Wa kwanza kutoka Kushoto ni Mke wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Mama Asha Suleiman Iddi na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Issa Juma.
Mbunge wa Jimbo la Mahonda Mh. Bahati Ali Abeid akitoa ahadi kwa walimu na wanafunzi wa Skuli ya Msingi Mangapwani ya kusaidia ujenzi wa mnara wa Tangfi la Maji kwenye Kisima cha Skuli hiyo ili kuwaondoshea usum,bufu wanafunzi wake.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu, Maandalizi na Msingi Bibi Safia Ali Rijali akiushukuru Uongozi wa Jimbo la Mahonda kwa hatua unaochukuwa wa kusaidia sekta ya elimu.
Baadhi ya Wanafunzi wa skuli ya msingi ya Mangapwani wakishuhudia hafla ya skuli yao kukabidhiwa madeski 50 kutoka kwa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif hayupo pichani yaliyotolewa msaada ya Kampuni ya Simu ya Tigo.
Baadhi ya Madeski 50 yaliyokabidhiwa skuli ya msingi Mangapwani kutoka kwa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif kwa msaada wa Kampuni ya Tigo.
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi Shilingi Milioni 1,000,000/- kwa Mshika Fedha wa Kikundi cha Ushirika cha Msitupumbaze cha Mtaa wa Kiduka Njaa Mangapwani Bibi Asha Muhsin Hassan kukamilisha ahadi aliyotoa wiki iliyopita ya kusaidia kukamilisha jengo la ufugaji wa mbuzi wa maziwa la wanaushirika hao.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amemuonya Mtu aliyeamua kuvamia Eneo la Skuli ya Msingi ya Mangapwani kwa ajili ya Ujenzi wa Nyumba kuacha mara moja mpango huo ili kuepuka hasara inayoweza kumtokea hapo baadaye.
Alisema Serikali kupitia Taasisi zake zinazosimamia ujenzi na masuala ya Ardhi hazitasita kumvunjia mtu huyo endapo ataamua kukaidi onyo hilo kutokana na kuonyesha dalili za mapema za kuweka mawe kwenye eneo hilo kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi huo.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo wakati akikabidhi Madeski 50 yenye Thamani ya Shilingi Milioni 9,000,000/- aliyopewa Msaada na Uongozi wa Kampuni ya Mtandao wa Simu za Mkononi wa Tigo kwa ajili ya Skuli ya Msingi Mangapwani ndani ya Jimbo la Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Balozi Seif katika hafla hiyo pia akakabidhi msaada wa Mashine Moja ya Fotokopi na Mbunge wa Jimbo hilo la Mahonda Mh. Bahati Ali Abeid akakabidhi msaada wa Kompyuta Moja na Printa yake kwa Skuli hiyo vyote vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 4,540,000/.
Alisema tabia ya baadhi ya Watu kuamua kuvamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za Kijamii kama Vituo vya Afya na Skuli inayoonekana kuongezeka kila siku katika maeneo mbali mbali hapa nchini inaondosha utulivu wa walimu na wanafunzi kiasi kwamba kwa sasa inastahiki kudhibitiwa.
Balozi Seif alisema Ardhi ni mali ya Serikali, hivyo Taasisi zinazosimamia ardhi na Mipango Miji ndizo zenye jukumu na wajibu wa kupima maeneo yote na baadaye kuyagawa kwa Wananchi na Miradi ya Jamii kwa mujibu wa mahitaji halisi ya matumizi ya ardhi husika.
Katika kuunga mkono jitihada za Walimu, Wanafunzi na Kamati ya Skuli ya Msingi Mangapwani Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda ameahidi kutoa mchango wa Kompyuta Mbili zitakazowasaidia walimu na wanafunzi hao katika masomo yao ili kwenda sambamba na mabadiliko ya sasa ya sayansi na Teknolojia.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mahonda Mh. Bahati Ali Abeid aliuagiza Uongozi wa Kamati ya Skuli ya Msingi Mangapwani kushirikiana na Sheha wa Shehia hiyo kuanza hatua za awali za kutafuta Hati Miliki ya Eneo la Skuli hiyo na uongozi wa Jimbo hilo utakuwa tayari kusaidia nguvu za uwezeshaji katika upatikanaji wa Hati Miliki hiyo.
Mh. Bahati alisema udhaifu mwingi unaoendelea kufanywa na baadhi ya Kamati za Skuli mbali mbali Nchini ndio unaotoa mwanya kwa wajanja kuzaa mbinu za kushirikiana na matapeli mitaani kuuza au kukata viwanja ndani ya Maeneo yaliyotengwa na Serikali kwa shughuli maalum za Kijamii.
Mbunge huyo wa Jimbo la Mahonda katika kuchangia nguvu za kupunguza changamoto zinazoikabili skuli hiyo ya msingi Mangapwani likiwemo tatizo la huduma za maji safi na salama aliahidi kusaidia fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mnara wa Tangi kwenye Kisima kilichopo ndani ya Skuli hiyo.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Wizara ya Elimu pamoja na Skuli ya Msingi Mangapwani, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu, Maandalizi na Msingi Bibi Safia Ali Rijali alisema jamii imekuwa ikishuhudia na kufarajika kutokana na kasi kubwa inayofanywa na Balozi Seif Ali Iddi katika kusaidia sekta ya Elimu.
Mkurugenzi Safia alisema jitihada zinazochukuliwa na Viongozi, wahisani pamoja na wananchi katika kuunga mkono mapambano dhidi ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto za Sekta ya Elimu zinatoa mwanga wa kusaidia Watoto katika kujitafutia Taalum inayokubalika.
Alisema nguvu za utengenezwaji wa madeski katika maeneo tofauti nchini zinazofanywa na Viongozi hao pamoja na washirika wa maendeleo zinawapa fursa nzuri walimu kuwasomesha wanafunzi wao katika utulivu mkubwa.
Skuli ya Msingi Mangapwani yenye Madarasa kuanzia la kwanza hadi la saba iliyofungulia rasmi Tarehe 3 Septemba mwaka 2007 na wanafunzi wake kuanza kufanya Mitihani ya Taifa ya Darasa la Saba kuanzia mwaka 2011 hivi sasa ni miongoni mwa skuli ya Msingi Wilaya ya Kaskazini “B” inayofanya vizuri katika kutoa wanafunzi wa mchepuo wa darasa la Tisa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
07/10/2016.
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
07/10/2016.