AMANI na utulivu wa Tanzania, umevutia watu zaidi 70 kutoka katika mataifa zaidi ya mataifa 15 duniani, ambao ni wa umoja wa wazungumzaji wa lugha ya Esperanto, kuja nchini kuhudhuria mkutano wa Amani na Maendeleo unaofanyika wilayani Bunda, mkoani Mara.
Mkutano huo ni wa sita kufanyika Afrika, mada kuu ikiwa ni kuhamasisha Amani na Maendeleo, kwani kama hakuna amani katika nchi yoyote ile kamwe maendeleo hayawezi kupatikana.
Hayo yalisemwa jana mjini Bunda na washiriki wa mkutano huo unaoshirikisha zaidi ya mataifa 15, yakiwemo ya mabara ya Asia na Ulaya, ambao walisema Tanzania ni nchi ya amani ndiyo maana wameuleta mkutano wao.
Wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa umoja huo duniani, Stephano Mackgli, walisema Tanzania mkutano huo ulikuwa umepangwa kufanyika Burundi, lakini kutokana na hali tete ya amani iliyoko katika nchi hiyo, walihamishia Tanzania.
Aidha, mjumbe mmoja kutoka katika barani Ulaya, Dk Markus Gabor, alisema amani ya Tanzania ni kubwa na inatakiwa kuigwa na nchi nyingine za Afrika na duniani kwa ujumla.
Awali, akifungua mkutano huo wa wiki moja kwa niaba ya serikali, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili alisema ni jambo la msingi kwa wananchi wote kudumisha amani iliyopo, kwani inaitangaza nchi yetu na kupata sifa ya kutembelewa na wageni kutoka mataifa ya mabara mbalimbali duniani, hivyo kusisitiza amani iliyopo ni tunu kwa taifa.
Mwenyekiti wa umoja wa watu wanaozungumza Lugha ya Esperanto nchini, Mramba Nyamkinda, alisema mkutano huo unafanyika Bunda kwa sababu wilaya hiyo ni kitovu cha Esperanto nchini na kuongeza kuwa katika mkutano huo wanajadili mada mbalimbali ikiwemo ya Amani na Maendeleo katika mataifa mbalimbali.