Home » » Wazee walindwe, uzee hauepukiki

Wazee walindwe, uzee hauepukiki

Written By CCMdijitali on Tuesday, October 18, 2016 | October 18, 2016

“WAZEE ni Hazina ya Taifa, tuwatunze na kuwatumia.” Hii ni kauli ambayo imekuwa ikitamkwa na viongozi mbalimbali nchini wakiwemo vyama vya kisiasa, asasi za kiraia na hata wale wa dini. Msingi wa kauli hii ni kuihimiza jamii kutambua umuhimu wa uwepo wa wazee. Nchini Tanzania kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, kuna wazee wapatao 2,507,508. Hii ni sawa na asilimia 5.6 ya watanzania wote.

Kati ya wazee hao 1,307,358 ni wanawake na 1,200,210 ni wanaume. Sera ya Wazee ya mwaka 2003, inaelekeza kuwa mzee ni mtu yeyote aliye na umri usiopungua miaka 60. Inasisitiza pia kuwatumia wazee kama Hazina ya Taifa na kwamba mchango wa wazee unatakiwa kutumiwa katika kuleta maendeleo.

Ni sera hii pia inayoelekeza kuweka mazingira mazuri ya kuwalinda na kuwatetea wazee siku zote za maisha yao ikiwemo dhidi ya vitendo vya unyanyasaji.

Oktoba mosi ya kila mwaka kama ilivyokuwa mwaka huu ilikuwa ni Siku ya Wazee duniani. Maadhimisho ya siku hii ni moja ya jitihada za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) katika kuhakikisha nchi wanachama wa umoja huo, ikiwemo Tanzania zinatambua na kuhamasisha jamii kuwaenzi wazee kama njia mojawapo ya kulinda, kuhifadhi, kukuza na kutetea haki za wazee katika jamii zao.

Ni maadhimisho haya pia ambayo yanatoa fursa kwa mataifa yote duniani kutafakari hali ya maisha ya wazee katika nchi zao na kuangalia upungufu uliopo na kuweka mipango mahsusi ya kushughulikia kundi hili muhimu kwa kuboresha maisha yao na kuwafanya wazee kuishi maisha ya heshima kwa kuwapatia mahitaji yao muhimu.

Kwa mwaka huu maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani hapa nchini yalifanyika katika mji wa Rujewa wilayani Mbarali mkoani Mbeya. Yalihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo makundi yaliyowakilisha wazee kutoka pande mbalimbali za nchi. Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ndiye aliyekuwa mgeni rasmi. Kaulimbiu ya mwaka huu ilikuwa ni ‘Zuia unyanyasaji dhidi ya Wazee.’

Waziri huyu mwenye dhamana ya Wazee, anasema licha ya jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na serikali katika kuwalinda na kuwaenzi wazee nchini bado wazee hasa walio vijijini wanafanyiwa vitendo vya unyanyasaji na ukatili.

Vitendo hivi anasema, siyo tu vinarudisha nyuma ustawi wa wazee bali pia kuwanyima haki yao ya msingi ya kuishi.

“Kinachosikitisha zaidi, vitendo hivi vinafanywa katika jamii zetu, katika koo zetu na katika kaya zetu. Na vinafanywa na watu wenye wajibu wa kuwalinda wazee hawa wengine wakiwa ndugu zao wa karibu! “Yaani ni jambo la kushangaza sana eti tunaowanyanyasa wazee ni sisi wanafamilia wenyewe.

Ni ama watoto wao, wajukuu wao au wengine wa karibu lakini hakuna mnyanyasaji anayetoka mbali,” anasema Mwalimu.

Anasema matukio ya unyanyasaji dhidi ya wazee na vikongwe hapa nchini ni jambo linalohuzunisha sana na kutia doa kwa Tanzania, nchi ambayo imekuwa ikijivunia amani, upendo na ustaarabu tangu enzi za mababu. Vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya wazee vinavyoongoza nchini Tanzania ni pamoja na mauaji ya wazee (vikongwe), hasa wanawake.

Takwimu za mwaka 2009 zinaonyesha kwamba wastani wa wazee 517 walikuwa wanauawa kila mwaka katika baadhi ya mikoa hapa nchini. Mikoa inayotajwa kuongoza kwa mauaji hayo ni Tabora, Geita, Mwanza na Shinyanga.

Taarifa za Wizara ya Mambo ya Ndani ya mwaka 2013 nayo ilionesha idadi ya wazee wanaouawa ilikuwa wastani wa wazee 500 kwa mwaka, idadi ambayo ni kubwa na pia jambo linaloashiria mabadiliko madogo.

“Ningependa kutumia maadhimisho haya kuitaka jamii ya watanzania kutafakari kwa pamoja maswali yafuatayo: Je, tunayo sababu yoyote ya msingi ya kufanya mauaji haya ya kikatili kwa wazee? Ni kwa nini tuwaue wazee wetu tena wasio na hatia? Je, ni wapi tunapotaka kuipeleka Tanzania endapo tutaacha kuwalinda na kuwaheshimu wazee wetu, wazazi wetu, rafiki zetu, babu na bibi zetu?”Alihoji Waziri Mwalimu.

“Wazee wana haki ya kuishi kama raia wengine. Hivyo wakati tunatafakari masuala haya napenda kuwathibitishia wazee wote Tanzania kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dk John Magufuli itaendelea kuchukua hatua za kisera na kisheria kuhakikisha wazee wanalindwa na vitendo vyote vya unyanyasaji na kikatili, ikiwemo vitendo vya mauaji ya wazee vinakoma.” Anasema sababu kubwa ya vitendo hivi ni imani potofu na uelewa mdogo ndani ya jamii, hivyo anasema serikali haina budi kuendelea kuelimisha wananchi ili kufahamu nafasi ya wazee katika jamii.

Anasema jamii ina wajibu wa kutambua kuwa wazee ni hazina, wana maarifa ya miaka mingi, ujuzi, hekima na busara ambavyo vina thamani kubwa katika malezi, makuzi, maendeleo na uongozi katika jamii na hivyo ni lazima watambulike.

Anahimiza jamii itambue kuwa ni wazee hawa walioweka misingi imara ya uwepo wa Tanzania na maendeleo ya Tanzania.

“Ni wazee hawa waliolima na kuchunga mifugo, wengine katika maisha yao yote ya ujana ili ili kuwezesha watoto wao kupata japo mlo mmoja wa siku.

Ni wazee wetu waliotembea umbali mrefu pengine bila maji wala chakula kwa sababu ya kupigana vita au kujishughulisha na shughuli za ulinzi na usalama wa Tanzania ili kuhakikisha uwepo wa Taifa letu,” anasema.

“Na hata baada ya Uhuru, hawa tunaowaita wazee ndio wameendelea kujitoa kwa hali na mali katika kuleta maendeleo ya familia zao, jamii zao na ya nchi yao kwa ujumla. Hivi bila wazee kuna vijana? Je, ni kwa vipi tunasahau mapema hivi kuwa bila uzee hakuna ujana? Hivi ni nani miongoni mwetu (kama Mwenyezi Mungu atamjaalia maisha marefu) anayeweza kuukwepa uzee?” Anahoji.

Anasema uzee na kuzeeka hakukwepeki. Kila mtu ni mzee mtarajiwa, hivyo kila mmoja anao wajibu wa kuwaheshimu, kuwalinda na kuwaenzi wazee waliopo na watakaoendelea kuwepo.

Anasema ni wakati kwa jamii, mashirika ya umma, Sekta binafsi na wadau wa maendeleo kuunga mkono jitihada za serikali katika kuhakikisha wazee wapo katika mazingira salama ya kulindwa, kutunzwa na kusaidiwa kupata huduma muhimu kwa ustawi na maisha yao.

Jukumu hili ni la kila mtu. Katika kutokomeza vitendo vya unyanyasaji ikiwemo mauaji ya kikatili dhidi ya wazee, Waziri anasema Serikali imepanga kupeleka bungeni Muswada wa Sheria ya Taifa ya Wazee kabla ya Juni 2017.

Anasema muswada huo sio tu kwamba utaweka adhabu kali kwa wote watakaokutwa na hatia ya kufanya vitendo hivyo bali pia utaweka wajibu wa kisheria kwa watoto, familia kuwalea na kuwatunza wazee wao.

“Ninatoa rai kwa wananchi wote kuwafichua wale wote wanaotenda maovu haya katika jamii yetu ili sheria iweze kuchukua mkondo wake katika kukomesha vitendo vya kuwanyanyasa na kuwaua wazee wetu,” anasema.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makalla anasema sula la kuilinda jamii ya wazee halipaswi kuwa na mikakati ya zima moto wala ya ubabaishaji.

Anasema ni lazima kila mwanajamii ahakikishe anawajibika kuwalinda, kuwalea na kuwatunza wazee ili kuwapa fursa ya kunufaika na rasilimali zilizopo katika taifa lao ambazo kimsingi walizilinda na ndiyo sababu zipo mpaka sasa.

Baadhi ya wazee waliozungumza na gazeti hili wanasisitiza umuhimu wa wazee wote kulipwa mafao ya uzeeni ili kuwawezesha kumudu gharama za maisha.


    Imeandikwa na Joachim Nyambo | Habari Leo

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link