WASOMI wa fani ya uchumi nchini, wametaja mambo yaliyochangia fedha kupotea kwenye mzunguko, tofauti na kauli ya Rais John Magufuli, kuwa huenda kuna watu wamezificha majumbani.
Huku wakitaka utafiti ufanyike kuhusu hali hiyo, wasomi hao wamesema hali hiyo pia imechangiwa na hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano, kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Profesa Humphrey Moshi alisema kutokana na hatua hizo, watu wako makini kwenye matumizi, kwa sababu fedha zinapatikana kwa wanaofanya kazi tu na ndiyo maana hazionekani mitaani.
“Watu wamekuwa makini katika utoaji na utumiaji wa fedha zao, mtu hawezi kutoa fedha tu wakati hazalishi, zamani kabla ya kuingia Rais John Magufuli, fedha zilikuwa zinazagaa kwa kuwa kulikuwa na mianya mingi ya kupiga ‘dili’,’’ alisema.
Alitaja mambo yanayosababisha kupotea kwa fedha mtaani, kuwa ni pamoja na kusitishwa kwa safari za nje kwa watumishi wa umma, ambazo kwa mujibu wa Profesa Moshi, safari hizo zilikuwa zikiwapa watu fedha za ziada.
Alitaja hatua ya Serikali kukabiliana na watumishi hewa waliogundulika, kwamba kabla ya hapo tatizo hilo lilisababisha watu kupata fedha kwa njia zisizo halali na kuzitumia hovyo mitaani.
“Pia kuna wafanyabiashara waliokuwa wakiingiza bidhaa bila kulipia kodi, nao walikuwa wanatumia fedha vibaya ndiyo maana zilikuwa zinazagaa tu na watu wanafanya starehe,’’ alisema.
Profesa Moshi alisema baada ya hatua hizo za Serikali ambazo zinaendelea, kwa sasa ili mtu apate fedha, ni lazima afanye kazi na kinachotakiwa si wananchi kulalamika, bali kujitahidi kutafuta njia za kujiingiza kipato.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi alisema hata kudorora wa shughuli za uchumi na kodi kubwa, vinaweza kupunguza fedha mifukoni, hivyo ni vyema kufanyie utafiti utakaosaidia kutoa majibu mazuri.
Kwa mujibu wa Profesa Ngowi, hata riba kubwa ya kukopa benki inaweza kupunguza fedha mitaani kwa kuwa zina tabia ya kukatisha tamaa wakopaji.
Alisema riba ya kuweka fedha benki nayo ikiwa kubwa, huvutia watu kuweka fedha benki badala ya kuziacha kwenye mzunguko, lakini hata sera za kifedha za kupunguza fedha kwenye mzunguko kwa sababu mbalimbali kama vile kupunguza mfumuko wa bei, nazo huchangia kupunguza fedha.
“Lakini pia fedha zinaweza kuondolewa kwenye mzunguko na watu kwa sababu kadhaa na kwa njia tofauti, ili hali hiyo ijitokeze na kutetemesha uchumi, lazima wawe watu wengi wanaofanya hivyo au wachache wenye fedha nyingi,” alisema.
William Shao | Jambo Leo