Home » » Ujenzi meli 2 za mizigo kukamilika mwezi huu

Ujenzi meli 2 za mizigo kukamilika mwezi huu

Written By CCMdijitali on Wednesday, October 19, 2016 | October 19, 2016

Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Transport Boatyard, Salehe Songoro
 
KAMPUNI ya Songoro Marine Transport Boatyard imeihakikishia Serikali kuwa meli mpya mbili za mizigo zinazoendelea kujengwa katika Bandari ya Itungi wilayani Kyela mkoani Mbeya zitakuwa zimekamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Salehe Songoro amesema ifikapo Oktoba 30, mwaka huu kampuni hiyo itaziingiza meli hizo mbili za mizigo ndani ya ziwa Nyasa tayari kwa safari za majaribio.

Alitoa uhakika huo juzi baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla kufanya ziara ya kushitukiza bandarini Itungi akilenga kufuatilia ujenzi huo wa meli mpya.

Mkurugenzi huyo alisema kwa sasa ujenzi wa meli mbili za mizigo umefikia zaidi ya asilimia 80, hivyo kazi zilizosalia ni za umaliziaji ikiwemo upakaji rangi na tayari meli hizo zimepewa majina ya Mv Ruvuma na Mv Njombe.

Alisema meli ya abiria ambayo ujenzi wake utakamilika Februari mwakani itapewa jina la Mv Mbeya II kwa kuwa jina la Mv Mbeya liliwahi kutumika miaka ya nyuma katika meli iliyozama ndani ya Ziwa Nyasa miaka mingi iliyopita.

“Mv Mbeya II tayari ujenzi umeanza kwa vipande vipande lakini tunataraji baada ya hizi meli mbili za mizigo kuingizwa ziwani ndipo tutapata nafasi ya kutosha kwaajili ya kuanza ujenzi mkubwa wa meli hiyo ya abiria itakayokuwa na uwezo wa kuchukua abiria miambili na tani miambili za mizigo kwa wakati mmoja,” alisema Songoro.

Akitoa tathmini yake baada ya ziara hiyo, Makalla alisema ameridhishwa na hatua za ujenzi huo na kuwa ana imani kuwa ahadi ya kuziingiza ziwani meli mbili za mizigo mwishoni mwa mwezi huu itatimizwa.

"Nimejionea kila kitu tayari kimefungwa. Injini, vyumba vya kuongozea vyote viko tayari. Kazi zilizosalia ni kidogo ambazo kama kasi itaendelea hivi ifikapo mwisho wa mwezi huu zitakuwa zimekwisha na mimi nitakuja kushiriki siku ya majaribio,” alisema Makalla.

Alisema tayari wadau mbalimbali wa kibiashara wameanza kuonesha nia ya kutumia usafiri huo mara tu utakapoanza kutoa huduma.

 Imeandikwa na Joachim Nyambo, Kyela    | Habari Leo


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link