima yaonekane kwenye Tovuti ya Sekretarieti ya Ajira www.ajira.go.tz au portal ya Ajira ambayo ni portal.ajira.go.tz. Hivyo, tunapenda kuwataarifu wadau wetu kuwa wanapoona matangazo kama hayo kabla ya kuyafanyia kazi wajiridhishe kama kweli yametolewa na Taasisi hii kwa kufungua Tovuti ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma. Uhakiki huo wa taarifa zinazotolewa kwenye mitandao mingine utawasaidia sana kuondokana na usumbufu usio wa lazima.

Nichukue fursa hii kuwahakikishia wadau wetu kuwa tunaendelea kufuatilia vyanzo vya upotoshaji huu kwa kushirikiana na Vyombo vingine ili kumbaini ama kuwabaini wale wote walioshiriki kufanya upotoshaji huu kwa jamii ili kuweza kuwachukulia hatua kwa mujibu wa Sheria. Tunapenda kuwaomba radhi kwa niaba ya Serikali wananchi na wadau wetu wote waliopata usumbufu kwa namna moja ama nyingine huku tukiwataka wadau wetu kuendelea kuvuta subira kwa kipindi hiki ambapo zoezi la kuhakiki watumishi hewa linafanyika hadi pale zoezi hilo litakapokamilika na taarifa rasmi ya nafasi wazi za kazi Serikalini itatolewa na Mamlaka husika, hivyo wasikubali kuendelea kupotoshwa na watu wachache pasipokuwa na sababu za msingi.

Imetolewa na;

Xavier M. Daudi

Katibu

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma

1 Oktoba, 2016



Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link